Je! umeingia Agano na Mungu?

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Hebu turudi nyuma kidogo kwenye Biblia. Tukisoma kitabu cha (Mwanzo 28) tunaona kuna vijana wawili Yakobo na Esau ambapo tunaona Yakobo anamkimbia Esau asije akamuua kwa sababu ya kumuibia haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Katika safari yake Yakobo anafika mahali jioni ili apumzike kesho aendelee na safari, usiku ule akaona maono ngazi imeanzia duniani hadi Mbinguni, malaika wakipanda na kushuka, kisha akamuona Mungu amesimama juu ya ile ngazi.

Sasa ukisoma pale (Mwanzo 28:13) Mungu anamwambia Yakobo “Mimi ni Mungu wa Baba zako Ibrahimu na Isaka” sasa utajiuliza kwanini Mungu alimwambia hivyo? Kwanini asingemwambia “Mimi ni Mungu wako” bali akasema “wa Baba zako”? Ni kwa sababu lile ni Agano na hakuna mtu anayeingia kwenye Agano na mwingine bila wao kuwa na makubaliano. Ni lazima mtu aamini na aamue kwa hiyari yake kuingia kwenye Agano na Mungu. Yakobo mwenyewe analithibitisha hilo (Mwanzo 28:20-21)

Hebu mwenyewe jiulize kitu, Yakobo aliishi maisha ya kumpendeza Mungu tokea utoto wake lakini Mungu hakufanya Agano naye tokea utoto wake (japo alishamchagua tayari Mwanzo 25:23, Warumi 9:10-13) Mungu alisubiri kwanza Yakobo awe na ufahamu wa kutosha na kufanya maamuzi sahihi kwa kuelewa gharama za kile anachokiamua ndipo aingie naye Agano lake thabiti.

Bwana Yesu aliwaambia wale waliomfuata kuwa mtu anayetaka kuwa mwanafunzi wake basi ajikane mwenyewe na ajitwike msalaba wake ndipo amfuate (Luka 14:25-27) lakini hakuishia hapo kuna maneno aliyasema kwenye mstari unaofuata (kuanzia 28-30) ambapo inafafanua vizuri mada yetu ya leo. Bwana Yesu alisema hivi;


Luka 14:28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

Umeona hapo? Neno la Mungu lipo wazi kuwa kuna gharama lazima uzipige unapotaka kumfuata Kristo, uko tayari kuyaacha yale yanayokupendeza wewe ili uyafanye yanayompendeza Kristo hata kama wewe hayakupendezi? Je! uko tayari kuyaacha yale unayoyapenda (au unaowapenda) wewe na kufanya yale anayoyapenda Yesu hata kama wewe huyapendi (au huwapendi au hupapendi)? Mambo kama vile jinsi ya kuvaa, watu sahihi wa kuambatana nao, kuwa na muda wa kutosha kufanya maombi na kusoma Neno  la Mungu hata kama mwili wako hautaki na mengine mengi, je! uko tayari? (japo hayo hutayaweza kwa nguvu zako Bwana Yesu atakuwa pamoja nawe kukutia nguvu ya kushinda).

Sasa hebu jiulize kama iko hivyo mtoto mdogo anaweza kuzipiga hizo gharama? Mtoto mdogo hawezi kuingia Agano na Mungu hivyo kubatiza mtoto ni tendo lisilo la kimaandiko wala asije mtu akasema kuwa ni ufunuo wa Roho, maana hawezi kukufunulia kitu ambacho ni kinyume na Neno lake.

Ndivyo hivyo hivyo Bwana Yesu anatuambia “Aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Marko 16:16). Sasa mtoto mdogo hajui kitu chochote wala hajaamini chochote hivyo ni ubatizo batili.

Mtu anapaswa ajue kuwa maisha ya dhambi yatamuangamiza maana kuna hatari inayoijia dunia yote nayo ni jehanamu ya moto kwa wote watendao maovu (2 Petro 3:6-7)

Pale mtu anapojua kuwa matendo yake maovu yatamuangamiza kama vile uzinzi, ulevi, wizi, chuki, visasi, ugomvi, uvaaji mbovu, starehe za kiulimwengu na mambo kama hayo anapaswa kuyaacha ila peke yetu hatuwezi kuushinda uovu ndani yetu bila kumkaribisha Bwana Yesu (Yohana 15:5)

Mtu anapotubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha zote na kumgeukia Mungu na kumuamini na kumkiri Bwana Yesu kuwa ndiye Bwana na Mwokozi huyo ndiye amekizi vigezo vya KUBATIZWA tena katika UBATIZO SAHIHI wa kuzamishwa kwenye maji tele na kwa Jina la Yesu Kristo.  

Yote unayoyafanya kwa ajili ya kumtumikia Mungu, kuhudhuria ibada, kufanya maombi au maombezi, kuimba kwaya, kutoa sadaka na mengineyo usiyafanye kwa desturi au tamaduni tu ulizozikuta bali fanya maaumuzi ya kumpa Kristo maisha yako kwa kumaanisha kisha thibitisha kwa kuingia Agano na Mungu kwa ubatizo sahihi. Kumbuka hata Yesu alimpendeza Mungu tokea utotoni lakini alibatizwa akiwa mtu mzima.

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT