WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, Bwana Yesu apewe sifa milele na milele. Ni neema ya Mungu kupata tena wasaa huu wa kuyatafari maneno yake yenye uzima, ambayo kwa hayo mwanadamu hupata uzima yakiwa ndani yake. Kuna mwandishi mmoja ambaye Bwana Yesu alimwambia sentensi moja ambayo nataka tujifunze kutoka kwa hiyo, na maneno ya sentensi hiyo tunayasoma katika kitabu cha Marko, labda tusome.

Marko 12:34  Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo. 

Maana yake ni kwamba, Bwana Yesu alimwona yule mtu kuwa hayuko mbali na ufalme wa Mungu. Sasa ni kwanini yule mwandishi aonekane na Bwana kuwa hayuko mbali na ufalme Mungu? Au ni nini kilichomfanya Bwana kumwambia yule mwandishi maneno hayo? Jibu tunasoma pale pale. 

Marko 12:34  Naye Yesu, alipoona kwamba AMEJIBU KWA BUSARA, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo. 

Kumbe sababu ni kuwa, yule mwandishi ALIJIBU KWA BUSARA, na hadi mtu anajibu kwa busara ni wazi kuwa, kuna hali fulani ya unyenyekevu ndani ya moyo wake kuna hali fulani ya kupondeka ndani yake na Mungu huangalia watu wenye mioyo na roho kama hizo na wala haidharau.

Zaburi 51:17  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; MOYO ULIOVUNJIKA NA KUPONDEKA, EE MUNGU, HUTAUDHARAU. 

Kumbe sasa, na sisi tunahitaji kuwa wanyenyekevu ili tusiwe mbali na ufalme Mungu. Ndugu yangu ambaye bado hujampa Kristo maisha yako, Mungu anataka uwe karibu na ufalme wake kwa kuanza kuwa mnyenyekevu pale unaposikia maneno yake, pale unapohubiriwa injili yake, pale unapohubiriwa kuacha ulevi, pale unapohubiriwa kuacha, chuki, pale unapohubiriwa uache uzinzi na uasherati, kwani faida yake ni kuwa Mungu na yeye atajisogeza karibu na wewe.

Yakobo 4:8  Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. 

Tafadhari washirikishe na wengine habari hizi njema. 

Bwana akubariki, Shalom.


MADA ZINGINEZO

KANISA LA KWELI NI LIPI DUNIANI?


USIBATILISHE KAZI YA MSALABA WA YESU KWA INJILI ISIYOWEZA KUOKOA ROHO ZA WATU.


TAFUTA PESA!  TAFUTA PESA! 

LEAVE A COMMENT