FANYA AGANO NA MACHO YAKO

Biblia kwa kina No Comments

FANYA AGANO NA MACHO YAKO

Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?

Ayubu, ingawa alikuwa ameoa, alijua kwamba macho angeweza kuona au kuangalia vitu ambavyo vinaweza kuathiri uhusiano wake na Mungu. Akaamua kuweka agano kati ya yeye na macho yake yasitazame mabaya.

Agano ni makubaliano, mkataba wa kisheria baina ya pande mbili. Ayubu aliingia agano lisilo la kawaida na kali, kati yake na macho yake.

Mbali na Agano ambalo mtu anaweza akaingia na mume au mke wasitoke nje ya ndoa au wasiachane mpaka kifo, Ayubu alikwenda zaidi ya hapo na kuweka kiwango kipya. Agano hili alilofanya lilikuwa la kipekee. Alifanya makubaliano ya lazima na macho yake ambayo yalihusisha kutomtazama na kutomtamani mwanamke. Sio ajabu hata Mungu alimwambia shetani “Je! Umemwangalia mtumishi wangu Ayubu, ya kuwa hapana mtu kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mnyofu, ambaye humcha Mungu, na kuepukana na mabaya? Na bado anashikilia sana uadilifu wake.” (Ayubu1:3)

Macho ni moja ya njia/lango la kupitisha dhambi ndani ya mtu iwe ameokoka au hajaokoka. Kupitia macho yako unaweza ukajikuta umenajisika na dhambi hususani ya uzinzi, pasipo hata kukusudia au kupanga. Bwana Yesu alisema..

Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu ATAZAMAYE mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mathayo5:27-28)

Unaona hapo Bwana anasema kila “ATAZAMAYE” na sio amgusaye au anayelala naye. Hapana!, Kwa macho yako tu unaweza ukazini na ukafanana na yule aliyelalanaye. Ayubu alijua hilo akasema sasa haya macho ni lazima niwekee mipaka, si kila kitu ni cha kutazama, akafahamu hata kutazama tu msishana kwa kumtamani tayari amezini… hivyo akaweka Agano na macho yake yasitazame.

Dhambi hii ya uzinzi/uasherati inaanzia katika macho, kutamani. Kisha mawazo ya uzinzi na huo ndio uzinzi.

Pale Edeni Hawa alidanganywa na nyoka akashawishika kutenda ile dhambi ya kula tunda aliloagizwa asilile, lakini tunasoma huo ushawishi ulianzia katika macho yake. Alipotazama akatamani na baadaye tamaa ikampelekea dhambi kama tunaposoma katika Yakobo kwamba tamaa huzaa dhambi na kisha mauti (Yakobo2:14-15), ndicho kilichowatokoea wazazi wetu Adamu na Hawa pale bustanini.

Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,

[5]kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.

[6]Mwanamke ALIPOONA ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, WAPENDEZA MACHO, nao ni mti wa KUTAMANIKA kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.

[7]Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.

Zingatia hilo Neno “ALIPOONA”, kumbe angekuwa hajaona asingeweza kutenda hiyo dhambi. Kwahiyo macho yake yalimpelekea atamani hilo TUNDA na mwisho baada ya kuzidiwa na tamaa akajikuta anaizalia hiyo tamaa dhambi.

Ndicho hata sasa anachokifanya shetani, anajua kupitia tu macho mtu anaweza akafarakana na Mungu wake. Na anajua uzinzi unaanzia katika mtu kutazama/kuona na kutamani hivyo amevileta vyanzo vingi vya uzinzi ikiwemo mitandao ya pornography (mikanda/video za ngono), filamu zenye maudhui ya uzinzi, miziki ya kizinzi ili mtu akitazama tu aone watu wanacheza uchi halafu azini moyoni mwake, pia amebuni mavazi yanayochochea uzinzi kwa kasi kubwa kiasi kwamba ukipita njiani unakutana na wanawake wamevaa mavazi ya nusu uchi, mavazi ya kubana na kuchora shepu zao, masuruali na makaputla, hayo yote ni mbinu ya shetani kuwazinisha watu wa Mungu kupitia macho yao.

Sasa usipoweka Agano na macho yako kama alivyofanya Ayubu utaponaje hasa katika kizazi hiki cha zinaa?

Ayubu alizungumza na macho yake na akafanya agano nao. Alitaka kuishi maisha safi, matakatifu, na ya kumcha Mungu, na sisi ni vivyo hivyo hatuna budi kufanya agano na macho yetu. Sio kila mwanamke/binti au kijana mwenye umbo nzuri akipita mbele yako ukodolee macho, angalia mara moja kisha nenda, na wakati mwingine elekeza macho yako mbele bila kugeukageuka nyuma.

Mithali 4:25 Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

Si kila picha, video iwe ni kichekesho au filamu utazame.. kumbuka shetani kama simba angurumaye anazungukazunguka akimtafuta mtu ammeze, hivyo unapopeleka macho yako huko mitandaoni kuwa makini sana…na usijidanganye kuwa wewe ni wa kiroho sana hivyo huwezi kutamani hayo ni mawazo ya shetani.

Kaa mbali na mitandaoni ya Facebook, TikTok, Instagram, n.k kama hauna jambo la maana la kufanya huko ni heri usiingie kabisa au futa kwenye simu yako kabisa.

Agano hili na macho linaweza kufanya kazi tu kwa wale ambao wameokoka au wamezaliwa mara ya pili, kwa kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi.

Lakini kama bado hujampokea Kristo kwa kumaanisha kabisa, uwe na uhakika kwamba siku zote utakuwa katika uzinzi tu na wala hutoweza kushinda kamwe haijalishi utaweka sheria elfu kumi. Macho yako yatakuwa ni yale yaliyojaa uzinzi tu mfano wa watu wa kupindi cha Sodoma na watu wa dunia ya leo wafuatao mwili katika tamaa zao sisizo na kiasi.

2Petro 2:9-14 basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu;

[10]na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka.

[11]Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.

[12]Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao;

[13]Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;

[14]WENYE MACHO YAJAAYO UZINZI, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana;

Hivyo ni heri ukampokea Yesu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zote na namna zote za ulimwengu ili upewe uwezo wa kuzitawala macho yako na kuuweza mwili wako katika utakatifu na heshima kama biblia isemavyo (1Wathesalonike 4:4)

Lakini pia tunaweza tukafanya agano na masikio yetu yasisikilize visivyofaa na ulimi wetu usizungumze mabaya yaani maneno ya uongo, usengenyaji, kiburi n.k kwa msaada wa Roho Mtakatifu tunaweza tukitia bidii.

Je umeokoka? Umempokea Yesu ipasavyo au umempokea kwa namna ile ya kidini? Kama huna huo uwezo wa kuzitawala macho yako na mwili wako, basi huwenda Roho Mtakatifu hajaingia ndani yako au umemzimimisha.

Ikiwa unahitaji msaada wa kupokea Roho Mtakatifu au kujazwa tena na hujui cha kufanya,. basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii nasi tutakupa muongozo utakaokusaidia.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *