Hili ni swali linaloulizwa na watu wengi, kwamba siku ile Kaini alipomuua ndugu yake Habili, biblia inasema alikimbilia nchi ya Nodi. Lakini swali linakuja huko Nodi alitolea wapi mke, wakati kipindi hicho dunia ilikuwa bado haina watu, isipokuwa ni Adamu, Hawa, pamoja na Kaini na Habili peke yao?
Mwanzo 4:13 “Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. 14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. 15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. 16 Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni. 17 Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe”.
Na hii imewafanya watu wengine wadhani kuwa huko Nodi Kaini alipokwenda labda aliona sokwe mmoja mkubwa sana, na ndipo akajipatia uzao kupitia huyo. Mtazamo ambao sio sawa.
Lakini kama si hivyo basi alitolea wapi mke?
Jibu tunalipata katika
Mwanzo 5:3 “Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. 4 Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, AKAZAA WANA, WAUME NA WAKE. 5 Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia kenda na thelathini, naye akafa”.
Unaona hapo? Kumbe Adamu alizaa watoto wengine wakike na wa kiume.
Na moja kati ya hao ndiye aliyekuwa mke wa Kaini. Kumbuka biblia haijaeleza ni wakati gani Kaini alimuua ndugu yake, vilevile haielezi alichukua muda gani mpaka kwenda kuishi nchi ya Nodi..Kwahiyo inawezekana kuwa kipindi cha hapo katikati Adamu alikuwa akiendelea kuzaa watoto wengine, ambao habari zao hazijazungumziwa kwa urefu katika biblia.
Hivyo kwa hitimisho ni kuwa, Kaini hakuoa sokwe, au kiumbe kingine chochote. Bali alimtwaa mmoja wa ndugu zake, akawa mke wake..
Bwana akubariki.