SWALI: Je! Ni kweli kuwa mshahara wa dhambi ni mauti tu na sio moto wa milele? Kwasababu maandiko yanasema kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, sasa dhana ya kusema kuwa wenye dhambi wataenda kwenye moto wa milele inatokea wapi wakati maandiko yanasema mwenye dhambi mshahara wake ni mauti tu?
JIBU: Ni kweli kabisa mshahara wa dhambi ni mauti kama maandiko yanavyosema katika
Warumi 6:23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Lakini inabidi tufahamu kuwa, mauti zipo za aina mbili, yaani mauti ya kwanza na mauti ya pili, na mauti ya pili ndo huko kwenye moto wa milele na hii mauti ya pili tunaweza tukaisoma katika
Ufunuo 20:14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.
Soma tena
Ufunuo 21:8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.
Hapo maandiko yana thibitisha kuwa, kuna mauti ya pili ambayo ni ziwa la moto, ambamo ile mauti ya kwanza na yenyewe itatupwa huko, hivyo basi usitegemee kuwa ukitenda dhambi utakufa tu, la! Bali fahamu kuwa kuna hii mauti ya pili ambayo ni ziwa liwakalo moto na kiberiti ambamo kuna mateso milele na milele kama maandiko yanavyothibitisha
Matayo 25:41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;
Soma tena
Ufunuo 20:10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.
Soma tena
2 Wathesalonike 1:8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;
9 watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;
Wewe mwalimu, wewe muhubiri, wewe mwinjilisti, na wewe mchungaji unayewaambia watu kuwa hakuna moto wa milele na kuwafaliji watu kuwa mshahara wa dhambi ni kifo tu, wakati maandiko yamethibisha kuwa kuna moto wa milele, acha mara moja hayo mafundisho yako kwasababu unayaondoa maneno ya unabii na utaondolewa sehemu yako katika ule mti wa uzima
Ufunuo 22:18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
Hivyo dhana ya kusema kuwa hakuna moto wa milele sio sahihi, bali fahamu kuwa ukitenda dhambi na usipotubu basi utakufa na kutupwa katika lile ziwa la moto. Ndugu yangu, muda wa kutubu unao sasa hivi, tubia huo uzinzi wako ulioufanya jana na leo, tubia huo ulevi wako unaoufanya kila siku kwani nafasi unayo sasa, tubia hizo rushwa zako unazozifanya hapo kazini kwako, tubia huo wizi na udokozi unao ufanya hapo kazini, Bwana Yesu anakupenda sana na yupo tayari kukusaidia leo na kukupa uwezo wa kushinda dhambi, hivyo mwamini na ukampokee leo na kubatizwa katika ubatizo sahihi.
Bwana akubariki. Shalom