Zamani wakulima walipokuwa wanakwenda kulima na wanyama, hususani ng’ombe, walikuwa wanajua kuwa watakumbana na ukinzani wa baadhi ya hawa wanyama, Kwasababu mara nyingine wapo ng’ombe viburi, ambao walikuwa hawataki kulimishwa, hivyo kila wakati walikuwa wanarusha mateke yao tu, na kuwasumbua sana wakulima.
Hivyo wakulima wakabuni kitu mifano wa mkuki ambacho walikisogeza karibu kabisa na migongo ya ng’ombe, ambacho kilikuwa na ncha kali, kiasi kwamba, ng’ombe akitaka kugeuka na kupiga mateke, alikutana nacho na kilimchoma, Hivyo kuwepo kwa hicho kitu, ng’ombe alikuwa analima kwa utulivu hata kama hataki,. Na huo ndio unaoitwa MCHOKOO. (Tazama katika picha juu)
Sasa tukirudi katika habari ya Mtume Paulo, yeye wakati anakwenda kuwatesa wakristo kule Dameski, alitokewa na Bwana Yesu Njia, ndipo akaambiwa maneno hayo; Tusome.
Matendo 26:12 “Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;
13 Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.
14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.
15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi”.
Umeona? Bwana Yesu anamwambia Paulo,! Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. Yaani kwa lugha rahisi, ni ngumu kwako wewe kushindana na kusudi la Mungu, utajiumiza tu wewe mwenyewe. Unajaribu kurushia ngumi mkuki, ni nani atakayeumia, unajaribu kuzuia upanga kwa mkono ni nani atakayekatika?
Ndivyo Paulo alivyokuwa anafanya, pale alipokuwa anajaribu kuwaua na kuwatesa watakatifu wa Mungu, alikuwa anajiandalia shimo lake mwenyewe.
Hata sasa, wapo watu mengi, na taasisi nyingi, ambazo adui wao wa kwanza ni wakristo. Na wamekuwa wakiwawekea vikwazo, wakiwapiga, wakidhani kuwa wanamkomoa Mungu, kumbe ni kwa hasara yao wenyewe.
Balaama alijaribu kufanya jambo kama hilo kwenda kuwalaani wayahudi, akidhani kuwa amefaulu kwa Balaki, lakini kinyume chake ni kuwa Mungu alikuwa ameshamwandalia malaika wake njiani kumuua. Na kama sio Yule punda kumsaidia, habari yake ingekuwa imeshakwisha. Kwasababu huwezi kumlaani aliyebarikiwa.
Nasi pia tuionapo kazi za Mungu, au watumishi wa Mungu wa kweli , yatupaswa kuwaaacha wala tusishindane nao, kwasababu ni sawa na kuupiga mateke MCHOKOO.
Bwana akubariki.