Kusaga meno, ni nini kama inavyozungumziwa katika maandiko?

  Maswali ya Biblia

Kwa kawaida mtu akiumia, pengine kajikata au kapigwa, ni ngumu sana kukaa bila kutokuonyesha Meno yake. Kwasababu kuna uhusiano mkubwa sana katika maumivu na meno ya mwanadamu, kama vile ilivyo uchungu na machozi.

Sasa kile kitendo cha mtu kupata maumivu hayo makali mpaka kufikia hatua ya meno kukutana Pamoja, na kuyapekecha pekecha, huko ndiko kusaga meno kunakozungumziwa katika maandiko.

Mpaka mtu afikie hatua hiyo ya kuyapekecha pekecha meno basi yupo katika kilele cha maumivu makali sana, aidha ya rohoni au ya mwilini au yote.

Maneno hayo Bwana Yesu aliyatumia sana, kuonyesha hali halisi ya Jehanamu na wale watakaoachwa mwisho wa dunia jinsi itakavyokuwa.

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Mathayo 13:41 “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,

42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Ndugu unaweza kudhani maneno haya ni hadithi tu, ukiachwa leo hii katika unyakuo utakumbana na uchungu mwingi sana. Kwasababu tukiachilia mbali dhiki kuu ya mpinga-Kristo, bado kutakuwa na mapigo ya Bwana, ambayo biblia inasema, watu watatamani mawe yawaangukie wafu haraka, kuliko kukutana na hiyo ghadhabu kali ya Mungu mwenyezi (Luka 23:29-30).

Inasikitisha kuona watu wengi leo hii, wanapuuzia wokovu wakidhani kuwa hii dunia itakuwa na muda mrefu sana. Kimsingi dalili zote Kristo alizozitabiri kuhusiana na kurudi kwake zimeshatimia, ni kwamba sisi watu wa karne ya 21 tunaishi tu katika muda wa nyongeza, Parapanda wakati wowote inalia, Kanisa tulilopo kulingana na Kalenda ya Mungu linaitwa Laodikia ndilo la mwisho, na hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili (Ufunuo 2&3).

Jiulize Kristo akirudi leo, halafu akakukuta katika hali hiyo hiyo ya uvuguvugu, utajibu nini kwake siku ile ya hukumu, angali injili umeshahubiriwa, na mambo yote yameshakuwa wazi kwako?

Huu si wakati wa kumwangalia ndugu, au Rafiki, au mzazi, jiokoe nafsi yako, kama ni ulimwengu ukatae macho meupe, kama ni tamaa za ujanani zikimbie kwa nguvu zako zote, kama ni kampani za marafiki wabaya wanaokukosesha waage kwa ujasiri wote. Iokoe nafsi yako, kwasababu muda wowote, saa yoyote, ni unyakuo.

Ikiwa utapenda kumpa Bwana Yesu Maisha yako, leo, basi fungua hapa, kwa ajili ya msaada wa kuokoka, na hakika Atakusamehe dhambi zako leo na kukufanya kiumbe kipya, fungua hapa ndugu yangu >>

https://wingulamashahidi.org/2020/07/22/kuongozwa-sala-ya-toba/

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT