TAFSIRI YA MITHALI 24:11, UWAOKOE WANAOCHUKULIWA WAUAWE,

Maswali ya Biblia No Comments

JIBU.. Mstari huu una maana mbili,

Maana ya kwanza ni uhai kama ‘uhai’ alionao mwanadamu yoyote,

Kwa tafsiri ni kuwa unapomwona mtu ambaye hana hatia amepangiwa njama za kufanyiwa kitendo chochote kibaya mfano kuuwawa na wewe upo Katika mazingira hayo na una uwezo wa kutoa msaada basi yakupasa ufanye hivyo haraka pasipo kusema kwamba mambo hayo hayakuhusu wewe


Mfano ni yule mtu aliyevamiwa na wanyang’anyi ambao Bwana Yesu aliuzungumzia, baadhi ya makundi ya watu yalipita kando ya mtu huyo, Mlawi alimpita,kuhani naye alipomwona alipita kando, lakini msamaria alipomwona alimuhurumia akampangusa vidonda akamtibu akaokoa uhai wake na Bwana akahitimisha kusema na huu ndio Upendo (Luka 10:25-37)

Jambo hili tunaliona kwa Mtume Paulo, wakati amepangiwa njama za kuuwawa na wayahudi kumvizia ili wamuue,mjomba wake kwa kulifahamu hilo akampasha akida wa kikosi habari hiyo (Matendo 23:12-22).. hivyo huyo mtu amemwokoa karibu na kuchinjwa..

Tunaliona tena kwa Mordekai kwa Mfalme Ahusuero, watu walipopanga njama za kumuua yeye alienda kuwatolea taarifa (Esta 6:1-12),. sawa na Yonathani alivyomtunza Daudi juu ya upanga wa baba yake Sauli ili asiuliwe, hivyo walitambua siri ya andiko hili na wala hawakuona hofu kutoa siri kwa wale wote waliokusudia mabaya juu ya wengine..

Lakini hata kipindi cha sasa vifo vingi vinatendeka kwasababu wengi wa watu wamekuwa ni wasiri wa kuripoti matukio fulani ya kikatili, mtu anaekewa sumu ili adhurike na wewe unafahamu kabisa lakini hutoi Msaada wowote mpka madhara makubwa yanatokea, pindi mwizi anapigwa huna budi kutoa taarifa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe juu yake, lakini unaweza ukasema mimi sihusiki atachomwa moto, kumbuka tu uhai wa mtu unathamani hata kama ana ubaya kiasi gani..

Hivyo tukisema si kazi yetu basi tufahamu kuna huruma tunakuwa tunaipunguza kwa Mungu,ndo mana anaendelea kwa kusema..

Mithali 24:11 “Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.  12 Ukisema, Sisi hatukujua hayo; Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye? Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye? Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?”

Kuwa mtu wa kutoa msaada pale ambapo unaona unahitajika, uthamini uhai wa mtu mwingine..

Lakini  maana ya pili ya mstari huu  ni ule Uhai wa rohoni..

Yapo makundi ya watu ambao adui amewashikilia ili kuwameza, na ukisema uwaache kwa kipindi fulani basi wataangamia kabisa kiroho, mwingine ni dhiki za magonjwa na masumbufu ya maisha haya, mwingine ni msongo wa mawazo na kukata tamaa, mtu mwingine anavutwa kwenye ushirikina na Imani potofu,wote hawa wewe kama Mkristo uliyesimama imara Katika Wokovu huna budi kuwaokoa na kuwasaidia wasipotelee kwenye mikono ya adui ili uwatoe huko..wala usiseme hilo sio jukumu langu..

Yuda 1:22  “Wahurumieni wengine walio na shaka, 23  na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.

Ukionyesha Upendo hu kwa kuwatunza watu uhai wao wa Mwilini na Rohoni,hakika Bwana atakutunza zaidi..

Shalom..

Bwana akubariki..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *