Nini maana ya wanawake saba watamshika mume mmoja?( Isaya 4:1)

SWALI: Je ni kweli kuna wakati utafika wanawake saba watamng’ang’ania mume mmoja kama ilivyotabiriwa kwenye Biblia?

Isaya 4:1
Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.

JIBU: Bwana Yesu asifiwe sana. Karibu tuzidi kuhabarishana habari njema za Ufalme wa Mungu.

Mimi ni mmoja kati ya watu wengi ambao wanalifahamu hilo andiko toka kwenye Biblia aidha kwa kulisoma au kulisikia kuwa imetabiriwa kuna nyakati zitafika wanawake saba watamfuata mwanaume mmoja ili waolewe na huyo kusitiri aibu yao.

Siku zote nilikuwa najua kuwa kuna wakati utafika idadi ya wanawake itakuwa kubwa duniani hivyo wanawake wengi watakosa wanaume wa kuwaoa na kupelekea wanawake wengi kujipeleka wenyewe kwa mwanaume mmoja awaoe ili wasitirike nao waitwe mke wa fulani.

Kumbe sivyo, Neno halikumaanisha hivyo. Kwanza tujue kuwa, hili Kanisa linafananishwa na mwanamke au mwanamke amebeba ufunuo wa Kanisa katika Biblia [Soma maandiko haya yatakusaidia kuelewa hili; Yeremia 31:31-32, Hosea 2, 2Wakorintho 11:1-2, Waefeso 5:21-32] hivyo andiko hilo ni moja kwa moja linafunua maisha ya kiroho ya Wakristo itakavyokuwa katika siku hizi za mwisho wa dunia.

Ndugu unabii huo umetimia wazi wazi katika Kanisa la Kristo leo kwani matendo ya Wakristo wengi leo yanafunua kilichotabiriwa hapo.

Leo watu hawathamini kabisa wokovu kwa kuishi maisha yale waliyoitiwa kuyaishi ndani ya Kristo bali watu wanachohitaji leo ni ile heshima ya utambulisho wa “Mkristo” tu katika jamii ili asionekane mpagani, wanachotaka tu ni ili wakifa wazikwe na Kanisa kwa heshima, wafungishwe ndoa Madhabahuni wakipata wenzi, wakiumwa au kupitia changamoto yoyote wapate huduma Kanisani kama vile maombezi au ushauri au msaada wa kifedha au msaada mwingine wowote lakini si kumzalia Kristo matunda yoyote katika maisha yao (Yohana 15:1-5)

Bwana Yesu alikuja ili kutuonesha njia ya kwenda Mbinguni maana maisha ya duniani ni ya kitambo tu, lazima tutaondoka hapa na tuendapo baada ya kutoweka katika ulimwengu huu kuna sehemu mbili tu, Mbinguni (kwenye raha ya milele) au Jehanamu yaani ziwa la moto (kwenye mateso ya milele) kama Mungu Baba alivyosema katika Neno lake (Kumbukumbu 30:15) maisha unayoishi leo ndiyo njia yako uliyoichagua mwenyewe uishie wapi kama ni peponi au kuzimu.

Sasa kundi kubwa la Wakristo leo hawamfuati tena Bwana Yesu kama njia (yaani kuishi maisha matakatifu ya kuikataa dhambi kwa kumuangalia Yeye aliekuja duniani ili afanyike kielelezo kwetu jinsi gani tunaweza kuishi kwa kumpendeza Mungu) wala hawataki tena kusikia kweli ya Mungu waishi kwa kuifuata hiyo ili wawe na uzima wa milele bali wanamuhitaji tu waitwe kwa jina lake yaani waitwe Wakristo (yaani wa Yesu) ili waeleweke kwenye jamii ya watu wasije kuonekana wachawi au washirikina, au wapagani, au watu wasio staarabika, jambo hili ndilo Neno lililomaanisha pale liposema; “lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.

Sasa je! Neno pia lilimaanisha nini pale liliposema; Isaya 4:1 “Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, TUTAKULA CHAKULA CHETU, NA KUVAA NGUO ZETU WENYEWE, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.” Ni kivipi watakula chakula chao wenyewe na kuvaa nguo zao wenyewe, maana yake ni nini?

Kama tunavyojua kawaida mwanamke huwa anahudumiwa na mume wake yaani ni haki ya mwanamke kuvalishwa na kulishwa na kupewa huduma zote anazohitajika kuzipata ili kuishi toka kwa mumewe. Sasa Kanisa ni mke (bibi harusi) wa Kristo (2Wakorintho 11:2) hivyo Bwana Yesu ndiye anayelihudumia Kanisa lake kwa mahitaji yote ya mwili na roho (Mathayo 6:31-32) lakini wote tunajua kuwa Mungu huwahudumia watoto wake kwa utaratibu anaoupenda Yeye na hivyo unahitaji subira na uvumilivu kuzifaidi baraka za Mungu kwa sababu anataka kwanza tuutafute Ufalme wake kwa bidii ndiyo hayo mengine yaje (Mathayo 6:33, Waebrania12:14, Kumbukumbu 28:1-10) lakini kwa sababu watu hawataki kutii maagizo ya Bwana kwa kupenda ulimwengu hivyo wanatafuta mambo yao wenyewe bila kumshirikisha Bwana kwa sababu yote wayafanyayo ni machukizo kwa Bwana.

Leo Wakristo hawataki tena kusubiri mke/mume mwema kutoka kwa Bwana, anaenda kuvunja ndoa ya mwingine alafu huyo ndiye anakwenda naye Madhabahuni ili naye apate heshima ya kuwa ana ndoa takatifu iliyobarikiwa na Bwana Yesu. Hivyo hawaihitaji tena Yesu awape mume/mke wanatafuta wenyewe alafu wanataka hiyo ndoa iitwe kwa jina lake Yesu kusitiri aibu yao ya uzinzi wanaofanya.

Wakristo wengi leo wanaenda Kanisani kumshuhudia Bwana Yesu amewatendea makuu kwa kuwapa kazi nzuri kumbe ni waongo wametoa rushwa ya ngono ndiyo wakapata kazi ila wanataka jina la Yesu lihusike ili kusitiri uovu wao waonekane wema

Wanajenga nyumba, wanafungua biashara kubwa kwa pesa za udangaji, kwa pesa za rushwa makazini, kwa pesa za wizi na ujambazi lakini wanataka kuitwa Wakristo ili wafiche uovu wao waonekane wema

Watumishi wa uongo wamejaa siku hizi ambao nyuma ya pazia ni majambazi, wauwaji, wanadhulumu masikini na wamejaa mapato ya udhalimu lakini wanajificha katika jina la Yesu na kutwa kujisifu Madhabahuni kuwa Bwana Yesu anawainua kimaisha kumbe ni uongo.

Hayo ndiyo yanatimiza ule unabii kuwa watamshika mume mmoja (ambaye ni Bwana Yesu) wakisema kula ni juu yetu na kuvaa ni juu yetu lakini tuitwe tu kwa jina lako. Kama na wewe ni mtu wa tabia hizo basi jua tu hayo matendo yatakupeleka kuzimu ni bora uache mara moja na uanze kumwabudu Bwana Yesu katika roho na kweli ili upate uzima wa milele ndugu. Mateso, dhiki, shida ni vya muda tu ni heri uvumilie na Bwana ameahidi kutufuta machozi siku ile atakaporudi (Ufunuo 7:17)

Nakusihi ndugu ajali thamani ya wokovu wako, tafuta kwa bidii sana kumjua Mungu na uishi maisha matakatifu ya kumpendeza Yeye na si kutumia jina la Yesu ili uonekane na wanadamu usije ukaangamia mwisho wa safari.

Bwana akubariki.

One Reply to “Nini maana ya wanawake saba watamshika mume mmoja?( Isaya 4:1)”
  1. I have been blessed with the sermon, be blessed you too. Please if I can find any teaching materials I can appreciate.may the lord bless you all in Jesus name.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *