Shalom, jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele. Karibu katika kuyatafakari maneno ya Mungu, na leo tutaenda kuutazama mfano mmoja ambao Bwana aliusema katika maandiko, na mfano wenyewe ni ule wa wana wawili wa baba mmoja, labda tusome.
Matayo 21:28 Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu.
29 Akajibu akasema, NAENDA, BWANA; ASIENDE.
30 Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, SITAKI; BAADAYE AKATUBU, AKAENDA.
Mfano huo Bwana Yesu aliwatolea wakuu wa makuhani na wazee wa watu baada ya kuona kuwa wana mioyo migumu ya kumwamini japokuwa walikuwa wakifahamika na watu kama watumishi wa Mungu. Sasa kama tunavyosoma kuwa, mtu mmoja mwenye watoto wawili, alimfata mtoto wake wa kwanza na kumwambia nenda kafanye kazi kwenye shamba langu la mizabibu, na yule mtoto akasema sawa harafu asiende. Akamfuata wapili na kumwambia hivyo hivyo, lakini huyu yeye akasema SITAKI ila baadae AKATUBU akaenda.
Kisha baada ya hayo, Bwana Yesu aliwauliza, katika hao ni yupi aliyefanya MAPENZI YA BABA YAKE? Wakasema ni huyo wapili na Bwana akawajibu na kuwaambia “watoza ushuru na makahaba wanawatangulia katika ufalme wa Mungu” kumaanisha kuwa, wao ni watumishi wa Mungu lakini hawataki kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa kumwamini yeye, lakini watoza ushuru na makahaba ambao ni wenye dhambi ipo siku watamwamini Kristo na kutubu dhambi zao na kuyafanya mapenzi ya Mungu; mfano yule kahaba aliyempaka marhamu (Luka 7:37-38)
Matayo 21:31 Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya MAPENZI YA BABAYE? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.
Sasa hii inafunua nini? Wakristo wengi leo hii ni kama huyo mtoto wa kwanza, wamefanyika kuwa wana wa Mungu (sawasawa na Yohana 1:12) lakini hawayatendi mapenzi ya Baba yao, wengi majibu yao NAENDA LAKINI HAWAENDI, wengi wanasema hatufanyi uzinzi lakini wanafanya, hatuli rushwa Baba lakini wanakula, hatusemi uongo baba lakini wanasema, hatuvai vimini na suruali lakini wanavaa nguo zinazoonesha maungo yao, hatutukani lakini wanatukana, hatuendi kwa waganga lakini wanaenda, hatunywi pombe lakini ni walevi, tunawapenda majirani zetu, lakini kutwa kuwasengenya, sisi si wa dunia lakini disco utawakuta.
Lakini wale ambao tunaowaona kama hawana habari na Mungu, hawa wanafananishwa na mtoto wa pili ambaye baadae alitubu na kufanya MAPENZI YA BABAYE. Hivyo kama wewe unajiita mkristo na huyafanyi mapenzi ya Mungu, jua tu yule anayeishi katika dhambi, ambaye anaonekana hafanyi mapenzi ya Mungu, kuna siku atatubu na kuacha dhambi na kuyafanya mapenzi ya Mungu na kukutangulia katika ufalme wa Mungu, kwasababu Bwana alisema yule atakayefanya mapenzi yake ndiye atakayeingia katika ufalme wa Mbinguni
Matayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye MAPENZI ya Baba yangu aliye mbinguni.
soma tena.
Waebrania 10:36 Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya MAPENZI YA MUNGU mpate ile ahadi.
Na mapenzi ya Mungu ni kumwamini Bwana Yesu na kushika maagizo yake kama ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu, kushiriki meza ya Bwana, kutawadhana miguu, wanawake kufunika vichwa wakatwa ibada, kuwa watakatifu nje na ndani n.k
Hivyo mpendwa jitathimini kama kweli unayafanya mapenzi ya Baba aliye Mbinguni au na wewe kauli yako ni NAENDA BWANA LAKINI HUENDI? Kama jibu ni la basi muda unao sasa wa KUTUBU na KUFANYA MAPENZI YA BABA kama yule mtoto wa pili. La sivyo watoza ushuru na makahaba (wasiookoka) watatutangulia
Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema,
Bwana akubariki, shalom.
MADA ZINGINEZO
Nini maana ya kuokoka katika biblia?