Hamna haja kukujibu katika neno hili.

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Shalom mpendwa, karibu tuyatafakari maneno ya uzima ili tuzidi kuimarika kiimani katika maisha yetu ya wokovu kwa neema hii ya thamani sana tuliyopewa huku tukitazamia makazi ya kudumu yaani ufalme wa Bwana wetu na Mungu wetu Yesu Kristo kama tunavyosoma katika

Waebrania 13:14  Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. 

Leo nataka tuangalie habari ya watu fulani katika maandiko ambao ni Shadraka, Meshaki, na Abednego harafu tutajifunza kitu fulani kitakacho tusaidia katika safari yetu hapa duniani kama wapitaji. 

Tusome

Danieli 3:14  Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? 

15 Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? 

16 Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. 

Kipindi kile akina Shadraka, na Meshaki, na Abednego walipopelekwa kwa mfalme Nebukadreza kwa kutokuitikii amri yake ya kuanguka na kuisujudia sanamu, mfalme akawaambia kama hawatokubali kutii basi  watatupwa katika tanuru ya moto, sasa waseme kama watakubali kuanguka na kusujudia sanamu lake au la! lakini kama tunavyosoma, watu hawa wa Mungu kwa jinsi walivyokua na imani na Mungu wa Mbinguni na kujua kuwa yeye ndiye atakaye watetea na kuwaokoa basi walimjibu  mfalme kuwa “HAMNA HAJA KUKUJIBU KATIKA NENO HILI” ndugu yangu uliyeokoka na kumwamini Bwana Yesu na unayafanya mapenzi yake, usiogope na wala usife moyo utakapopitia majaribu kutoka kwa mtu katika safari yako ya wokovu, bali jibu lako likawe “HAMNA HAJA KUKUJIBU KATIKA NENO HILI” ukijua kuwa, huyu Bwana Yesu ambaye unayafanya mapenzi yake ndiye atakaye kuokoa.

Unaweza pata majaribu katika familia, Mama akakwambia mbona njia unayoenda unapotea? Mbona watu wengi hawapo kama wewe? Mbona ndugu zako wote hatupo kama wewe, unataka kusema kuwa wewe tu ndo upo sahihi? Mimi nitakuacha ili nione utafika wapi na uko kuokoka kwako. Wewe mpe jibu moja tu kuwa “HAMNA HAJA KUKUJIBU KATIKA NENO HILI” kwani Bwana Yesu huyu aliyenitoa katika utumwa wa dhambi, yeye ndiye atakaye nipigania 

Unaweza ambiwa na bosi wako kazini kuwa, utoe rushwa ya ngono ili upandishwe cheo, kama hutaki sikupandishi cheo, hivyo unakubari kutoa rushwa ya ngono au la! wewe kataa hiyo dhambi ya uzinzi na umpe jibu moja kuwa “HAMNA HAJA KUKUJIBU KATIKA NENO HILI” Bwana atanishindia kwani wazinzi wote sehemu yao ni katika ziwa la moto.

Ndugu yangu uliyemwamini Bwana, endelea hivyo hivyo kupinga matendo yote ya giza kwa kuyafanya mapenzi ya Mungu bila kujari utachukiwa na ndugu au la!  weka tumaini kwake yeye aliyekufanya uache maisha maovu na mwisho wako utakua mzuri  huko Mbinguni au hapa duniani kama ukimkiri Bwana na watu wote watesema kuwa hakika huyu ni mwana wa Mungu, kweli huyu amesimama na Mungu na Bwana atapokea sifa na heshima kama ilivyokua kwa akina Shadraka, Meshaki, na Abednego.

Danieli 3:28  Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. 

29  Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. 

Hivyo ndugu yangu, nakutia moyo katika safari yako ya wokovu kuwa watu wote wanao kusumbua waambie kuwa hamna haja kukujibu katika neno hili kwani Bwana Yesu ndiye ngao yangu.

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *