Tusome;
Yohana 19:32 “Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.
33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;
34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.
35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.
36 Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa”.
Kila tukio, lililokuwa linaendelea pale msalabani lilikuwa na maana yake kubwa rohoni, kwamfano kitendo cha Bwana Yesu kuchomwa mkuki ubavuni, kisha kutoka maji na damu, ni ishara kubwa sana kwetu, katika ukombozi, kwamba ili tukamilishwe na Kristo, hatuna budi, kusafishwa kwa damu na maji.
Damu ni pale tunapotubu, na kuondolewa dhambi zetu kwa damu yake Yesu Kristo. Na maji ni pale tunapobatizwa.(1Yohana 5:5-9)
Vivyo hivyo na katika tukio kama hili, utaona wale wezi wote walivunjwa mifupa yao, lakini walipofika kwa Bwana Yesu hawakumvunja mfupa wake wowote, na mwandishi anaendelea kusisitiza kwamba hiyo haikuwa kwa bahati mbaya, bali ilitokea hivyo ili andiko litimie linalosema “Hapana mfupa wake utakaovunjwa”
Hii ikiwa na maana kwamba mfupa wowote wa Kristo hauwezi kuvunjwa. Huwezi kuutenganisha mguu kutoka katika mwili wake.
Tafsiri yake rohoni ni kuwa sisi kama KANISA lake, ni mwili wake. Biblia inasema hivyo katika,
Warumi 12:4 “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;
5 Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake”.
Hivyo kama ni mwili wake, basi tufahamu kuwa mwili wa Kristo huwa hauvunjwi. Kanisa la Kristo huwa halitenganishwi kwa namna yoyote. Tukishaona mahali tulipo kama ndugu, halafu, kila mmoja anamtumikia Mungu ajuavyo yeye, au hana ushirikiano na mwenzake, tujue kuwa hapo Kristo hayupo. Kwasababu mifupa yake haivunjwi.
Kinyume chake, tukiwa tunashikamana, kama viungo basi Kristo yupo. Hili ni jukumu la kila mmoja anayejiona ni mtakatifu kuhakikisha hana faraka na kiungo kingine katika imani.
Bwana atusaidie, kulitimiliza hili.