Je! Ni kweli ubatizo wa maji hauna umuhimu tena?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Je! Ni kweli hatuhitaji kubatizwa kwa maji, kwamba tukimkiri tu Yesu kwa vinywa vyetu inatosha. Hakuna haja tena ya kubatizwa?

Watu wanaoishi kwa dhana hii huwa wametawaliwa na moja kati ya mambo haya matatu au yote kwa pamoja

  1. Yohana alisema “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” (Mathayo 3:11)

Hivyo watu hao husema ubatizo wa Yohana (yaani wa maji) hauna maana tena kwa sababu Bwana Yesu anatubatiza kwa Roho Mtakatifu na ndiye wa muhimu na sio maji.

  1. Kama ubatizo wa maji ni wa lazima je yule mwizi pale msalabani alibatizwa na nani? Na Bwana  Yesu alimuhakikishia kuwa atakuwa naye Peponi (Luka 23:39-43)
  2. Neno linasema ukimkiri Yesu kwa kinywa na kuamini kuwa ndie Bwana na Mwokozi wako utaokoka hivyo ubatizo wa maji sio lazima. (Warumi 10:9)

Dhana zote hizo si sahihi;

Tukianza na dhana ya kwanza ya Yohana, ni kweli Bwana Yesu ndiye atubatizaye kwa Roho wake Mtakatifu ila haimaanishi usibatizwe kwa maji tena. Bwana Yesu mwenyewe alimwambia Yohana imetupasa kufanya hivi ili kuitimiza “Haki yote” (Mathayo 3:13-15) kumbe tunabatizwa katika maji ili kuitimiza haki yote ya Mungu.

Na pia kwa dhana hiyo kama ubatizo wa maji usingekuwa na maana tena baada ya Yeye mwenyewe kuja (Bwana Yesu) na kuanza kazi, basi ni wazi Bwana Yesu asingefanya hivyo (kuwabatiza watu) au kuwafundisha wanafunzi wake jinsi ya kubatiza kwa maji


Yohana 3:26 Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea.

Soma pia Yohana 4:1-2

Na kumbuka hata baada ya Bwana Yesu kwenda Mbinguni alipomtokea Sauli (ambaye ndiye Mtume Paulo) baada ya kuamini alimwambia aende mjini ataambiwa cha kufanya na tunaona alienda kubatizwa na Anania (Matendo 22:16 ila soma kuanzia mstari wa 6-16) hivyo ubatizo bado ni wa lazima. Soma zaidi (Matendo 2:38, 19:1-5,)


Kuhusu yule mwizi aliyesulubiwa pamoja na Bwana Yesu  ni kweli aliokolewa kwa kumuamini na kumkiri Bwana Yesu kwa sababu hakukuwa na nafasi ya yeye kwenda kubatizwa pale, kama ingekuwepo ingempasa naye akabatizwe ila hiyo nafasi haikuwepo, ni kama vile tu leo uende hospitalini kumuhubiria mgonjwa mahututi na akakubali kumpokea Yesu, akaongozwa sala ya toba ila baada ya hapo akafa, sasa utasema hatoenda mbinguni kwasababu hajabatizwa? Hapana. Ila kama angepona ingempasa akabatizwe.

Na pia kuhusu kumkiri Yesu na kumwamini tu, hebu tukumbuke;

Paulo alimwamini Yesu na kumkiri lakini bado alilazimika kubatizwa (Matendo 22:6-16)

Towashi Mkushi alimwamini Yesu na ikampasa kubatizwa (Matendo 8:25-39)

Na pia lile kundi siku ya Pentekoste (watu elfu 3) walimwamini Yesu ikawapasa kubatizwa (Matendo 2:36-41)

Ndugu yangu, Bwana Yesu mwenyewe alisema maneno haya;

Marko 16:16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.

Umeona hapo? Hajasema tu atakayemuamini ataokoka, bali atakaye muamini na kubatizwa. Na pia alimsisitizia Nikodemo katika.

Yohana 3:5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

Umeona tena na hapo? Kumbe ni lazima uzaliwe mara ya pili kwa maji na kwa Roho na si kwa Roho peke yake kama watu wanavyojidanganya sasa hivi. Soma pia (Mathayo 28:19)

Hivyo dhana ya kwamba ukimwamini Bwana Yesu tu na kumkiri inatosha sio dhana sahihi kabisa, Biblia inakataa.

Kumbuka ubatizo sahihi ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo; na anaye batizwa lazima awe na ufahamu wa kutosha kuwa dhambi ni nini na kuwa anapaswa kujitenga na maisha ya uovu na kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu na kuwa hakuna njia nyingine ya kwenda kwa Mungu Mbinguni isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo pekee. Na si ule ubatizo uliobatizwa utotoni, ni ubatizo wa uongo, kama wewe mwenyewe unajiamini kuwa umeshabatizwa na huna haja ya kubatizwa tena basi unajidanganya nafsi yako ndugu, fanya ukabatizwe ukiwa na ufahamu wako, kumbuka lile ni Agano na Mungu, sasa agano gani Mungu anaweza ingia na mtoto mchanga? Acha utani na Wokovu wako ndugu, fanya maamuzi sahihi.

Bwana akubariki.

2 thoughts on - Je! Ni kweli ubatizo wa maji hauna umuhimu tena?

  • Asatesa kwaneno pia na shukurusana ila onilagu mimi kwa wale wakuri tu nihii waache kugeuza neno la Mungu kuwa kama matakwa yao wale ni wapiga kristo na mitume, walehataki kazi zakuwa chosha diyowale waku batiza watoto wadogo waku batiza na maji yakopo pia wana mitari michache ya kujitetea kwa sababu baba yao pia alikuwa na ndogo mbele Ya Bwana wetu Yesu kristo
    Warumi 6:2-6) mate 2:39-41) wagalatia 3 :27 )

LEAVE A COMMENT