SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema. “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili”. Je hao kondoo wengine ni wapi? Na Zizi hilo ni lipi?
Yohana 10:16 “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja”.
JIBU: Maneno hayo, Bwana Yesu alikuwa anawaambia wayahudi, ambao ndio alikuwa nao, akiwahubiria wakati ule. Na wote waliomwamini ndio walikuwa kondoo wake, Na pale Israeli ndio lilikuwa Zizi lao.
Ukisoma, Ezekieli 34:13-15, utaona Bwana anawafananisha wana wa Israeli na kondoo wake, na Nchi ya Israeli kama zizi lao.
Ezekieli 34:13 “Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.
14 Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.
15 Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU”.
Hivyo hao kondoo wengine aliokuwa anawazungumzia, ndio sisi watu wote wa mataifa, na zizi letu ndio haya mataifa. Kwahiyo Bwana alikuwa anawapata taarifa wayahudi juu ya neema ambayo itawafikia watu watu wa mataifa baadaye (ambao ndio sisi).
Na kweli tunaona baada ya Kristo, kufa na kufufuka, neema ilianza kuhubiriwa ulimwenguni, kote, na mataifa yote, yakamwamini Kristo, na yenyewe yakahesabiwa kama sehemu ya urithi wa wana wa Mungu.
Wagalatia 3:27 “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. 28 Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu”.
Umeona? Biblia inasema pia katika Waefeso 2:12-14 kwamba;
“kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.
13 Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.
14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, ALIYETUFANYA SISI SOTE TULIOKUWA WAWILI KUWA MMOJA; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga”.
Hivyo, ili mimi na wewe, tuwe sehemu katika zizi hili la Mungu, hatuna budi, kumpa Bwana Yesu Maisha yetu kuanzia sasa,ayaongoze na hiyo inakuja kwa kumaanisha kabisa kutubu na kubatizwa, na kupokea Roho Mtakatifu. Hapo ndipo tunapofanyika kuwa wana wa Mungu kweli kweli, wanaostahili kwenda katika unyakuo.
Bwana akubariki.