Biblia ni nini? Je Neno hilo lipo katika biblia yenyewe?.

Maswali ya Biblia, Uncategorized No Comments

BIBLIA NI NINI?

Chimbuko la Neno Biblia, ni kutoka katika lugha ya Kiyunani, lenye maana ya “Mkusanyiko wa vitabu vitakatifu” Kikiwa kimoja kinaitwa Biblioni, lakini vikiwa vingi huitwa Biblia.

Na vilizoeleka kuitwa hivyo kwasababu vitabu vya awali vya agano jipya, sehemu kubwa viliandikwa katika lugha hii ya Kiyunani, Kwahiyo vilipokusanywa Pamoja viliendelea kuitwa hivyo hivyo kiyunani Biblia kwa kipindi chote.

Hivyo huwezi kukuta neno hili ndani yake, kwasababu ni Neno la wasifa. {Vitabu vitakatifu}. Hakuna asiyejua hilo. Na ndio maana biblia angalizo kali limetolewa kwa yeyote atakayejaribu kuongeza au kupunguza kitu chochote ndani yake.

Ufunuo 22:18 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki”.

Biblia ni kitabu kilichoandikwa na Mungu mwenyewe kupitia wanadamu aliowachagua kulingana na wakati na majira. Na  sio kitabu chenye mawazo afu fikra za mwanadamu yeyote. Tunalithibitisha hilo katika;

2Petro 1:20 “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu.

21 Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu”.

Ndani ya biblia utakutana na Historia ya mwanadamu, ya  mataifa, na watu wa Mungu, Vilevile utapata uponyaji wa Roho, mwili na Nafsi, Halikadhalika utakutana na Tabiri za mambo yajayo ya siku za mwisho na umilele.

Biblia imegawanyika katika Sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni Agano la Kale. Na Sehemu ya pili ni Agano jipya. Ambayo yote kwa Pamoja yanaunda vitabu 66. Agano la Kale likiwa na vitabu 39, Agano jipya likiwa limeundwa na vitabu 27.

Biblia yote inamlenga mtu mmoja, ambaye ni YESU KRISTO MWOKOZI  wa Ulimwengu. Ikiwa na maana vitabu vyote 66, kwa namna moja au nyingine vinamuelezea Kristo, na ukombozi wake, kwa mwanadamu, yenye ndio kiini cha Vitabu hivyo.

Kulikuweko na vitabu vingine vingi, vijulikanavyo kama vitabu vya Apokrifa, ambavyo vinaaminiwa na baadha ya madhehebu duniani, kwamba vingejumuishwa katika orodha ya vitabu vitakatifu.

Lakini vilisadikika tangu zamani za mitume kuwa havikuvuviwa na Roho Mtakatifu, kwasababu vinakinzana na mafundisho ya msingi Ya mitume, ambayo yalimlenga Kristo Yesu.

Hivyo Hakikisha biblia uliyonayo, inayojumla ya vitabu 66, na si Zaidi. Na vitabu vyenyewe ndio hivi.

Agano la Kale

  1. Mwanzo
  2. Kutoka
  3. Mambo ya Walawi
  4. Hesabu
  5. Kumbukumbu la Torati
  6. Yoshua
  7. Waamuzi
  8. Ruthu
  9. 1Samweli
  10. 2Samweli
  11. 1Wafalme
  12. 2Wafalme
  13. 1Mambo ya Nyakati
  14. 2 Mambo ya Nyakati
  15. Ezra
  16. Nehemia
  17. Esta
  18. Ayubu
  19. Zaburi
  20. Mithali
  21. Mhubiri
  22. Wimbo ulio bora
  23. Isaya
  24. Yeremia
  25. Maombolezo
  26. Ezekieli
  27. Danieli
  28. Hosea
  29. Yoeli
  30. Amosi
  31. Obadia
  32. Yona
  33. Mika
  34. Nahumu
  35. Habakuki
  36. Sefania
  37. Hagai
  38. Zekaria
  39. Malaki

Agano Jipya

  1. Mathayo
  2. Marko
  3. Luka
  4. Yohana
  5. Matendo
  6. Warumi
  7. 1Wakorintho
  8. 2Wakorintho
  9. Wagalatia
  10. Waefeso
  11. Wafilipi
  12. Wakolosai
  13. 1Wathesalonike
  14. 2Wathesalonike
  15. 1Timotheo
  16. 2Timotheo
  17. Tito
  18. Filemoni
  19. Waebrania
  20. Yakobo
  21. 1Petro
  22. 2Petro
  23. 1Yohana
  24. 2Yohana
  25. 3Yohana
  26. Yuda
  27. Ufunuo

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *