Bwana Yesu Kristo Asifiwe
Kuna makundi makuu matatu ya ndoto, Kwa ufupi kidogo tutayaangalia
{1} Ndoto zinazotokana na Shughuli
(muhubiri 5:3)
Hizi ni za mara kwa mara, kwa mfano mtu amefanya Shughuli Fulani kutwa nzima, Sasa anapolala anajikuta anaendelea kuifanya kazi Ile hata ndotoni. Aina hii hailetwi na Mungu Wala Shetani Bali na mwili.
Hii ni kutokana na kazi yake kuchukua sehemu kubwa ya maisha au ufahamu hivyo inaenda kutawala mpaka katika Ulimwengu wa ndoto.
{2} Ndoto zinazotokana na mwovu
Maudhui makuu ya hizi ni kuikana Imani. Hutengenezwa na mwovu na kuziachilia ndani ya mtu kumfanya atende dhambi, Ajitenge mbali na mpango wa Mungu
Sifa nyingine ya ndoto hizi ni kuwa Zina ushawishi mkubwa Baada ya kuamka
Mfano, Mwanandoa (mwanamke) anaota ameachana na Mumewe na kwenda kwa bwana mwingine, baada ya kuamka maisha yanaendelea na anajikuta anaona kero kuishi na Mumewe hivyo anashawishika kuachana na mumewe
Inaweza kuja kwa namna nyingine ya kwamba anaota anafanya uasherati na mtu fulani anayemfahamu au anayemtamani, na baada ya kuamka Ile tamaa inakuwa kubwa zaidi kuliko Mwanzo hivyo kumchochea aingie katika dhambi ya uasherati.
Zitakuja kwa namna nyingi, mtu anaweza kuota kaenda kwa mganga na amefanikiwa au mtu anaota kawa tajiri kwa kucheza kamari au kuiba kwa tajiri wake, mbaya zaidi ni Ile mtu anaota ametenda dhambi ametubu lakini Mungu hajamsamehe, mwisho wa hizi zote baada ya kuamka mazingira yanakushawishi uyafanye Yale uliyo yaota Ambayo yatakutenga mbali na Mungu wako.
Hivyo kwa hayo, ni dhahiri kwamba ndoto za Namna hii ni ndoto zisababishwazo na shetani mwenyewe ili kukufanya ufe kiroho, utende dhambi na ukae nje ya uwepo wa Mungu.
Njia pekee ya kuzishinda ni kukaa Uweponi mwa Mungu kwa kulisoma neno lake na maisha matakatifu.
Maana mishale hiyo ya shetani huja kwa lengo la kukuweka mbali na Mungu, hivyo linapokukuta hauna neno ndani yako hakika atakushinda.
Maandiko yanasema..
1 Yohana 1:9
“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”
Kwa Ile ndoto ya kuachana na mkeo au mmeo ni ya mwovu maana IPO kinyume na Maandiko
Soma
Luka 16:18
“Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.”
Unaweza kuota umetajirika haraka sana baada ya kubeti, lakini unashinda na kujua ni hila za mwovu kwa kuwa una neno la Mungu
Mithali 13:11
” Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.”
Neno la Mungu litakuweka mbali na ndoto hizi, pia na kusali kabla ya kulala itakusaidia kuuondoa upenyo wa mwovu asikuletee ndoto za Namna hii
{3} Ndoto zinazotokana na Mungu
Hizi hutoka kwa Mungu zikiwa na maudhui ya kumuonya au kumuimarisha mtu katika Imani hivyo haziji mara nyingi kama zile Zitokanazo na Shughuli
Mfano ni pale mtu anaota amekutana na mhubiri au rafiki na anamuonya kuhusu maisha yake Maovu, na anapoamka anakuta kweli dhamira yake inamsuta na anaamua kuacha Maovu yake, au Mtu anaota unyakuo umepita na ameachwa! Hivyo anapoamka Anaanza kujichunguza njia zake na kubadilika, wengine huota hata wapo kuzimu.
Inaweza kuja kwa namna hii, mfano mtu anaota kamfanyiwa jambo baya na la kuumiza Lakini anapoamka anagundua yeye ndiye aliyemfanyia mwenzie jambo Hilo hivyo anaumia na kutubu, Au anaota amebaka,ameiba, kacheza kamali, amebeti,amelala na mke wa mtu, Kafanya uasherati, na anapata magonjwa ya kifo kabisa au anahukumiwa kifungo Cha kifo mahakamani. Mtu huyu atakapoamka hawezi kufanya lolote kati ya Yale.
Mungu pia humwonya mtu na mienendo yake mfano, mtu anaota yupo shuleni anafanya mitihani anafeli Kila siku na anapoamka anagundua alishamaliza shule mda mrefu! Hivyo linakuwa onyo kuhusu kwamba yupo nyuma ya wakati na pia hata nyuma katika kumtafuta Mungu.
Sikiliza, Ndoto zinazotokana na Mungu utazijua kama tu neno la Mungu lipo ndani yako, mfano kama ndoto inapingana na neno la Mungu basi unajua ni hila za adui, lakini kama inakuonya na kukurudisha katika mafundisho ya kibiblia basi hiyo ni ndoto kutoka kwa Mungu.
Soma..
Ayubu 33:14-19
14 Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.
15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;
16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,
17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;
18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.
19 Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;”
Na Mungu akubariki sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.