Kumekuwa na aina moja ya mahubiri yaliyoshamiri sana siku hizi, na mahubiri hayo si mengine zaidi ya Manabii, wachungaji n.k kuwahimiza na kuwasisitiza waumini KUTAFUTA PESA. Si kosa mkristo kuwa na pesa na wala si dhambi mkristo kuwa tajiri, lakini aina hii ya mahubiri inapochukua kipaumbele katika kanisa na madhabahu takatifu ya Mungu inakuwa si sawa kabisa, unakuta kiongozi anahubiri na kusisitiza waumini wake kuwa, pesa ndio kila kitu katika maisha yao, kuna mmoja nilimsikia akisema kuwa, ukiwa huna pesa mtu hawezi kuokoka, lakini ukiwa na pesa zimejaa mfukoni, na ukamwambia mtu aokoke, huyo mtu ataokoka tu hata kwa uongo kwasababu tu pesa zipo, kana kwamba nguvu ya pesa ndiyo inayomvuta mtu kwa Bwana Yesu na si nguvu ya Roho mtakatifu tena. Kwa kweli inasikitisha sana. Na bila hao viongozi kufahamu kuwa kwa aina hiyo ya mahubiri wanaweza poteza kondoo wao katika njia sahihi ya Mungu kwani wataamini kuwa, kiongozi wao wa kiroho kawasisitiza kutafuta pesa, na hivyo kusahau kabisa mambo muhimu yanayohusu imani na wokovu wa roho zao.
Waebrania 13:5 Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.
Ndugu yangu, ukiona unahubiriwa injili kama hiyo ya kutafuta pesa katika maisha yako kwa kiwango kikubwa na huku mambo muhimu yanayohusu utakatifu husisitiziwi, basi, anza kutafakari upya, kwani manabii wote na mitume walisisitiza watu kumtafuta Mungu kwa bidii sana, walisisitiza watu kuutafuta uso wa Bwana, walisisitiza watu kutafuta amani na watu wote na utakatifu na wala si pesa.
Amosi 5:4 Maana Bwana awaambia hivi nyumba ya Israeli, NITAFUTENI MIMI, nanyi mtaishi;
1 Mambo ya Nyakati 16:11 Mtakeni Bwana na nguvu zake; UTAFUTENI USO WAKE SIKU ZOTE.
Maandiko yamsema kuwa, tuchunguze kila roho kwani siku hizi za mwisho kuna mahubiri mengi kutoka kwa watumishi wa uongo
1 Yohana 4:1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
2 Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.
Sasa hakuna mtumishi atakaye sema kuwa mimi ni mtumishi wa uongo au akabandika bango na kusema yeye ni nabii wa uongo, lakini matunda yao, na mafundisho yao kama hayaendani na ya Kristo basi hizo roho hazitokani na Mungu.
Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani, kitu alichosisitiza ni habari za toba, habari za watu kuacha dhambi na kumgeukia Mungu, habari za watu kuutafuta kwanza ufalme wa Mbinguni.
Matayo 6:33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
Sio kwamba Mchungaji mkuu na Nabii mkuu, Bwana wetu Yesu Kristo hakujua kwamba watu wanatakiwa kutafuta pesa, alijua lakini aliona hivyo vyote havitamfaidia mtu kuwa navyo hapa na kisha kukosa uzima wa milele.
Marko 8:36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
Watumishi kama hao ambao mawazo yao yameelekea katika mambo ya duniani tu, biblia inatuonya kuto kuwafuata.
Wafilipi 3:18 Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;
19 mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, WANIAO MAMBO YA DUNIANI.
Wewe mchungaji unayesisitiza waumini wako kila jumapili tafuta pesa! Tafuta pesa! Badala ya kufundisha utakatifu na watu kumcha Bwana, Fahamu kuwa si kila anayekuja Kanisani ana haja na pesa, si kila anayekuja Kanisani hana pesa nyumbani kwake, wanazo lakini wameona Mungu ni wa thamani sana katika maisha yao kuliko hizo pesa, wanakuja Kanisani ili wapate msaada wa kumjua Mungu katika maisha, wanataka kupata furaha katika muumba wao, hivyo ni jukumu lako kuwaelekeza katika njia sahihi ya Wokovu wa roho zao.
Bwana akubariki. Shalom.
Mada zinginezo:
Itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni.
Kivipi tunafarakana na imani kwa kutamani fedha?