Shalom Wapendwa. Karibu Tujifunze Maandiko matakatifu
Kumekuwa na maswali mengi sana miongoni mwa wakristo {Mkristro ni mtu aliyegeuka na kudhamiria kwa gharama zozote kujitwika msalaba wake na kumfuata kristo Yesu}. Wanajikuta wana maswali mengi sana yakosayo majibu.
Akisema nimempa Yesu maisha yangu na hakika nimepata furaha kubwa ya kiMungu ndani yangu, lakini vipi kuhusu nje!
Najaribu kuishi maisha matakatifu lakini wapi, bado kuna mengi hayaendi sawa, nilitengwa na rafiki zangu baada ya kuacha dhambi, nikachukiwa na ndugu, nilipoacha masengenyo ndipo ikawa Mwanzo wa kuonekana mwenye kujidai sana
Nilipoacha Rushwa kazini vikainuka vikwazo na kuchukiwa na wengi zaidi, Niliposaidia watu niliambulia Lawama maradufu, nilipoanza kufunga na kuomba badala ya shida kupunguza lakini ulikuwa ndio Mwanzo wa utungu, Nilipomtumikia Mungu kwa kwa uaminifu matatizo ya kiuchumi yaliibuka zaidi
Unafikia hatua mpaka ya kusema hakuna faida katika kujitenga na maisha ya kidunia na kujinyima, zaidi zaidi kubakia yule yule siku zote! Mbona ni tofauti kwa wasiomcha Mungu! Ni matajiri na wenye familia zenye Raha Kila siku pamoja na kumkana kwao Mungu, hata wazinzi hunawiri kwa Afya njema..
Pamoja na utakatifu wangu wote, Mbona Mungu hanipi furaha kama wao, hanipi zile ahadi alizowaaidia wamfuatao?! Ni laana Gani juu yangu kuyapitia haya yote? Au wao hupata Raha hizo kwa kipi Cha ziada juu yangu?
Mpendwa wewe sio wa kwanza kujiuliza hayo ni watakatifu wengi ulimwenguni hujiuliza hivyo. Hata mtumishi mwaminifu kwa Mungu Daudi aliwaza kama wewe katika…..
Zaburi 69:7-12
7″ Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
9 Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
10 Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11 Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.
12 Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.”
Zaburi 73:1-12
1 “Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao.2 Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza.
3 Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.
4 Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu.
5 Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu.
6 Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo.
7 Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.
8 Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.
9 Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani.
10 Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao.
11 Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
12 Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.”
Zaburi 42:3
“Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako.”
Angalia, pamoja na Wema wote wa Daudi, kuwaombea wengine fadhili za Mungu kwa kufunga na hata kwa machozi, lakini bado alikuwa mgeni na kituko mbele za nduguye. Hata kufikia kuwaonea wivu walio waovu
Mambo hayahaya yapo katika fikra za watakatifu wengi Leo, Wakisema mioyoni na hata kwa vinywa vyao Mungu wetu uko wapi? Ikwapi faida katika kukutumikia? Ikwapi faida kuacha kuendana na fashion, kupaka lipstick, wigi? Mbona wayafanyayo hayo wanapata waume wazuri ndoa nzuri lakini Mimi ni yule yule tu.
Mpendwa utasema kuna faida Gani katika kuacha pombe, sigara,Wanawake na Anasa? Kuna faida Gani kuacha uhuni, kamali, kubet? Angali wenzangu wanafanikiwa haraka sana katika hayo. Wenzangu wanaopokea Rushwa wanajenga, wakisomesha na kulisha familia zao kifahari, si zaidi Mimi?
Ndugu hayo yamekuwa maswali ya WATAKATIFU wengi tangu Zamani, lakini Bwana aliyasikia na kutoa majibu katika kitabu Cha Malaki 3 akisema..
Malaki 3:13-17
13″ Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?14 MMESEMA, KUMTUMIKIA MUNGU HAKUNA FAIDA; NA, TUMEPATA FAIDA GANI KWA KUYASHIKA MAAGIZO YAKE, na KWA KWENDA KWA HUZUNI MBELE ZA BWANA WA MAJESHI?
15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. NAYE BWANA AKASIKILIZA, AKASIKIA; na KITABU CHA UKUMBUSHO KIKAANDIKWA MBELE ZAKE, KWA AJILI YA HAO WALIOMCHA BWANA, NA KULITAFAKARI JINA LAKE.
17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.
18 Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.”
Kama tunavyoona, hakuna Wema wowote wa Mtakatifu upitao Bure tu! Bali Mbinguni kuna KITABU CHA KUMBUKUMBU kwa ajili ya watu maalum, kikirekodi mambo mema wafanyayo watakatifu duniani.
Kama ilivyo kwa vitabu vingine lazima kiwe chenye kurasa nyingi, Na matendo mema tu ya watakatifu ndiyo yakijazacho kitabu hicho, si vinginevyo.
Mpendwa kwa kadri yako kumcha Mungu kwa kuyafanya yaliyo mema mbele zake hakika yanarekodiwa Kila siku, ndio yaliyobeba Wingi wa thawabu utakazopewa Mbinguni siku Ile ya Mwanakondoo.
Hivyo ndugu mpendwa huu si wakati wa kusema hakuna faida yoyote katika kumcha Bwana, faida ni nyingi sana ambazo nyingi utazijua kwa undani katika urithi wako wa uzima wa milele.
Mambo ya Dunia hii si urithi wetu, hivyo yote ni mema kukosa au kupata, umaskini ama ukwasi, Afya au magonjwa! Cha kufanya ni kupiga mbio zaidi katika kumcha Bwana, Maana Mungu wako aonaye taabu yako atakulipa, Maadamu wayatenda yaliyo mapenzi yake kipi kikukwamishe? Weka kumbukumbu lako Mbinguni, achana na mafundisho ya watumishi bandia kwamba mafanikio ya kifedha ndio uthibitisho wa Mungu kuwa pamoja nawe au Amekuacha, La! Kumbukumbu sahihi lipo Mbinguni.
Ongeza bidii kama ni kuacha pombe, uasherati, vimini, suruali, kataa Rushwa na hakika mema yako hayatokwenda Bure Bure!
Usiwaze kwamba utafanya hayo ukiwa umri Fulani, hakuna ajuaye sekunde mbele yake, huenda ukawa umechelewa tayari.
Usipange kuukosa urithi na faraja isiyoelezeka ya milele na milele, Usifuate mienendo ya Dunia hii.
JE? Ni kwanini Mungu anaruhusu Waovu Wafanikiwe ?
Ni kwasababu hawana sehemu ya urithi katika Ulimwengu unaokuja,Bali urithi wao upo katika Dunia ya sasa.
Ndio Maana Bwana huruhusu wapate faraja yao hapa
Bwana asema na Daudi….
Zaburi 92:7
” WASIO HAKI WAKICHIPUKA KAMA MAJANI NA WOTE WATENDAO MAOVU WAKISTAWI. NI KWA KUSUDI WAANGAMIZWE MILELE;”
JE mpendwa u tayari kuwa miongoni mwao? Kwanini ujinufaishe kwa Rushwa, Ulevi, Utapeli, kamari, Ukahaba, biashara haramu ili Uangamizwe hata milele?
ITAKUFAIDIA NINI KUPATA ULIMWENGU MZIMA NA KUPATA HASARA YA NAFSI YAKO? kuonekana wa kisasa Leo kwenda na fashion itakufaidia Nini mpendwa?
Kumbuka KUMBUKUMBU LA WENYE HAKI LINAANDIKWA MBINGUNI!
Usitamani njia zao Wala mafanikio yao, Mpe Kristo maisha yako Sasa ingali upo hai kabla haujachelewa maana hakuna aijuae kesho, fanya kabla mlango wa neema haujafungwa.
Na ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.