SWALI: Kauli hiyo ilimaanisha nini? Kwanini Bwana Yesu asema “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme”
Luka 10:17 “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.
18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.
19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”.
JIBU: Wengi wetu tunaitazama kauli hiyo, kama lile tukio ambalo lilitokea zamani mbinguni. Kipindi ambacho shetani na malaika zake walipokuwa wanapigana na Mikaeli na Malaika zake, na baada ya kupigwa na kushindwa, ndipo akafukuzwa mbinguni, na katika kuondoka kwake akawa anashuka chini, kwa spidi ya umeme. Na hapa Bwana Yesu anakuja kuwaelezea wanafunzi wake kile alichokiona katika vita hiyo. Jambo ambalo ni sahihi kabisa. Sehemu ya pili ya unabii huo ilimaanisha hivyo, Shetani baada ya kuanguka kwake alitupwa chini, soma.
Ufunuo 12:9 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
10 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku”.
Lakini Pamoja na hayo, maana ya kwanza kabisa, katika Habari ile haikuwa vita ya mbinguni. Hapana, bali ya hapa duniani, ambayo ilienda kufanywa na wale wanafunzi 70 wa Bwana, ambao walitumwa waende katika kila Kijiji na mji kuhubiri na kutoa pepo. (Luka 10:1-42)
Na tunaona, walikwenda vizuri kwa mafanikio makubwa, Sasa wakati wanarudi kwa furaha, ili wampe Bwana Repoti za mafanikio yao. Kwamba hata pepo wanawatii.. Hapo ndipo Bwana akawaambia, “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme”.
Yaani mlipokuwa mkihubiri na kutoa pepo, niliziona kazi nyingi za shetani zikianguka kwa haraka sana, mlipokuwa mkikatiza vijiji na miji, kuwaangazia watu nuru, katika ulimwengu wa roho shetani alikuwa anaanguka kwa kasi sana.
Hiyo ikifunua nini?
Na sisi tunapotoka na kuhubiri injili kwa pamoja, Tunapoangaza Nuru yetu kwa wengine, basi tunaziangusha kazi nyingi sana za adui, tunakidhoofisha kiti cha enzi cha shetani duniani, hata kule mbinguni alipokwenda kutushitaki, ni kama tunamfukuza, aondoke huko kabisa kabisa.
Lakini kinyume chake ni kweli, ikiwa tutasema tumeokoka, halafu, hatutaki kuhubiri ni sawa na tunampandisha juu shetani, kwa kasi ya umeme, na hivyo anapata nguvu ya kutushitaki kwa Mungu na vilevile, kuutawala ulimwenguni, Na matokeo yake, maovu kuongezeka, na watu kwenda kuzimu.
Hivyo sote kama maaskari wa Bwana tuamke, tukaihubiri injili, ili ufalme wa Mungu wetu, ukue na kuenea, watu waokoke, watoke katika Kamba za shetani na adui, kwasababu mwisho upo karibu sana.