JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA APOLO.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele na milele. Karibu katika kujifunza maandiko matakatifu na leo tutatazama tabia moja ya Apolo kwenye biblia ambayo itatusaidia na sisi tuliomwamini Bwana kwenye safari yetu ya hapa duniani ya kuutafuta ule mji unaodumu milele kwa neema ya Bwana Yesu kama maandiko yanavyosema katika.

Waebrania 13:14  Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. 

Maandiko yanamweleza Apolo kama MTU WA ELIMU, kumaanisha kwamba, ni mtu mwenye maarifa ya kutosha au kwa lugha rahisi ni mtu aliyeenda shule kweli kweli. Mbali na kuwa mtu wa elimu tu, pia alifundishwa njia ya Bwana na alikuwa ni MTU HODARI KATIKA MAANDIKO, hadi maandiko yanamtaja kama mtu hadari ni wazi alikuwa hodari hasa. Ni kama vile tu uwapo chuoni, inawezekana wote mkawa mnasoma chuo kimoja na fani moja, labda ya udaktari, lakini kuna watu katika hiyo fani ni hodari kuzidi Wengine, ndivyo alivyokuwa Apolo, yaani kwenye suala maandiko alikuwa hodari au THE BEST, na alikuwa akifundisha na kunena habari za Bwana Yesu kwa usahihi kabisa.

Matendo Ya Mitume 18:24  Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, MTU WA ELIMU, akafika Efeso; naye ALIKUWA HODARI KATIKA MAANDIKO.

 25  Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza KUNENA NA KUFUNDISHA KWA USAHIHI HABARI ZA YESU; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. 

Ijapokuwa Apolo alikuwa ni mtu wa elimu, mtu aliyehodari wa maandiko na kufundisha habari za Bwana Yesu kwa usahihi, lakini kuna kitu ambacho alipungukiwa katika uhodari aliokuwa nao, kuna kitu ambacho hakuwahi kukijua kabla hadi hapo alipoelezwa kwa usahihi zaidi na akina Prisila na Akila, na kitu hicho ni yeye kuwa na uelewa wa ubatizo wa Yohana tu.

Matendo Ya Mitume 18:25  Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari  za Yesu; NAYE ALIJUA UBATIZO WA YOHANA TU.

 26 Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, WAKAMWELEZA NJIA YA BWANA KWA USAHIHI ZAIDI. 

Sasa tabia ambayo nataka tujifunze kutoka kwa Apolo ni kuwa WASIKIVU KWA MAMBO TUSIYOYAFAHAMU. Kwa elimu na uhodari wa maandiko aliokuwa nao Apolo ni wazi kabisa angeweza kuwaambia akina Prisila na Akila kuwa, ninyi hamna elimu yoyote kunizidi, ninyi hamjasoma na wala hamyajui maandiko kunizidi. Lakini kinyume chake tunaona kuwa, Apolo na uhodari wake wote alikubali kwenda kwa akina Prisila na Akila na kuelezwa njia ya Bwana kwa usahihi zaidi na kurekebisha ubatizo na baada ya hapo Apolo alifanya kazi ya Mungu kwa kiwango kikubwa sana hadi kupelekea mtume Paulo kumtaja katika barua zake.

1 Wakorinto 16:12  Lakini kwa habari za Apolo, ndugu yetu, nalimsihi sana aende kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi. 

Hii inafunua nini kwetu sisi? Sasa hivi Kuna watu ambao ni kama Apolo, kuna watu ambao wamesoma biblia yoye na kuimaliza, tena zaidi ya hata mara moja, kuna watu ambao wamekalili vifungu vyote vya kwenye maandiko na vipo kichwani hata wakiamshwa saa saba za usiku wanaweza kukutajia. 

Kuna watu ambao wamesoma miaka zaidi ya miwili au pengine zaidi ya saba kwenye chuo cha biblia, hivyo vyote visikufanye wewe kujiona unafahamu kila kitu, inawezekana kuna kitu ukawa unakosa katika uhodari wako, hivyo penda kuwa msikivu na nyenyekevu Kama Apolo, inawezekana Bwana anataka upande viwango vingine zaidi, hebu fikiria kama Apolo angewapuuzia akina Prisila na Akila, ni wazi angekuacamekosa kitu muhimu katika uhodari wake, lakini kwa kuwa msikivu na mnyenyekevu alipata kitu kipya na akaendelea kuwa hodari zaidi.

Hivyo ndugu, unapohubiriwa njia sahihi ya wokovu wa nafsi yako usianze kusema nimesoma miaka mimi kadhaa hivyo huwezi nieleza kitu, nina shahada kadhaa utaniambia nini, bali penda kuwa mtulivu na msikivu kama Apolo ili upokee maarifa ambayo hukuwahi kuwa nayo kabla na Bwana atakutumia katika viwango vingine kwaajiri ya ufalme wake.

Bwana akubariki. Shalom.

Mada zinginezo:

Jifunze tabia hii kutoka kwa mtume Paulo.


JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA KORNELIO


KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?


Kwanini Bwana alisema ‘Ninyi ni chumvi ya dunia’?

4 thoughts on - JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA APOLO.

LEAVE A COMMENT