Kwanini biblia inalitambua kanisa kama mwanamke?

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Hivi umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu alilifananisha Kanisa na mwanamke? Au kwanini Mungu alifananisha mahusiano Yake na Kanisa kama mahusiano ya Mume na mke wake?

Yeremia 31:31
Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, INGAWA NALIKUWA MUME KWAO, asema BWANA.

Umeona hapo mwisho? Anasema “ingawa nalikuwa Mume kwao”

Soma pia katika kitabu cha Hosea sura ya 2 utaona hilo Mungu analiita taifa la Israeli kama mwanamke kahaba kwa sababu wameenda kuabudu miungu mingine

Lakini ukisoma pia katika Agano jipya bado utaona hivyo hivyo kuwa Kanisa ni kama mke wa Kristo

2 Wakorintho 11:2
Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.

Sasa ni kwanini iwe hivyo? Hapo ndio tutajifunza mahusiano ya Mume na mke yapoje.

Siku zote katika jamii zetu na hata Biblia inakiri hivyo kuwa Mwanaume siku zote anataka KUTIIWA na mwanamke na pia mwanamke naye siku zote anataka KUPENDWA na mwanaume. Mwanaume anataka siku zote kuona mke wake anafanya kama alivyomuagiza ndiyo raha yake, kwa mfano; “sitaki uwe unaenda kuzurura kwa mashoga zako nataka utulie nyumbani” au “sitaki chakula kipikwe na mwingine ila wewe tu” na maagizo mengine mengi anayoweza kumpa, sasa mwanamke akitenda kama alivyosema basi mwanaume huwa anafarijika sana kwani mwanaume hata usipompenda sana ila ukimwonyesha kuwa UNAMHESHIMU na UNAMTII basi atakupenda sana.

Mwanamke naye huwa anataka APENDWE yaani awe anapewa muda wa kutosha kwenye ratiba ya mwanaume wake, awe anatimiziwa mahitaji yake kwa wakati, kudekezwa, kupewa kupaumbele zaidi ya wengine wote na mengine mengi.

Sasa mwanaume ukimwonyesha kuwa unampenda ila HAUMTII maagizo yake basi jua upendo wako kwake ni bure na vivyo hivyo mwanamke naye hata ujifanye unamtii kila anachosema ndiyo unachokifanya lakini kama huonyeshi kama unampenda basi jua yote uyafanyayo ni bure tu.

Hebu tusome kwenye Biblia inasemaje kuhusu hili ili turudi kwenye msingi wa somo letu la leo

Waefeso 5:21-25
21 hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.

22 Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.
23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.
24 Lakini kama vile KANISA LIMTIIVYO KRISTO VIVYO HIVYO WAKE NAO WAWATII WANAUME ZAO KATIKA KILA JAMBO.

25 ENYI WAUME, WAPENDENI WAKE ZENU, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

Umeona nafasi ya Kristo kwenye hilo andiko? Bwana Yesu amewekwa kwenye nafasi ya Mume na Kanisa limewekwa kwenye nafasi ya mke, ni kwanini basi?

Hii ni kufunua kwamba jambo kubwa na la muhimu kwetu kama Kanisa ni KUMTII Mungu kwanza katika kila jambo ndiyo mengine yafuate nyuma. Watu wengi ni kweli tunampenda Mungu sana sana kupitiliza hata ukimuuliza leo mtu yeyote kuwa unampenda Mungu atakujibu ndiyo na si kwamba anakudanganya, hapana, anamaanisha kabisa ila tatizo ni kumtii Mungu ndiyo watu wanaposhindwa.

Watu wanakwenda ibadani kwa uaminifu kabisa, wengine hadi ni waimba kwaya Kanisani, wanajihusisha na shughuli zote za Kanisani (kama usafi, ujenzi, kuhudumia watumishi n.k), ni wahudhuriaji wazuri wa mikutano ya Injili, ibada za kusifu na kuabudu zote yupo, simu yake imejaa nyimbo za Injili na pia hadi anavaa cheni ya Msalaba yote hayo ni kuonesha wazi upendo wake kwa Mungu wake.

Lakini leo najaribu kuwakumbusha ndugu zangu ambao tupo katika safari yakuelekea kwa Baba yetu Mbinguni kuwa cha kwanza ni KUMTII Mungu na si kumpenda. Sasa kumtii kunakuwaje?

Kwanza tukumbuke Bwana Yesu alisema yoyote atakaye kumfuata ajikane kwanza nafsi yake mwenyewe na ajitwike msalaba wake ndipo amfuate. Jamani msalaba sio godoro la kulalia bali ni chombo cha kusulubishia sasa ni aliweka wazi kuwa katika kumfuata Yeye kuna mateso utayapitia hivyo uwe tayari kwa hilo.

Utakuta mtu anaenda ibadani na pengine ni muimba kwaya lakini weekend anaingia club

Mwingine mdada ansema ameokoka lakini anavaa mavazi ya kuonesha sehemu za mwili wake ambazo hazipaswi kuonekana (kama mgongo, matiti, mapaja, n.k) na ni kinyume cha maagizo ya Bwana soma 1Timotheo 2:9-10, 1Petro 3-5

Anasema ni mkristo lakini ana boyfriend/girlfriend na anajua kabisa huo ni upagani na ni kinyume na maagizo ya Bwana. Soma Waefeso 5:3

Mwingine anakwenda ibadani anavyotaka yeye na ukimwambia anakuambia kwenda Kanisani sio kwamba wewe ndio mtakatifu sana. Ni kweli wanachosema ila kama kweli unampenda Yesu basi utatii alichosema kuwa tusiache kukusanyika kwa ajili ya ibada. Soma Waebrania 10:25

Mwingine akipata tatizo tu anakimbilia kwa waganga wa kienyeji kuaguliwa na utakuta anamsifia kabisa eti “yule mganga mwaya ni mzuri yaani anakuambia kabisa tumtegemee Mungu, tena amenambia niwe namuomba Mungu sana anisaidie” pumbavu kabisa, Neno limetukataza soma Kumbukumbu 18:10-12

Mtu anasema ameokoka lakini haachi kusikiliza na kutazama miziki, muvi na tamthiliya ya kidunia ambayo hayana mafundisho yoyote ya kiMungu ila maudhui ya mapenzi/kingono, kujiinua, visasi na mashindano. (1 Yohana 2:15)

Hayo na mengine mengi ambayo Wakristo leo wanayafanya na wakikemewa hawataki wanakimbilia kuwa unawahukumu, na kuwa wanaishi ndani ya neema na si chini ya sheria ila Neno lipo wazi kuwa ndani ya Neema sio uhalali wa kutenda dhambi (Warumi 6:15)

Mathayo 7:21
Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT