Je! Haturuhusiwi kutoza riba kulingana na biblia?

Maswali ya Biblia 2 Comments

SWALI: Biblia inasema tusikopeshe kwa riba, je! Wanaowakopesha watu kwa riba wanafanya dhambi?

JIBU: Bwana ameruhusu kuchukua riba kutoka katika mikopo tuwapayo wenzetu kama moja ya namna ya kujipatia faida, lakini ameweka  mipaka yake. Siyo mipaka ya asilimia za riba za kuwatoza tuwapao mikopo, Hapana, Ila ni mipaka ya kwa nani haturuhusiwi kuchukua riba. Na watu hao ambao haturuhusiwi kuchukua riba toka kwao ni ndugu zetu katika mwili na katika Kristo (kiimani)pia.

Kumbukumbu 23:19 “Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;

20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki”.

Kwa hali ya kawaida ndugu yako mfano Kaka au dada akipitia shida akahitaji msaada wa mkopo kutoka kwako, kibinadamu tunaguswa kuwapa bila masharti, siyo ya riba wala ya muda wa kurudisha, na wakati mwingine tunaweza kuwapa moja kwa moja hata wasirudishe kile walichotukopa.

Au pale inapotokea unafanya biashara mfano ya chakula na nduguyo akapita na njaa, unaweza kumwacha akala pasipo malipo tofauti na wateja wengine.

Sasa hyo tabia ya kutopenda kujinufaisha au kujitajirisha kutoka kwa ndugu zetu  ndiyo mapenzi ya Mungu wetu,

Hali kadhalika katika Ukristo, wote tuliomwamini Yesu Kristo tunafanyika kuwa ndugu..Upendo wa Kristo unatuunganisha pamoja.tunakuwa tunapendana bila masharti..Upendo huo unatufanya kusiwepo hata na hamu ya kutaka faida kutoka kwa ndugu zetu katika Imani kama vile ilivyo katika ndugu zetu wa mwili. Ndio hapo biblia inatuasa kwamba tusitozane riba sisi kwa sisi. Lakini kwa mtu mwingine nje na ndugu zetu wa kimwili na kiimani, tunaweza kuwatoza ili tupate faida katika shughuli tuzifanyazo.

Mahali pengine Bwana alipotilia mkazo katika upendo wa namna  hii ni  katika Mambo ya walawi 25:35-37.

“35 Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.

36 Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe.

37 Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida”.

Vinginevyo tunapofanya kinyume kwa kujinufaisha kutoka kwa ndugu zetu kwa namna zozote kama kujitwalia riba, hatumpendezi Mungu na ule upendo wa Kristo unakua haupo ndani yetu.

Ezekieli 22:12 “Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU.

Ubarikiwe.

2 thoughts on - Je! Haturuhusiwi kutoza riba kulingana na biblia?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *