Shalom mwana wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu…
Biblia inatuambia roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamjia Sauli, bila shaka unajiulza ni roho ya namna gani? Sote tunajua Mungu wetu hutupa roho nzuri na ya amani, sasa inakuwaje aachilie roho mbaya kwa mtu tena ambaye ameshamtia mafuta na roho hiyo inafanya uharibifu kwa watu wasio na hatia
1 Samweli 16:14-23
[14]Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua.
[15]Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
[16]Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.
[17]Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.
[18]Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye.
[19]Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.
[20]Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe.
[21]Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake.
[22]Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu.
[23]Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.
Ili tujue kwa nini hayo yalimpata Sauli tuangalie historia yake. Maandiko yanasema Sauli alikuwa kijana, mzuri na mrefu mwenye uso wenye haya, mlaini. Sauli hakutokea familia ya kikuhani au ya waamuzi walioamua Israel kwa wakati ule, hakuwahi kwenda vitani wala hakuonyesha dalili yoyote kama ni mtu wa vita. Wakati nabii Samweli anampaka mafuta kumtangaza kuwa mfalme wa Israel watu wengine walimdharau maana walipomtazama mwonekano wake, alionekana kama mtoto, hana udhoefu na uongozi wakaona hawezi kuliongoza taifa kubwa kama Israeli jambo ambalo ni kweli hakuwa na uwezo wowote wa kuwaongoza Israel…
Lakini Sauli aligeuzwa na kuwa mtu tofauti kabisa siku ile aliyotiwa mafuta na nabii Samweli maana Roho ya Mungu ilimjilia juu yake (1SAMWELI 10:6)
Taifa la Israel lilikuwa taifa kubwa na hodari hivyo roho ambayo ilitakiwa kuachiliwa kwa Sauli ilitakiwa iwe roho ya uongozi, ujasiri, ushujaa na roho ya maamuzi magumu. Mambo ambayo yangetokea kwa Sauli yangekuwa katika mfumo huo lakini Sauli hakulijua hilo hadi ilipofika siku maadui wa ndugu zao walipotokea na kutaka kuwatawala, wakawaambia kila myahudi ang’olewe jicho lake la kuume la sivyo wote wauwawe. Taarifa hizo zikaenea kila sehemu watu waliposikia wakalia sana maana adui wa ndugu zao alikuwa mkuu sana hakukuwa na mtu wa kuwasaidia kumshinda ili wawaokoe ndugu zao. ..
Habari hizi Sauli alizisikia baada ya mwezi mmoja tangu atiwe mafuta kuwa mfalme, pamoja na kuwa hakuwa na udhoefu wowote wa kupigana vita alisimama kwa ujasiri na hasira na kutamka maneno haya…
1 Samweli 11:4-13
[4]Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.
[5]Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
[6]Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana.
[7]Naye akatwaa jozi ya ng’ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng’ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa BWANA ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
[8]Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
[9]Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
[10]Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.
[11]Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
[12]Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue.
[13]Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israeli.
Maandiko yanatuambia Roho wa Bwana alipomjilia Sauli, alipata hasira kali, Na tukumbuke kuwa hasira inapompata mtu hufanya jambo lolote bila kujali chochote mradi tu afanikishe jambo alilokusudia,
Sauli alipata hasira ambayo hakuweza kujizuia yeye mwenyewe, hasira ya namna hii haikumjia kila wakati isipokuwa wakati ambao lilikuwepo kusudi la Mungu ambalo alipaswa alitimize na Mungu ndiye aliyeiachilia ili kuwaokoa Israel dhidi ya adui zao wakati wa vita vikali. Mungu alikuwa anaituma roho ya hasira kwa Sauli ndipo Sauli alipoenda vitani anakuwa kama simba na kuangamiza maadui wote, hata wale mashujaa hodari wa vita walimwogopa kutokana na hiyo roho.
Roho hiyo tunaiona hata kwa Samsoni, aliposhukiwa na roho ya Mungu kwa nguvu hasira yake iliwaka akafanya mambo bila kujali matokeo yake yatakuwa mazuri au mabaya. Hata alipopigana na wafilisti roho ya Bwana ilimshukia hasira ikawaka ndani yake…
Waamuzi 14:19[19]Roho ya BWANA ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.
Ndivyo tunaona kwa mfalme Sauli, Mungu alimtia mafuta na aliruhusu hasira zile ili kuwaokoa dhidi ya adui zao, lakini tunaona ilipotokea mfalme Sauli akayaacha maagizo ya Mungu basi Bwana aliacha kumtumia, na kumchagua Daudi badala yake. Sauli aliondolewa roho ya uongozi lakini Roho wa Bwana alibaki ndani yake.
Kitu tunachojifunza hapo ni kwamba, Mungu anapomtia mtu mafuta kwa kazi yake huwa hayaondoi, atayaacha yaongozwe na hisia pamoja na akili za mtu huyo wala si kwa mwongozo wa Roho wa Bwana. Inapofikia hatua hii hali huwa mbaya maana mtu huyo atatumia kipawa alichopewa na Mungu kwa manufaa yake binafsi. Tunaona baada ya Mungu kumtoa Sauli katika ufalme na kumpa Daudi, mfalme Sauli hakupenda ndipo kwa hasira akaanza kutumia nguvu nyingi kumuwinda Daudi ili amuangamize. Kwa mamlaka na nguvu alizokuwa nazo alitakiwa kuvitumia kulilinda taifa la Israel dhidi ya adui zao lakini badala yake alielekeza nguvu hizo kwa kumuwinda Daudi kila siku.
Jambo hili tunaliona kwa shetani, alipokuwa mbinguni alikuwa kerubi aliyetiwa mafuta kuliko makerubi wote lakini alishindwa kukaa katika nafasi yake hakutaka kufuata maagizo ya Mungu ndipo Mungu akamvua mamlaka aliyompa na kuwapa wengine. Mungu hakumuondolea yale mafuta aliyomtia ndio maana tunaona hadi leo hii shetani anatumia kuunda falme zake za giza ili atimize anayoyahitaji, hiyo sasa ndio roho mbaya kutoka kwa Mungu..
Haya pia yapo kwa watumishi wengi wa uongo,walimu wa uongo, manabii wa uongo,waimbaji na wachungaji wa uongo, kipindi cha mwanzoni walitiwa mafuta wawalishe na kuliangalia kundi la Mungu Katika njia nzuri, lakini kidogo kidogo wakaanza kukengeuka kwa kuziacha zile njia za Mungu kama alivyofanya sauli, na mwisho wa siku Mungu anawaacha kuwatumia kama watumishi wake na Mungu anaiondoa ile roho ya kuongoza juu yao wanabaki na yale mafuta tu ndani yao ili waende kwa tamaa zao na sio kuongozwa tena na Roho wa Mungu…
Ndo hapo usishangae kuona ni Nabii anatabiria watu na kuona maono hata ya mambo yajayo lakini amejaa Uasherati,atofautiani na mtu wa kidunia hana kielelezo cha kuwafanya watu waende Mbinguni,mwisho anaanza kuwaelekeza watu waje kwake na sio kwa Mungu tena, muda mwingi ni kujisifia yeye na kuuchukua utukufu wa Mungu bila kukumbuka kuwa si kwa juhudi zake akawa hivyo bali ni kipawa cha Mungu kinachomfanya atimize kusudi la Bwana, hatalijali hilo kwa kuwa ile Roho ya Mungu ilishamwacha ikabaki ile roho mbaya kwa Bwana na kufanya kazi juu yake, mwisho wake ni kuleta madhara makubwa kwa kuwapeleka watu wengi kuzimu, na kuwapoteza hata wale waliosimama, na kupelekea kuwa adui wa watumishi wa Mungu wa kweli kama tulivyoona kwa Sauli na Daudi…
Fahamu kabisa, Karama za Mungu hazina majuto, si vya kuvichezea kabisa, kunena kwa lugha unakoringia usifikiri ndo ishara ya kuwa una Roho Mtakatifu, au kuona kwako maono kwamba ndio Mungu anapendezwa na wewe, kujionyesha na kuzitoa Nabii nyingi kana kwamba ukajiona upo kwenye njia sahihi..hayo hayatakuwa kwako chochote kama utakuwa mbali na Neno la Mungu…
Maandiko yanasema..
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO
Ikiwa utakatifu hautakuwa ndani yako zaidi ya mambo machafu, uzinzi, uongo, Uasherati,uchawi,ibada za masanamu, unatukana na mengine mengi,haijalishi utakuwa na ukaribu na malaika na kuzungumza nao kila wakati,fahamu mapema mbingu utaikosa tu..
Usiwe Mtumishi uliyeanza vizuri na Bwana na kumaliza vibaya ,kubali uongozi wa Roho wa Mungu utawale juu yako na sio fikra zako wala akili yako,hata mwisho wetu utakuwa mzuri na wenye kumpendeza Mungu katika safari yetu, hitimisho ni kuwa Mungu hatoi roho mbaya bali sisi ndio tunaitumia vibaya Roho mwema wa Mungu katika kufanya ubaya…
Bwana Yesu atusaidie sana..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.