Je! Umeiamini Injili Ipi?

  Biblia kwa kina, Uncategorized

BWANA YESU asifiwe, Neno la Mungu linasema katika

Marko 1:15 akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

Sasa hapo BWANA anatoa taarifa na pia maelekezo ya nini cha kufanya. Taarifa anayotoa hapo ni kuwa ufalme wa Mungu umekaribia na maelekezo ya kufanya ni tutubu na kuiamini injili, sasa hadi hapo utakua umeona kuwa ufalme wa Mungu utakapo kuja ( maana upo karibu ) hautakua kwaajili ya watu wote bali ni kwa wale tu ambao watakao tubu dhambi zao na kuiamini injili. Lakini sasa kutubu tu peke yake haitoshi pasipo kuiamini injili, sasa swali ni je! Umeiamini injili ipi wewe kama mtu uliyetubu? Kwamaana biblia inathibitisha kuwa hakuna injili moja (soma 2 wakorintho 11:4)
Hivyo basi, Kama umetubu na bado hujaamini injili sahihi ya BWANA basi jua ufalme huu utakapokuja hautokuhusu wewe, kama umetubu na hutaki kuamini injili ya BWANA YESU basi jua kuwa ufalme huu utakapokuja hautokuhusu wewe bali wale walio tubu na kuiamini injili ya Bwana.

Sasa utajiuliza injili ya Bwana ni ipi? Au ni injili ya namna gani? Injili ya Bwana ni kumwamini yeye na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu ( matendo 8:16 matendo 10:48) maana alisema atakaye amini na kubatizwa ataokoka, manake kama umebatizwa vinginevyo hiyo siyo injili ya Bwana na ufalme wa Mungu utakapokuja hautokuhusu kwasababu ulishindwa kuiamini injili ya Bwana

Injili ya Bwana inasema tushiriki meza ya Bwana kwa ukumbusho wake hadi atakapokuja, usiku ule Bwana aliutoa mkate na kuwapa wanafunzi wale, sasa wakati anafanya hicho kitu mtume paulo hakuwepo lakini utaona baadae baada ya Bwana kupaa paulo anafunuliwa kitu hicho hicho tena

1 Wakorinto 11:23 Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,
24 naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

Unaona hapo? Ni kitu kile kile Bwana anakifunua tena kwa mtume Paulo, Sasa hii ni kuonesha kuwa maagizo yake ni yale yale. Sasa ikiwa umeamini injili nyingine tofauti na hii basi ufalme wa Mungu hautokuhusu.

Injili ya Bwana inatuagiza kutawadhana miguu ( yohana 13:3-17 ) sasa wakati Bwana anatoa haya maagizo paulo hakuwepo lakini kitu hicho hicho utakikuta tena kwa paulo miaka mingi baada ya Bwana kupaa

1 Timotheo 5:10 naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema.

sasa hii ni kuonesha kuwa maagizo yake ni thabiti sasa kama wewe bado hujaamini hili jua basi ufalme wa Mungu utakapokuja hautokuhusu wewe

Injili ya Bwana inasisitiza upendo kati yetu na kuwapenda adui zetu

Luka 6:27 Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi


Lakini wewe kutwa kumsengenya jirani yako na kuwachukia adui zako. Kama bado upo hivyo jua kua bado hujaiamini injili ya BWANA na ufalme utakapokuj hautokuhusu

Injili ya Bwana inatukataza kuacha wake zetu na waume zetu kwa sababu zetu binafsi

Marko 10:11 Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;

12 na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

Na wazinzi wote hawana urithi katika ufalme wa Mungu ( 1 wakorintho 6:9-10 ) sasa kama wewe umemwacha mke wako au mume wako kwasababu isiyo ya uasherati ni heri upatane naye manake ufalme wa Mungu utakapokuja hautokuhusu, kwani utakua bado haujaiamini injili ya Bwana

Injili ya Bwma inaagiza wanawake wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri

1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

Lakini wewe dada unayesema umemwamini Bwana unavaa vimini na suruali ambazo hazilusitiri mwili wako, ukijiona unafanya hayo jua kuwa bado hujaiamini injili na ufalme wa Mungu utakapo kuja hautokuhusu.

Sasa wewe unayesema kuwa umemwamini Bwana jiulize kama kweli unayafanya hayo na kama sivyo basi jirekebishe ili usiwe mmoja wapo wa wale wasioamini injili na kuukosa ufalme wa Mungu.

Bwana akubariki 🙏