SWALI: Ikiwa yeye ndio mwanzilishi wa ubatizo wa maji tele na akawabatiza watu wengi, swali ni je yeye naye alibatizwa kama wao? Na kama ni ndio je alibatizwa na nani?
JIBU: Katika suala la wokovu, kanuni ya Mungu huwa haichagui cheo cha mtu, ukubwa wa mtu, nafasi ya mtu au kwamba wewe ni mwanzilishi au mfuasi..Hapana.
Maadamu ni agizo linalomuhusu mwanadamu basi wote watashiriki kikombe sawa, kama ni tendo basi wote watalifanya.
Hata Bwana Yesu ambaye yeye hakuwa na dhambi hata moja, maadamu alikuwa katika mwili, ilimpasa aende kubatizwa, kwa Yohana..mpaka Yohana alipomwona akasema wewe ndio ungepaswa unibatize mimi, iweje mimi nikubatize wewe? Lakini Bwana Yesu akamwambia fanya hivi sasa kuitimiza haki yote..
Mathayo 3:13-15
[13]Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.
[14]Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
[15]Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.
Hata katika agano la kale utakumbuka Mungu aliingia agano na Ibrahimu na akampa ishara ya tohara kama uthibitisho wa agano lile.
Akaambiwa awatahiri wazao wake wote…lakini utaona hakuwatahiri hao tu peke yao, bali na yeye pia mbeba maono alitahiriwa awe kama kielelezo na pia kuonyesha kwamba agano hilo linamuhusu hata yeye.
Mwanzo 17:23-26
[23]Ibrahimu akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote waliozaliwa nyumbani mwake, na wote walionunuliwa kwa fedha yake, wanaume wote wa watu wa nyumba ya Ibrahimu, akawatahiri nyama ya magovi yao siku ile ile, kama Mungu alivyomwambia.
[24]Naye Ibrahimu alikuwa mwenye umri wa miaka tisini na kenda alipotahiriwa nyama ya govi lake.
[25]Na Ishmaeli mwanawe alikuwa mtu wa miaka kumi na mitatu, alipotahiriwa nyama ya govi lake.
[26]Siku ile ile akatahiriwa Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe.
Na tohara ya agano la kale inafunua ubatizo kwa agano jipya Hali kadhalika Yohana mbatizaji naye alibatizwa, japo hatuwezi kujua alibatizwa na nani, pengine na mmoja wa wanafunzi wake, au mmoja wa makuhani walioamini injili yake wakageuka.
Lakini hakuishi hivi hivi tu mpaka kufa bila kubatizwa..naye pia alibatizwa katika maji tele.
Hiyo ni kutufundisha kuwa maagizo ya msingi kama hayo hatuwezi kuyaepuka kama tutasema tumeokoka. Inasikitisha kusikia wapo watu na wengine ni viongozi wa makanisa wanasema ubatizo wa maji hauna umuhimu wowote..Hivyo mtu anaweza kuishi bila kubatizwa..
Kanuni za Mungu zipo palepale..kama Bwana Yesu Kristo alibatizwa..iweje wewe usibatizwe?
Tafuta ubatizo..kumbuka ubatizo ni lazima uwe katika maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la YESU KRISTO. sawasawa na Matendo 2:38.
Bwana akubariki.
BWANA