Siku sahihi ya kuabudu ni ipi, siku ya sabato ni lini?

  Kanisa, Uncategorized

Sabato maana yake ni PUMZIKO. Na pumziko la Mungu lilikuja katika siku ya saba, baada ya kumaliza uumbaji wake kwa siku sita. Hivyo akaibariki, akasema siku hiyo ni Sabato yangu.

Lakini miaka mingi mbeleni, alipokuja kulichagua taifa moja teule, akawaagiza kuwa siku hiyo ya saba itakuwa ni siku ya kupumzika kwao, Na taifa lenyewe ndio taifa la Israeli. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, bali utamtafakari Mungu wako na kumfanyia Ibada. Ambayo kwa sasa ndio siku ya jumamosi.(Kutoka 20:8-11)

Hivyo jambo hilo lilikuwa ni agizo la Mungu kwao kwa kipindi chote.

Lakini tunapokuja katika agano jipya lililoletwa na Yesu Kristo mwokozi wetu, linageuka na kuwa si la mwilini tena bali la rohoni, agizo la kuifanya siku Fulani takatifu kuliko nyingine linageuka na kuwa la kumwabudu Mungu katika Roho na kweli.

Yohana 4:23 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”.

Hii ikiwa na maana, haijalishi ni siku gani mtu atamwabudu Mungu, kinachojalisha ni ibada inayotoka moyoni iliyojaa matunda ya kweli ya Roho. Hicho ndicho Mungu anakitazama, iwe ni jumamosi, au jumapili, au jumatano, haijalishi maadamu ni katika Roho na kweli, basi ibada hiyo Mungu anaikubali.

Vilevile kinyume chake ni kweli, ikiwa ibada hiyo haipo katika Roho na kweli, ni ibada ya juu juu tu, haina misingi ya Neno la Mungu, haina upendo, haina utakatifu, haina kumaanisha kwa Mungu, basi hata kama ni Siku ya jumamosi, bado si kitu mbele za Mungu.

Na ndio mtume Paulo kwa kufunuliwa na Roho aliandika hivi;

Wakolosai 2:16 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.

Akasema tena katika Wagalatia maneno haya;

Wagalatia 4:9 “Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?

10 Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka”.

Unaona? Hatupo katika zama za kushika, siku, miezi na miaka mitakatifu, Mungu hazitazami hizo tena. Hivyo kama umekombolewa na Kristo, basi fahamu kuwa Kristo ndio sabato yako. Kama alivyosema katika Mathayo 12:8.

Kwahiyo kama utaratibu kwa kanisa lenu ni kukutanika Jumamosi kwa wiki, ni sawa, ikiwa ni jumapili pia ni sawa, ikiwa ni jumatano pia ni sawa.

Lakini utauliza wanaokutanika jumapili walitolea wapi utaratibu huo?

Jibu ni kuwa watakatifu wa kanisa la kwanza walikuwa wanakutanika siku ya kwanza ya juma, ambayo ndio Jumapili kwa ajili ya mambo ya kiibada, Soma(1Wakorintho 16:1-2, Matendo 20:7). Na pia ndio siku ambayo mwokozi wetu alifufuka. Hivyo ni siku ya ushindi kwa ulimwengu.Kwa hiyo ni pendwa pia.

Lakini tukumbuke kuwa hakuna siku takatifu Zaidi ya nyingine, kwasababu Mungu ni Roho, nasi tunamwabudu katika roho na kweli. Wa jumamosi asimuhukumu wa jumapili, halidhalika wa jumapili asimuhukumu wa jumamosi.. Sikuzote ni za Bwana.

Ubarikiwe.

3 thoughts on - Siku sahihi ya kuabudu ni ipi, siku ya sabato ni lini?

LEAVE A COMMENT