Je unamtumikia Mungu mahali ulipo?

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu kwa Jina kuu kupita majina yote, Jina la Yesu Kristo. Amani ya Kristo iwe pamoja nawe. Amina.

Watu huwa wanafurahi sana wanapookoka na kufanyika watoto wa Mungu kwa kuwa ndani ya Yesu, ni jambo jema sana kwani hata mimi naifahamu vyema furaha ya Wokovu, yaani ni raha kweli hebu jaribu na wewe uone ambaye bado hujafanyika kuwa wa Kristo.

Mpendwa uliye ndani ya Kristo nakukumbusha kama siyo kukufahamisha (kama ulikuwa hujui) Mungu hakututoa katika utumwa wa dhambi ili tuje kwa Kristo tulale, hapana, bali tumtumike Yeye. Kumbuka maneno ya Mungu aliyomwambia Farao;

Kutoka 4:22
Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;

23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili APATE KUNITUMIKIA,…”

Umeona hapo? Kumbe Mungu hakwenda kuwatoa wana wa Israeli utumwani kule Misri ili awapeleke Nchi ya ahadi wakapumzike, hapana, kumbe nia ya Mungu ni kuwatoa utumwani ili wakamtumikie Yeye Mungu. Unadhani inaishia hapo? Hata sisi wa Agano jipya ni hivyo hivyo Bwana Yesu hakuja kututoa kwenye utumwa wa dhambi ili tuje kustarehe tu katika Wokovu bali tupate kumtumikia Yeye. Bwana Yesu alisema maneno haya;

Mathayo 11:28
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 KWA MAANA NIRA YANGU NI LAINI, NA MZIGO WANGU NI MWEPESI.

Umeona anasema tujitie “nira” yake, kwa ufupi nira ni kamba wanayofungwa wanyama kama ng’ombe ili kuongozwa kufanya kazi kama za shambani kwahiyo inaashiria utumishi. Kumbuka unapokuwa kwenye dhambi unayemtumikia ni shetani kwa matendo yako yote maovu (Warumi 6:16)

Unaweza ukajiuliza mimi siyo Mchungaji, au Muinjilisti, au Muimba kwanya, au Shemasi, au sipo kwenye nafasi yoyote Kanisani ni muumini wa kawaida tu, sasa namtumikiaje Mungu wangu?

Jibu ni tumeitwa tofauti kila mtu Mungu alimuweka katika sehemu na nafasi tofauti ili atumike huko kumletea Kristo matunda. Neno linasema vyote vilifanyika kwa njia yake na kwa ajili yake (Wakolosai 1:16)

Sehemu ya kwanza ya utumishi wako ni mwili wako (muonekano wako) unapaswa umpe Yesu utukufu kikamilifu. Kivipi sasa, kwanza hakikisha uvaaji wako haumpi shetani nafasi ya kujitukuza hata kidogo (kwa msisitizo hata chembe) kwa mfano kijana wa kiume uliyeokoka hupaswi kuvaa milegezo (suruali chini ya kiuno), suruali za kubana wengine hadi nguo inashikana na ngozi (hata mashati), nguo za kuchanika chanika, kuvaa hereni, kusuka nywele au rasta (1Wakorintho 11:14) na mengineyo

Vivo hivyo kwa mwanamke hakikisha unavaa kwa kujistiri; achana na make-up binti wa Yesu jiamini paka mafuta yako ya kawaida au lotion (losheni) ya kawaida isiyobadilisha mwonekano wako wa asili inatosha, achana na kuvaa suruali binti uliyeokoka, usivae nguo zinazoonesha sehemu za mwili wako (kama kifua/matiti, mgongo, mapaja, kitovu/tumbo, hata mabega), achana na nywele bandia (rasta, dreds, mawigi)

Kwanini ufanye hivyo sasa, kuna faida gani? Ukifanya hivyo utakuwa umeruhusu Kristo adhihilishe utukufu wake kwa asilimia mia. Kwa mfano; mdada ambaye atakuwa akifanya hayo Kristo akambariki Mume mzuri mwenye heshima na upendo mwingi kwa mkewe wale ambao walidhani kuvaa kuendana na fasheni za kidunia ndiyo kupata Mume watafumbuka macho kujua kuwa Bwana Yesu ndiye pekee anaeweza kukupa vitu ambavyo fasheni haiwezi kukupa, hivyo hapo utakuwa umemhubiri Kristo pakubwa sana. (Warumi 12:1)

Pili utamtumikia Kristo katika mahusiano yako na watu wengine (jinsi unavyoishi na watu wengine katika jamii). Kwa mfano huwezi kupata kazi bila kutoa rushwa ya ngono (kwa mwanamke) wengine kwa kukosa tumaini inabidi wafanye hivyo ili wapate kazi lakini wewe kwa kuwa unaye Yesu (Jemadari wa vita) hufanyi hivyo wengine watataka kukuona utafika wapi ila watashangaa siku unapata kazi tena nzuri kuliko zao hivyo watatambua kuwa Mungu uliyenaye ni mkuu sana na utawavuta wengi kwa Kristo.

Usiwe na tabia hizi katika jamii ili wajifunze kwako, ulevi, wizi, uchonganishi, mtu wa visasi, uasherati, uongo na mengineyo yote mabaya. Ila uwe mtu wa kupatanisha watu wanaogombana, kufariji wenye huzuni, kusaidia wenye uhutaji, mfano wa adabu njema. Vyote hivyo ukivitenda kwa uaminifu vinahubiri sana. Zaidi ya yote jitahidi kuwahubiria watu wampokee Kristo na waliompokea mzidi kuimarishana; ndugu zako, majirani, marafiki zako na wengine Mungu atakao kujalia kukutana nao.

Tatu ni kuhakikisha kwa nguvu zako zote na kwa maarifa yako yote na kwa mali zako zote unasaidia watumishi wengine wa Kristo kuipeleka injili ya Yesu mbele iwafikie watu wengi zaidi. Kwa sadaka zako (ukiona wahubiri masokoni, barabarani, kwenye daladala, kwenye mikutano, redioni na kwenye TV jaribu kuwaunga mkono kwa chochote ulichojaaliwa. Achana na fikra kuwa wanataka sadaka hilo mwachie Mungu atahukumu mwenyewe), ushauri wako, kutumia muda wako na ikibidi kwenda pamoja nao katika matukio yao kama ni kwaya, au kuhubiri mitaani au kwenye mikutano ya injili na jambo lolote lile la kumhubiri Yesu Kristo.

UFUNUO WA YOHANA 22:12
TAZAMA, NAJA UPESI, NA UJIRA WANGU U PAMOJA NAMI, KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.

Je, unaifanya kazi ya Bwana? Je, unafahamu yu karibu kurudi kwa kuwa hizi ndizo siku za mwisho alizosema atarudi kwa ghafla, maana dalili zote zimetimia? Amka sasa uifanye kazi ya Bwana.

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *