Jibu ni kuwa hatufahamu mtu husika aliyembatiza, lakini ni wazi kuwa na yeye pia “alibatizwa”.
Pengine na mmoja ya wanafunzi wake ,.
Lakini unaweza kuuliza ni kigezo gani, tumetumia mpaka tukajua kuwa na yeye pia alibatizwa?
Tukio la ubatizo linafanana na tukio la Ibrahimu kupewa agano la toraha yeye na uzao wake. Mungu alimwambia Ibrahimu awatahiri wazao wake wote, pamoja na watu wa nyumbani kwake, wote. Lakini utaona pamoja na kuwa alipewa agizo lile, yeye naye hakujitenga kana kwamba halimuhusu. Bali, na yeye pia alikwenda kutahiriwa. Kuonyesha kuwa agano lile, na yeye linamuhusu.
Mwanzo 17:23 “Ibrahimu akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote waliozaliwa nyumbani mwake, na wote walionunuliwa kwa fedha yake, wanaume wote wa watu wa nyumba ya Ibrahimu, akawatahiri nyama ya magovi yao siku ile ile, kama Mungu alivyomwambia. 24 Naye Ibrahimu alikuwa mwenye umri wa miaka tisini na kenda alipotahiriwa nyama ya govi lake. 25 Na Ishmaeli mwanawe alikuwa mtu wa miaka kumi na mitatu, alipotahiriwa nyama ya govi lake. 26 Siku ile ile akatahiriwa Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe”.
Ndivyo ilivyokuwa pia na kwa Yohana mbatizaji, Mungu kumpa ufunuo wa Ubatizo, haimaanishi kuwa na yeye haumuhusu, Hapana.
Hata Bwana wetu Yesu Kristo, japokuwa alikuwa mkuu kuliko Yohana Mbatizaji, alilazimika kujishusha mpaka kubatizwa ili kutimiza haki yote, japokuwa kulikuwa hakuna maana yoyote ya yeye kubatizwa kwani alikuwa mkamilifu lakini ilimpasa abatizwe. Sasa si zaidi Yohana mbatizaji?
Naye pia ni sharti atimize haki yote, na kwamba awe kielelezo kwa wale atakaowabatiza.