Ipo injili iliyoenea sana siku hizi za mwisho wa dunia tunazoishi sasa (maana dalili zote za Bwana Yesu kurudi zimetimia) injili iliyojikita katika kuhubiri mafanikio ya kimwili (yaani kupata watoto, kupata mume/mke, kupata mali/utajiri, kupata kazi, kupandishwa vyeo, na mengineyo).
Sio dhambi kumuomba Muumba wako hayo yote unayoyahitaji maana tumeambiwa “ombeni nanyi mtapewa” ila tatizo lililopo sasa ni pale tunapoigeza injili ya Kristo iletayo wokovu wa roho za watu ili watubu dhambi zao na kuachana na mambo ya dunia hii warekebishe njia zao na kuutafuta utakatifu kwa bidii wakiwa ndani ya Neema ya Yesu Kristo ili wakiondoka hapa duniani waende wakaishi na Mungu wao kwenye raha ya milele lakini sivyo, watu wamepofushwa macho kwa injili ya uongo ya kupokea vitu vya mwilini (pokea gari, pokea nyumba, pokea mtoto, pokea utajiri).
Ndugu Bwana Yesu hakuja kufa msalabani ili wewe upate vitu vya mwilini kwani hivyo watu walivipata hata kabla ya Yeye kuja katika mwili na kuishi pamoja nasi hapa duniani.
Kama ni utajiri mbona Sulemani alipewa na Mungu (Soma 1 Mambo ya Nyakati 1:9-12)
Kama ni kupata mtoto wapo wanawake kama Hana waliomba watoto wakapewa (Soma 1 Samweli sura ya 1)
Kama ni kupata mume yupo Ruthu ambaye alihitaji mume na Mungu akampa (Soma kitabu cha Ruthu chote kwakuwa ni kifupi sana na utajifunza mengi pia)
Kama ni biashara na mafanikio ya kimaisha Yabesi aliomba na Mungu akampa yote (1 Mambo ya Nyakati 4:9-10)
Hayo na mengine yote wanadamu waliyoyahitaji kwa maisha yao ya duniani walimwendea Mungu naye akawapa hata kabla ya Bwana Yesu kuja kutukomboa.
Mungu hamkutuma mwanae wa pekee yaani Yesu kuja kuwapa watu utajiri, au watoto, au ndoa, au vyeo kwa sababu vyote vilikuwepo hivyo ila ili aje aukomboe ulimwengu usije ukaangamia katika ghadhabu ya Mungu sababu ya dhambi (Yohana 3:16)
Wagalatia 1:4
ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.
Bwana Yesu alisema yeye ndio njia, na kweli, na uzima mtu hawezi kumfikia Mungu isipokuwa kwa njia ya yeye Yesu (Yohana 14:6) hivyo nakushauri ndugu mfuate Yesu kama njia ya kwenda kwa Mungu Baba na si kwa ajili ya mambo ya mwili, tunatakiwa kuiga mfano wake Yeye alivyoishi alipokuwapo pamoja nasi hapa ulimwenguni maana hicho ndicho kilichomleta duniani ili kutuonesha ni maisha gani tunapaswa kuishi ili tufanyike watoto wa Mungu.
1 Wathesalonike 4:1
Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana.
2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.
3 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;
4 Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;
5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.
Umeona Neno linavyotuambia jinsi ya kuenenda katika Kristo? Basi tufuate njia hiyo ili tuwe salama hapa duniani na tuwe na uhakika wa kuingia Mbinguni. Tuutafute sana utakatifu kwa bidii maana maandiko yanasema hatutoingia Mbinguni bila kuwa watakatifu (Waebrania12:14)
Mathayo 6:31
Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
33 BALI UTAFUTENI KWANZA UFALME WAKE, NA HAKI YAKE; NA HAYO YOTE MTAZIDISHIWA.
Bwana akubariki.