Karibu tujifunze Neno la Mungu…
JIBU..
Madhabahu ni sehemu ambayo watu hupeleka sadaka zao…Tunaposoma agano la kale tunaona wana wa Israel walipewa agizo na Bwana la kumtolea sadaka, kulikuwa na sadaka za aina mbalimbali mfano sadaka za dhambi, sadaka za shukrani n.k
Na kila sadaka ilitolewa kama sadaka ya kuteketezwa na hapo ndipo ilipolazimu madhabahu itengenezwe, ikiwa na maana kwamba mnyama aliyechinjwa kwa ajili ya sadaka aliweka juu ya kuni ambazo zilkuwa juu ya mawe, kwa hiyo Madhabahu ilitengenezwa kwa kutumia kuni na mawe. Na hiyo ndiyo ilkuwa sehemu ya kumchomea mnyama hadi ateketee bila kusalia kitu.
Habili ndiye alikuwa mtu wa kwanza kutengeneza madhabahu, yeye alipeleka sadaka kwa Bwana kutoka katika wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu za wanyama zilizonona na Mungu akaikubali sadaka yake kuliko ya nduguye Kaini.
Mtu mwingine aliyemtengenezea Mungu madhabahu alikuwa ni Nuhu baada ya kutoka ndani ya safina (Mwanzo 8:20)
Hata Ibrahimu alipotaka kumtolea Mungu sadaka alijenga madhabahu. Biblia inatuambia Mungu alimjaribu Ibrahimu kwa kumtaka amtoe Isaka mwanae sadaka ya kuteketezwa na Ibrahimu alimjengea Mungu madhabahu kwa ajili ya sadaka hiyo.
Hata Yakobo, Musa, Eliya walitengeneza madhabahu kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka. Na madhabahu zilitengenezwa kwa kufuata maagizo maalumu kama Mungu alivyopenda, hawakuruhusiwa kutengeneza madhabahu kama za watu wasiomjua Mungu. Tuangalie baadhi ya maagizo hayo
Kumbukumbu la Torati 27:5-6
[5]Na huko umjengee madhabahu BWANA, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake.
[6]Jenga hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee BWANA, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;
Kuna madhabahu pia iliyotumika kuchomea uvumba ndani ya nyumba ya Mungu. Hii iliitwa madhabahu ya kuvukiza uvumba, aina hii ya madhabahu ilikuwa ndogo kama jiko haikutengenezwa kwa mawe wala kuni.
Tunapoangalia agano jipya madhabahu kama hizo hazipo tena. Kwa sasa mioyo yetu ndiyo madhabahu. Tunapompokea Yesu Kristo ndani ya mioyo yetu, anaingia na kutusafisha kisha anatupa Roho wake Mtakatifu na hapo madhabahu yetu inakamilika kama jinsi Mungu anavyotaka. Na hapo mambo yote yanayohusu ibaada mfano, sadaka, maombi, sala, dua, utukufu,shukrani hukubalika mbele za Bwana…
Zaburi 51:16-17
[16]Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
[17]Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.
Mtu yoyote ambae hakukusafishwa kwa damu ya Yesu moyo wake huwa katika hali ya uchafu ,hali hii haimpendezi Mungu katika jambo lolote
Baadhi watu huiita mimbari ya kanisa kama madhabahu ila kwa uhalisia ile sio madhabahu japo si vibaya kuuita hivyo na kuiheshimu. Maana hapo ndipo neno la Mungu linahubiriwa na tunapeleka matoleo yetu. Na ikitokea likafanyika jambo lolote lililo kinyume na neno la Mungu hiyo ni dhambi na watu wanaweza kupata laana badala baraka. Eneo hilo halitakiwi kuwekewa mapambo kama mishumaa au sanamu kiasi ambacho watu wakaenda kuzisujudia hapo itakuwa ni ibaada ya sanamu tena ni machukizo mbele za Mungu, mimbari inatakiwa kuwa na muonekano wa kawaida.
Mioyo yetu ndiyo madhabahu, haitafaa kuiheshimu madhabahu ya kanisa ikiwa mioyo yetu sio safi,maandiko yanatuambia
Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”
Kuna watu waiogopa na kuiheshimu madhabahu ya kanisa wanashindwa kuiheshimu madhabahu halisi ya mioyo yao sehemu ambayo Mungu yupo karibu yao sana.
Tumwombe Mungu atuwezeshe kusafisha madhabahu za mioyo yetu ili hata maombi yetu na sadaka zetu zikubaliwe mbele yake.
Shalom..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.