Je ubatizo sahihi ni kwa jina la Yesu au Baba, Mwana na Roho Mtakatifu?

Maswali ya Biblia, Uncategorized 4 Comments

SWALI: Je! wanafunzi wa Bwana Yesu walienda kinyume na Agizo la Bwana wao, alipowaagiza waende ulimwenguni kote wakawafanye mataifa kuwa wanafunzi wake wakiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19), ila badala yake wakaenda kubatiza kwa jina la Yesu Kristo?

JIBU: Jina la Yesu litukuzwe sana. Amani ya Kristo iwe pamoja nawe. Amina

Je! wanafunzi walikaidi agizo la Bwana wao au? Jibu ni hapana bali walielewa ni nini Bwana Yesu alicho kimaanisha kwa kusema vile kuwa, walitakiwa wabatize waaminio kwa Jina la Yesu Kristo.

Sasa ni kivipi?

Jina la Yesu ndilo Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu

  1. Uthibitisho kuwa Jina la Yesu ndilo Jina la Baba.

• Wayahudi walilitambua hilo kuwa Bwana Yesu alikuja kwa Jina la Baba yake na ndio maana walimuimbia “Hosana, Hosana mabarikiwa ajaye kwa Jina la Bwana” Soma (Mathayo 21:9, Marko 11:9, Yohana 12:13)

• Pia Neno  linasema Jina la Yesu alilirithi kutoka kwa Baba yake. “amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao” (Waebrania 1:4) mtu hawezi kurithi chake mwenyewe.

• Yesu mwenyewe alithibitisha hilo kwa kinywa chake. “Nimekuja kwa Jina la Baba yangu wala ninyi hamnipokei…” Soma (Yohana 5:43)

  1. Yesu ndilo jina la Mwana,
    “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Na pia katika injili ya Luka Neno linasema; “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.”
    soma (Mathayo 1:21, Luka 1:31)
  2. Uthibitisho kuwa Jina la Yesu ndilo Jina la Roho Mtakatifu

• Yesu alisema huyo Roho Mtakatifu atakuja kwetu kwa jina lake Yesu. Soma (Yohana 14:26)

• Roho Mtakatifu ni Bwana Yesu mwenyewe “Basi Bwana ndiye Roho”, “kama vile utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho” (2 Wakorintho 3:17,18)

Hivyo wanafunzi walimuelewa Bwana wao alichokimaanisha na ndio maana walibatiza kwa Jina la Yesu Kristo. Hata hivyo ukisoma hapo Mathayo 28:19 amesema KWA JINA na sio KWA MAJINA, hivyo ni wazi kuwa jina moja. Na pia ukisoma (Ufunuo 14:1) inasema “Jina lake na Jina la Baba yake Limeandikwa” umeona hapo? Ni LIMEANDIKWA na SIO YAMEANDIKWA ikimaanisha kuwa ni Jina moja nalo ni “YESU KRISTO”

Kwahiyo shetani amevuruga hapo ndiyo maana leo kama wa Kristo hatuna ubatizo mmoja kama Neno linavyotaka (Waefeso 4:1-6) kila kundi linafanya linavyotaka kutokana na sababu zao wenyewe na nguvu ya ushawishi waliyonayo. Ila wewe kama unapenda kwenda sawasawa na Neno linavyotaka, basi huna budi kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko nao ni wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo.


Matendo ya Mitume 2:38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Pia katika

Matendo ya Mitume 8:16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.

17 Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

Tena katika


Matendo ya Mitume 10:48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

Soma tena

Matendo ya Mitume 19:5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.

Maandiko yote hayo yanaonesha ubatizo ni kwa jina la “Yesu Kristo” na si kwa jina la “Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” kama wengi wanavyofanya maana hapo ni unaeleza sifa za hilo jina lakini hujalitaja jina lenyewe ambalo ni “Yesu Kristo”


Wakolosai 3:17 Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

Bwana akubariki.

4 thoughts on - Je ubatizo sahihi ni kwa jina la Yesu au Baba, Mwana na Roho Mtakatifu?
  1. Ikiwa ubatizo halali ni kubatiza kwa jina la Yesu ; Kwa nini Katika Matayo 28:19 Yesu mwenyewe hakuwatuma waenda wakibatiza kwa jina la Yesu ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *