Swali: Mimi naona maono, naoteshwa ndoto, nanena kwa lugha, maombi yangu Mungu ananijibu; Sasa unaponiambia nikabatizwe katika ubatizo sahihi ili unisaidie nini? Kama Roho Mtakatifu si tayari ninaye?
Jibu: Bwana Yesu asifiwe sana. Karibu tujifunze Neno la Mungu ili tuongeze maarifa ya Elimu ya Ufalme wa Mbinguni kama tulivyosisitizwa katika kitabu cha Mithali 4:13.
Neno ambalo ndiyo taa ya miguu yetu na mwangaza wa njia yetu (Zaburi 119:105) limetuasa kama wafuasi wa Kristo basi, wote njia yetu iwe moja katika kumfuata Kristo, yaani tuwe na imani moja, Bwana mmoja, Mungu mmoja, Roho mmoja na zaidi UBATIZO MMOJA. (Waefeso 4:1-6)
Sasa hebu jiulize kama mkristo ni kweli tunaenda sawa na Neno linavyotaka? Hebu jiulize kwanini leo Wakristo hatuna ubatizo unaofanana, wengine wanabatiza watoto wachanga, wengine ubatizo wa kunyunyizia kichwani, wengine ubatizo wa kuzamisha (maji mengi), wengine wanabatiza kwa “jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” na wengine kwa “jina la Yesu Kristo” huku wapo ambao hawabatizi kabisa wakiamini mtu akimkiri Yesu Kristo basi inatosha hayo mengine ni mbwembwe tu.
Ukijiuliza yote hayo utagundua jambo moja kuwa shetani “baba wa uongo” ameshalipofusha Kanisa la Kristo tayari na ule umoja Bwana Yesu alioutaka kwa wafuasi wake (kwenye Waefeso 4:1-6) haupo tena kila mmoja anafanya atakavyo yeye. Lakini leo hatuongelei ubatizo upi ni sahihi kwa sababu tayari tumesha uongelea kwenye tafakari zilizopita (unaweza kuzisoma) ila tunalotaka tuliangalie leo ni hili;
Tunajua kuwa tunapobatizwa tunampokea Roho Mtakatifu lakini kuna mtu alipomuamini na kumkiri Bwana Yesu karama za Roho Mtakatifu zikaanza kujidhihirisha kwake anaona maono, au anatabiri, au ananena kwa lugha, anaombea mtu anapona, anaoteshwa ndoto na Roho Mtakatifu, anaweza kuhubiri na mengineyo ila hajabatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo bado. Tunajua anayefanya yote hayo juu ya mtu ni Roho Mtakatifu, sasa kama huyu mtu ameshampokea Roho unapomuambia lazima akabatizwe katika ubatizo sahihi si ni sawa na kukosa imani? Kwani tunayemuhitaji ni Roho Mtakatifu au maji?
Lazima tujue kwanza kuwa, huduma ya Roho Mtakatifu imegawanyika katika sehemu kuu mbili nazo ni; Roho wa Mungu juu yetu (kutupa karama/vipawa) na Roho Mtakatifu ndani yetu (kutuwezesha kuwa watakatifu na kututia muhuri kuwa warithi wa ule Ufalme wa Mungu katika ulimwengu ujao)
Roho kuwa juu yetu ni kwa ajili ya kutupa uwezo wa kuzidhihirisha Nguvu za Mungu katikati ya watu hasa wasioamini ili waone uweza wa Mungu waamini. Kama vile kuponya wagonjwa, kutabiri, kuona maono, ndoto, kunena kwa lugha, nguvu ya kuhubiri injili ya Kristo n.k.
Kama ingekuwa mtu akiona maono basi hakuna tena haja ya kubatizwa kwa maji mkumbuke Sauli (Mtume Paulo) kwa mara ya kwanza tu alipokutanana na Bwana Yesu na kuamini baada ya hapo alipoomba aliona maono kuhusu Anania, lakini tunaona Anania alipokuja alienda kumbatiza
Matendo Ya Mitume 22:12 Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,
13 Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.
14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.
15 Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.
16 Basi sasa, unakawilia nini? SIMAMA, UBATIZWE, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.
Soma pia (Matendo 9:1-19)
Nyumba ya Kornelio walishukiwa na Roho Mtakatifu kabla ya kubatizwa wakaanza kumuazimisha Mungu na kunena kwa lugha (Matendo 10:44-48) lakini pamoja na hayo Petro alisisitiza ni lazima wabatizwe kwa maji (soma ule mstari wa 47, Matendo 10:47)
Na kama unaona upo na Yesu tayari kwa kuwa ukikemea pepo linatii basi hebu wakumbuke wanafunzi wa Bwana Yesu walipokuja kwake wakifurahi kuwa mapepo wanawatii kwa jina lake lakini Yeye akawaambia wasifurahi kwa kuwa mapepo yanawatii bali wafurahi majina yao yanapoandikwa Mbinguni kwa sababu alijua kuna mtu kama Yuda naye alikuwa akifurahi ametoa pepo kwa jina la Yesu huku ni muovu na jina halipo Mbinguni. (Luka 10:17-20)
Kwahiyo kutoa pepo, kunena kwa lugha, kuota ndoto, maono, kutabiri, kipawa cha kuhubiri na mengineyo visikupe kiburi cha kukataa kubatizwa katika ubatizo sahihi.
Bwana Yesu ndiye aliyetoa agizo hili Yeye mwenyewe, akasema; mtu asipozaliwa mara ya pili KWA MAJI na kwa Roho hatouona Ufalme wa Mungu (Yohana 3:5), aaminiye na KUBATIZWA ataokoka (Marko 16:16), alisema tuenende ulimwenguni kote tuwafanye mataifa kuwa wanafunzi wake na KUWABATIZA kwa jina lake (Mathayo 28:19).
Na ukiidanganya nafsi yako kuwa ulishabatizwa utotoni jiulize kwanini Bwana Yesu aliye kielelezo chetu kwa mambo yote hakubatizwa akiwa mtoto? Kwani Mungu alishindwa kupeleka mtu akambatize akiwa mchanga? Au Yeye mwenyewe ni wapi alipoagiza watoto wabatizwe? Na kama Bwana Yesu ambaye hakuwa na dhambi alinyenyekea akabatizwa na akasema alifanya hivyo ili kuitimiza haki yote ya Mungu (Mathayo 3:13-17) je wewe mwenye dhambi kwanini ukatae kubatizwa? Hutaki kutimiza haki yote ya Mungu unataka kubaki na Wokovu wako wa mazoea?
Kubali ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo utimize haki yote ya Mungu.
Bwana akubariki.