Je Bwana anaposema, nitaliweka jina langu”alimaanisha nini?

Maswali ya Biblia No Comments

Karibu tujifunze Maneno ya Uzima..

Mahali popote unapoona Mungu anasema ameliweka jina lake anamaanisha sehemu hiyo au kitu hicho ni ” kiteule chake yaani Amekichagua ” Au amekiweka wakfu kwa ajili ya kumwabudu, Kumtangaza, kumfanyia Ibada n.k si vinginevyo!

Ni kitu,mtu au mahali popote ambapo pamewekwa wakfu kwa Mungu au kupakwa mafuta ya Utumishi, basi kitu au Mtu huyo anatakiwa kuchukuliwa kwa umakini sana, kutoghafilishwa, au kutotiwa unajisi maana Mungu kashaweka jina lake Ndani yake na atakayekikosea hicho atapata adhabu kali kutoka kwa MUNGU.

Mfano mzuri ni pale Mungu anapoliweka jina lake Ndani ya malaika wake ili awahudumie Wana Israeli


Kutoka 23:20-21
20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa JINA LANGU LIMO NDANI YAKE.”

Mfano mwingine pia tunaona Mungu analiweka jina lake juu ya Wana wa Israel, Yaani wanawekwa wakfu kwa Mungu kati ya mataifa yote ulimwenguni, Hivyo mtu/taifa lolote lililo wafadhaisha Wana Israel lilishiriki adhabu Kali ya Mungu

Hesabu 6:27
“Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.”

Tangu hapo hata sasa Mungu alimbariki aliyeibariki na kumlaani aliyei laani Israel na itaendelea kuwa hivo.

Pia tunaona Mungu analiweka jina lake katika hekalu alilolijenga mfalme Sulemani pale Yerusalem

2 Wafalme 21:4
” Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.”

Kuna wakati Mungu alighairi ghadhabu yake dhidi ya Wana wa Israel, si kwa sababu walimpendeza sana, La! Ni kwa sababu ameliweka jina lake Ndani yao.
Kwa undani wa Hilo soma Ezekiel 36:21, 20:9-10 na Isaya 48:9-10

Katika Agano jipya Mungu ameliweka jina lake katika vitu vikuu viwili

Kanisa lake : popote palipo na kanisa hai la kristo Hilo ni hekalu la Mungu na jina lake li mahali hapo, pamewekwa wakfu kwa ajili ya ibada, Dua, sala, shukrani n.k
Sasa inapotokea mtu akalinajisi kwa namna yoyote Ile basi yupo kinyume na Mungu, na adhabu ya Mungu itakuwa juu yake.

Ndani ya Waamini/ Waliookoka ; Mtu aliyeokoka anapokea kibali Cha Mungu moja kwa moja ndani yake kupitia yule Roho Mtakatifu anayeachiliwa ndani yake, mtu wa namna hii anakuwa rasmi chombo kiteule cha Mungu, Vivo hivyo yeyote atakaye mfadhaisha basi Hukumu ya Mungu itakuwa juu yake mtu huyo

Na mtu anaokoka kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi kwa ” Jina la Yesu Kristo ” sawa na Matendo 2:38

Anapoyakamilisha hayo Roho mtakatifu humjilia ndani yake na kuanzia hapo Jina hai la Mungu linawekwa ndani yake na anakuwa ” mtiwa mafuta wa Bwana “.

Maran atha…

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *