Je watenda kazi ni wachache?

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo karibu tujifunze maneno ya uzima?.

Umewahi kujiuliza hili jambo na kutafakari, kauli hii aliyoizungumza Bwana Yesu? huenda huwa tunaiosoma tu mara kwa mara pasipo kuitafakari kwa kina…Leo tutakwenda kutazama kwa undani ni kwa namna gani watendakazi ni wachache.

Mathayo 9:36-38”

Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.

[37]Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.[38] Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

Hapo tunaona Bwana Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa “….mavuno ni mengi watendakazi ni wachache”

Lakini je? Watendakazi kweli ni wachache? Hapana watendakazi sio wachache ni wengi sana tu, lakini kwa nini Bwana Yesu aseme hivyo?

“si kwamba watendakazi ni wachache la!, ni wengi ila wenye nguvu na uwezo wa kuifanya kazi ndio wachache” kwasababu kunahitaji nguvu za rohoni nyingi kuifanya kazi ya Bwana na kunahitajika gharama pia..


Kwa kuwa waliotayari kuifanya kazi ya Bwana ni wachache..jiulize kwa nini wengi wanaikimbia? na kwa namna gani?…

Kuifanya kazi ya Mungu kuna gharama lazima kama mwamini uingie na kwa bahati mbaya wengi wanakwepa kuziingia gharama hizi, wengi wanataka kupokea tu taji/heshima pasipo kuingia gharama jambo ambalo haliwezekani…

Mmoja wao ni wewe unaesoma huu ujumbe! Tangu uokoke hujawahi kuwahubiria watu habari njema za ufalme wa Mungu, hujawahi kufanya uinjilisti wa namna yoyote ile kuwavuta watu kwa Kristo. Wewe ni kanisani jumapili kwa jumapili, ukitoka hapo imeisha hakuna kitu kingine unafanya kwa ajili ya Mungu wako,hata huyo jirani yako mlevi,mganga,muislamu,nk hujawahi hata kuwahubiria, na kuwapa hata ushuhuda jinsi Yesu alivyokutendea.


Una simu yako lakini pia ni ngumu kuitumia kufanya uinjilisti hata kwa kupost tu neno la Mungu kwenye status yako huwezi, lakini unaitunia kupost memes(vichekesho ) na umeokoka unasema unampenda Yesu.

Ukitoka kanisani unakwenda kwenye mipira,unakaa na wenye dhambi na wanatukana na wewe uko hapo na hakuna chochote unachofanya badala yake unaungana nao ama unakaa kimya tu na kucheka wala huwaambii na kuwakemea wabadilike wamwamini Yesu.

Ukweli ni kwamba

“kila aliemwamini Yesu Kristo na kuoshwa dhambi zake huyo ni mtenda kazi katika Shamba la Bwana”

lakini je unatenda kazi katika shamba la Bwana ama ni mtumwa mlegevu usiejua wajibu wako?.

Una miaka 2 – 10 kwenye wokovu lakini hujawahi hata kumvuta mtu mmoja kwa Kristo,hata kumhubiri Kristo kwa watu/ familia yako, hujishughulishi na kazi ya Bwana wewe ni kupokea tu lakini huwezi kutoa.

njia moja wapo ya kupokea kitu kipya na kukielewa vyema ni kutoa kile ulichonacho kwa wengine”

huwezi kupokea kitu kipya zaidi na kukielewa kwa kina kama hutaki kutoa ulichonacho kwa wengine.


Gari likiwa limejaa mafuta(full tank) na limepaki tu halina pa kwenda haliwezi kupokea mafuta mengine litabaki na yale yale mafuta tu

maana ni hasara kujaza mafuta full tank na halina pa kwenda.

Watu wengi wameokoka kanisa lina watu 1000 au 300 mpaka 5000 lakini watendakazi ni 20 au 10 au hakuna kabisa.(fikiria watu wote makanisa yote wangekuwa ni watendakazi ni watu wangapi wangeokoka) ulimwengu ungepinduliwa kama kanisa la kwanza.


“mtendakazi sio mchungaji tu,shemasi,mzee wa kanisa,katibu,nabii nk” la bali ni sisi sote tuliomwamini Yesu na wewe ukiwemo ,kuwashudia wengine sio karama sote tumepewa huduma ya upatanisho ndani yetu.


2 Wakorintho 5:18 ” Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo,NAYE ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;”
Usilisahau hili hata kidogo.

GHARAMA ZISIZOEPUKIKA KWA MTENDAKAZI YOYOTE.


Tutatazama gharama ambazo mtu aliemwamini Yesu Kristo na kuwa mtendakazi katika shamba la Bwana.


I. MAOMBI


Hii ni gharama inayokwepwa na wakristo wengi sana katika nyakati hizi za mwisho. Uvivu wa kuomba umewavaa watu wengi, mkristo yuko radhi kuangalia mpira movie masa2 lakini hawezi kuomba hata dk30. Maombi ndio sehemu maalumu, na ndio Mungu alioichagua ya sisi kuzungumza nae lakini cha ajabu tunamkimbia Mungu kuzungumza nae..

Na ndio sehemu tunapopata faraja,tumaini na nguvu za kumuangusha Yule mwovu ibilisi, wakati mwingine unaona mambo ni magumu hayawezekani kumbe yanawezekana na yote kwa sababu huombi, katika maombi unapata ujasiri na tumaini na kongezeka imani na kusimama imara katika roho na kuijenga nafsi yako.

II. NENO


Hii ni gharama nyingine ambayo watu hawataki kuibeba, kusoma Neno neno ni chakula cha roho zetu Mkristo anapokosa neno ndani yake hawezi kusimama imara na kuziepuka hila za Yule ibilisi….


Ni sawa na mtu asiejua kusoma ukimpelekea karatasi asaini ambalo linamtaka ahame mahali alipo bila malipo ila mtu anakuja anamwambia saini hapa ukisaini utapata milioni 500” atasaini maana hajui kusoma…Vivyo hivyo usipojua neno shetani atakuletea hadi vifungu vya “jisaidie na Mungu atakusaidia” wakati hakuna sehemu yoyote kwenye biblia imesema hivyo.

III. UOGA.
Kuogopa watu watakuonaje, kutukanwa, kutengwa, kufukuzwa, kudharauliwa,nk, hii yote inawapata wakristo wengi kwa sababu hawana maombi ndani yao wala Neno, wanazificha talanta zao wanaogopa maisha ya kuchekwa na kuonekana wamerukwa na akili…

Lakini wangelikuwa ni waombaji na wasomaji wa neno wangelifahamu hata mitume na Bwana Wetu Yesu mwenyewe alifanyiwa hivyo hivyo.

Yapo mengi sana lakini kwa leo nilitamani tuyafahamu haya, Usijidharau wala usifikiri watenda kazi ni wachache ni wengi lakini wengi hawana nguvu kwa sababu ni wavivu wa kuomba, kusoma neno,na ni waoga, maana yake ni wadhaifu…

Wewe hapo ni mtenda kazi jiulize hadi leo umeitenda kazi ya Bwana? Na je ni mtendakazi unayestahili ujira wako pale Bwana atakaporudi?.

Jiulize je tutakaposimama wote mbele zake Mungu mwenyezi muumba wa mbingu na nchi, ili kazi zetu zipimwe je! Utakuwa na kazi ipi ulioifanya ikapimwa ukiachana na matunda ya haki… Je utakuwa na matunda ya kazi?.


1 Wakorintho 3:13” Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.”

Unaona hapo anasema “….kila mtu…..”vile vile unaifanya kazi ya Mungu, je unawajenga watu katika msingi gani? Ni wa Kristo ili wakue kiriho au wa mafanikio na kukomboa ardhi nk… Jibu unalo

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

MARANATHA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *