“Mke wa ujana wako” anayezungumziwa katika biblia ni yupi?

Ndoa na Mahusiano No Comments

Neno hilo utalipata katika vifungu hivi;

Mithali  5:18 “Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako”.

Malaki 2:14 “Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako”.

Watu wengi wanadhani hili neno “Mke wa ujana wako”. Linamaanisha  Yule rafiki wa kike(Girlfriend) uliyekuwa naye mwanzo, ndio unayepaswa kuishi naye, Yaani kama ulikuwa nao 10, basi hupaswi kumuoa Yule wa 9 au wa 10, bali unapaswa umuoe Yule wa kwanza kabisa kwasababu yeye ndiye mke wa ujana wako.

Mtazamo ambao sio sahihi, na usio wa kimaandiko.

Mke wa ujana anayezungumziwa, ambaye mtu hapaswi kumuacha, ni mwanamke Yule ambaye ulimuoa ulipokuwa kijana ukaishi naye mpaka mmekuwa wazee, huyo ndiye mke wa Ujana wako, kwasababu ulimpata ujanani, mkafunga ndoa mkaishi pamoja.

Sasa anapokuwa mzee, usimchukie, wala usifikirie kumwacha na kwenda kuoa mwanamke mwingine. Hiyo ni dhambi mbele za Mungu.Kwasababu huyo alishakuwa ni mke wa agano lako. Hii inasimama hata kwa upande wa mwanamke. Hupaswi kumwacha mume wa ujana wako, ukaenda kutangatanga na wanaume wengine, kisa wanapesa, au wanavutia, hiyo ni dhambi na ni makosa makubwa.

Vilevile sio lazima mpaka ufikie uzee ndipo Yule awe mke wa ujana wako, hapana, pindi tu unapooa katika ujana wako, hapo hapo tayari kashafanyika mke wa ujana wako. Na biblia inakatazama kuishi na mwanamke/mwanaume ambaye hamjafunga naye ndoa (Girlfriend/Boyfriend), hiyo ni dhambi.

JAMBO HILI LINATUFUNDISHA NINI?

Kanuni hiyo ipo rohoni pia, Sisi kama watakatifu ni (WAKE WA KRISTO), Na Kristo hawezi kutuacha, hata pale nguvu za kuhubiri injili zitakapotuishia pengine kwasababu ya uzee au magonjwa. Ikiwa miaka yote tulitembea naye, tuliishi naye, kamwe hawezi kutuacha hata tutakapoishiwa nguvu.

Ndio maana wote, wanaomcha Bwana, hata mwisho wao unakuwa wa raha, Bwana anawatunza, na kuwahifadhi, na zaidi sana, hata baada ya haya maisha, Kristo bado hawezi kuwaacha, atawakaribisha katika ufalme wake  waishi naye milele.

Swali ni je mimi na wewe tumefanyika kuwa bibi-arusi wa Kristo kwa kuokoka? Kama sio tunategemea vipi, atatukumbuka katika ufalme wake?

Hizi ni siku za mwisho, majira haya ni ya kumalizia, hivyo geuka utubu dhambi zako, ukabatizwe, na Kristo atakuonekania.

Shalom

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *