Shalom ndugu yangu katika Bwana, karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Bwana aliwahi kufundisha mfano mmoja ambao unafahamika sana na wakristo wengi, lakini leo nataka tuutazame tena na kisha tutapata kitu kingine ambacho kitaweza kutufanya tuwe macho katika maisha yetu ya wokovu wakati tunapo mngojea Bwana kuja kutuchukua na kutupeleka katika makao aliyo tuandalia kama alivyosema katika
Yohana 14:2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.
Bwana alipojiwa na mkutano mkubwa, aliwatolea mfano ambao tunausoma katika
Luka 8:5 Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila.
6 Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba.
7 Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga.
8 Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie.
Na mfano huu Bwana akaja kuuelezea nini maana yake kama tunavyosoma katika
Luka 8:11 Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.
12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.
13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga.
14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.
15 Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.
Sasa ukisoma maandiko hapo utagundua kuwa kuna watu wengi sana ambao leo hii ni wafuasi wa Bwana Yesu, lakini watu hawa wamegawanyika katika makundi manne kulingana na jinsi wanavyosikia neno la Mungu kama ufafanuzi wa Bwana unavyojieleza, na hii ni hatari sana katika maisha yetu ya wokovu kwasababu mwisho wa siku Bwana hatoweza kuchukuliana na makundi yote manne isipokuwa hilo kundi la mwisho tu kwasababu alisema tuangalie jinsi tusikiavyo akimaanisha kuwa, tuwe katika kundi hilo la nne na faida ya kuwa katika kundi hilo ni kwamba, tunakuwa ndugu zake kama yeye mwenyewe alivyosema katika.
Luka 8:21 Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Umeona hapo faida ya kuwa katika kundi la nne la watu wanao sikia neno la Mungu na kulifanya?
Kumbe sio wote walio wafuasi wa Bwana Yesu bali ni wale watakao sikia neno la Mungu na kulifanya na hivyo tutaitwa ndugu zake kama biblia inavyosema katika
Warumi 8:29 Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa NDUGU WENGI.
Lakini Bwana alisema kuwa sio kitu rahisi kuwa miongoni mwa ndugu zake kwasababu ni lazima tusikie nano la Mungu na kulifanya kwani kuna vitu vingi sana ambavyo vinatufanya wengi tushindwe kusikia neno la Mungu na kulifanya na ndio maana Bwana alitoa Onyo na kusema JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO”
Luka 8:18 Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
Akimaanisha kuwa tuwe wasikiaji kama lile kundi la nne na tusiwe waskiaji kama hayo makundi mengine, yaani tuwe makini sana katika kusikia na kuyafanya maneno ya Mungu.
Je! Wewe unayejiita mchungaji unasikia na kufanya neno la Mungu linalokwambia kuwa uache uo uzinzi unaoufanya na wauumini wako hapo kanisani? Wewe kijana uliyeokoka unasikia na kufanya neno la Mungu linalokwambia kuwa uache hizo picha za ngono na pornography unazozitazama huko mtandaoni? Wewe dada uliyeokoka unasikia na kufanya neno la Mungu linalosema kuwa uvae mavazi ya kujisitiri na uache hivyo vimini vyako na tight ambazo zinawakosesha ndugu wenzako hapo kanisani wanapokutazama? Wewe mwalimu unasikia na kufanya neno la Mungu linalosema uwalishe kondoo zake kwa mafunzo ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo? Je unafundisha utakatifu katika kanisa? Unasikia na kulishika neno la Mungu linalosema wanawake wafunike vichwa vyao wakati wa ibada? Maana imeandikwa pia sehemu nyingine kuwa tusiwe wasikiaji tu bali watendaji wa neno la Mumgu
Yakobo 1:22 Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
Je! Unayatenda hayo? Kama husikii na kuyafanya hayo maneno ya Mungu jua wewe unajidanganya nasfi yako tu, kama huyafanyi maagizo ya Bwana jua unajidanganya nafsi yako tu na hautokua miongoni mwa ndugu wengi siku ile, hivyo tubu leo na ukawe msikiaji na mtendaji wa neno la Mungu kwa uvumilivu wote.
Shalom, Bwana akufanye uwe msikiaji na mtendaji wa neno lake.