Je! Na wewe ni kama Belshaza?

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele kwani ni jina ambalo tulilopewa sisi wanadamu ili tuweze kuokolewa kwa hilo

Matendo Ya Mitume 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. 

Kama maandiko yanavyosema kuwa hakuna jipya chini ya jua kumaanisha kuwa tabia zote za wakati ule pia bado zinaendelea hadi sasa hivi katika roho au hata mwilini pia, basi leo nataka tumsome mtu mmoja katika maandiko ambaye anafunua tabia za wakristo wengi leo hii katika siku hizi za mwisho na mtu huyo si mwengine zaidi ya mfalme wa pili wa Babeli aliyeitwa Belshaza

Wakati wa kutawala kwake mfalme huyu, kuna siku aliwafanyia karamu wakuu zake kwa kula na kunywa na kibaya zaidi aliamuru vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo baba yake Nebukadreza alivitoa Yerusalemu na hivyo kuvitumia yeye na wake zake na masuria zake na wakuu wake. Jambo hili lilimchukiza sana Mungu na ndipo mfalme huyu akaona vidole vya mkonko wa mwanadamu vikiandika katika ukuta wa chokaa katika enzi yake na kuamuru waletwe watu ili wapate kumpa fasiri na maana. Hebu tusome kidogo

Danieli 5:5 Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. 

6 Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. 

7 Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme. 

8 Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake. 

9 Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa. 

10 Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. 

11 Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; 

Sasa ukisoma mbele zaidi utagundua kuwa, huyu mfalme aliambiwa kile alichokua anakihitaji lakini yale maovu yake aliyoambiwa ayaache hakusikia, alicho jari yeye ni kutatua tatizo lake lililomsumbua tu, habari za kuacha maovu aliyokuwa akifanya hakusikia. Ndivyo ilivyo kwa wakristo wengi leo hii katika siku hizi za mwisho, wakristo wengi wana tabia kama ya huyu mfalme Belshaza.

Wakristo wengi leo hii wanachojari wao ni kutatua matatizo ya kimaisha lakini habari za kuacha dhambi hawataki kusikia. Utakuta mkristo yupo tayari atumie gharama yoyote ile ili akakanyage mafuta kusudi apate kazi lakini ni mzinzi kupindukia, anachojali yeye ni kutatua hiyo shida yake ya kupata kazi tu na sio kuacha huo uzinzi wake kama vile naye Belshaza alivyojari kupata tafsiri tu lakini habari za maovu aliyokemewa hakuwa na habari nayo.

Leo hii wakristo wanatafuta njia za kutatua matatizo yao ya kiuchumi lakini habari za kuacha ulevi na anasa hawataki kusikia. Wanatafuta njia za kupata suluhisho lao pale kazini kwa kwenda kwa nabii fulani lakini habari za rushwa na wizi wanao ufanya hawataki kusikia, ndugu yangu mkristo mwenzangu, fahamu kuwa huko unapoenda kwa manabii na waganga wa kienyeji kutafuta suluhisho lako kwa maji ya upako na mafuta n.k, jua kuwa utapata tu suluhisho lako lakini mwisho wako utakua mbaya kama ulivyokua kwa huyu mfalme Belshaza. 

Mpendwa unayesoma ujumbe huu, usiwe mwenye tabia kama za huyu Belshaza za kutafuta majibu ya tatizo lako na huku hutaki kusikia na kujirekebisha kwa habari za dhambi zako, ni mara ngapi unasikia kuhusu hayo mavazi yako ya kikahaba na hutaki kuacha? Mara ngapi unasikia kuhusu huo uchawi wako na utaki kuacha? Mara ngapi unasikia uache kwenda kwa hao waganga wa kienyeji na hutaki kuacha? Kutwa unataka kutatua shida zako na uovu wako hutaki kuacha kama huyu Belshaza. Ndugu yangu badilika sasa ukatubu na kama bado hujampa Bwana Yesu maisha yako na kubatizwa katika ubatizo sahihi basi fahamu kuwa huu ndio wakati wa kufanya hivyo, fanya haraka sana kabla uharibifu haujakujia kama ulivyomjia Belshaza. 

Danieli 5:30  Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. 

Bwana akubariki. Shalom 

LEAVE A COMMENT