Hili ni Neno linalomaanisha mashitaka, au malalamiko, ambayo lengo lake ni kufikishwa mbele ya mahakama ili kutolewa hukumu.
Kwamfano, pale mfanyakazi wako, amekuibia, au amekutukana, au amekuharibia mali zako na wewe unataka kumpeleka mahakamani kwa tendo hilo, ili awajibishwe. Sasa hilo shitaka ambalo unampelekea mahakamani kwa jina lingine ndio linaloitwa Daawa.
Neno hili katika agano jipya tunalisoma katika vifungu hivi;
1Wakorintho 6:1 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu?
2 Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?
3 Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya?
4 Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa?
5 Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake?
6 Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini”.
Katika Habari hii ni, Mtume Paulo, alikuwa analirekebisha kanisa kwa tabia za watakatifu kushindwa kutatua mashitaka yao(Daawa) wao kwa wao mpaka inafikia hatua ya kuyapeleka kwa waamuzi wa kidunia kuwaamua. Jambo ambalo ni la aibu ni kuonyesha udhaifu wa maamuzi.
Kwamfano, labda mtakatifu mmoja katika kanisa, kazidisha mpaka wa kiwanja chake, hadi kuingia kwa mtakatifu mwingine, na wao kwa wao wakashindwa kuelewana, hivyo ni sharti kanisa liwasaidie kutatua mashitaka hayo kwa hekima ya ki-Mungu, si lazima mpaka watu wa ulimwengu wawasaidie kutatua au wajue ni nini kinaendelea katikati ya wapendwa. Ni aibu.
Ndicho ambacho mtume Paulo alichokuwa anajaribu kuwaeleza watakatifu wa kanisa lililokuwa Korintho, kwamba ndugu akiwa na Daawa kwa ndugu mwenzake, basi kanisa limalize migogoro yao.
Hata sasa, tunapaswa tutumie hekima hii, leo hii utakuta mafaili ya watakatifu wengi mahakamani, kuliko kanisani, migogoro utaisikia mpaka kwenye magazeti, mchungaji Fulani, azozana na mke wake, wagombania mali.. Haipendezi kwa watakatifu.
Neno hili pia utalisoma pia katika vifungu hivi,
Kumbukumbu 16:19 “Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki”.
Soma Ayubu 5:8, 35:14, 31:13, Kumbukumbu 16:19
Bwana akubariki.