Shalom, Bwana Yesu apewe sifa ndugu yangu mpendwa katika Bwana. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima maadamu ule mwisho wetu hapa duniani unakaribia.
Leo tutaenda kutazama tabia moja ya mtume Paulo katika biblia na pia kupitia tabia yake tutaangalia ni nini biblia inatuhusia na sisi wakristo wa siku hizi za mwisho, wakristo wa kanisa la Laodikia lenye sifa ya kuwa vuguvugu.
Ukisoma maandiko utagundua tabia moja ambayo mtume paulo alikuwa nayo kabla ya kumwamini Bwana Yesu na pia hata baada ya kumwamini Bwana Yesu. Na tabia hiyo si nyingine zaidi ya kuwa mtu wa BIDII SANA katika mambo yake, hasa kwa yale aliyoyaamini kuwa ni kwaajiri ya Mungu, na ndio maana Mungu alimtumia sana katika kufikisha injili kwa watu wa mataifa.
Alikua na bidii sana katika kushika Amri, sheria na hukumu, ambazo zilikuwapo katika taifa lake na kwa watu wa taifa lake kwa ujumla, mpaka alijishuhudia kwa uwazi kabisa, kuwa, katika kuvishika hivyo, basi hakua na hatia mbele za Mungu kama ni kuhesabiwa haki kwa hivyo.
Wafilipi 3:6 kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, KWA HABARI YA HAKI IPATIKANAYO KWA SHERIA SIKUWA NA HATIA.
Unaweza vuta picha alikuwa ni mtu wa namna gani? Ni wazi alikuwa ni mtu wa BIDII SANA katika kuenenda katika hizo sheria zao. Nadhani hata wewe, usingeweza kusema hivyo kuwa, kama ni kuhesabiwa haki kwa sheria basi, huna hatia mbele za Mungu, ni ngumu sana, lakini Mtume Paulo aliweza na alikuwa binadamu kama sisi.
Lakini pia, hata kile kipindi ambacho yeye na Barnaba walipopewa mkono wa kuume wa shirika na mitume Yakobo, Kefa, na Yohana ili waende kuhubiri injili kwa mataifa, walisisitizwa kuwakumbuka maskini na jambo hilo Paulo alikuwa na BIDII kulifanya kama tunavyosoma.
Wagalatia 2:10 ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; NAMI NENO LILO HILO NALIKUWA NA BIDII KULIFANYA.
Unaona hapo? Ni tabia ile ile ya kuwa na bidii katika mambo yake anaiendeleza hapa baada ya kumwamini Bwana Yesu, kitu ambacho ni kigumu kwa wengi wetu leo hii kuwa na bidii hata katika vile vitu tunavyohusiwa na wazazi wetu kama kusoma tuwapo mashuleni n.k
Vivyo hivyo pia na sisi wakristo, tunapaswa kuinga tabia hiyo ya mtume Paulo ya kuwa na bidii katika maisha yetu ya wokovu, tunapaswa tuwe watu wa bidii katika neema hii tuliyoitiwa, na biblia inatuhasa tuwe na BIDII katika mambo makuu mawili ambayo ni KUWA NA AMANI NA WATU WOTE (upendo) na UTAKATIFU.
Waebrania 12:14 Tafuteni KWA BIDII KUWA NA AMANI NA WATU WOTE, NA HUO UTAKATIFU,ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
Utakatifu unaovungumziwa hapo ni wa mwili na roho yaani utakatifu wa ndani na nje, (si kama wahubiri wengi wanavyohubiri leo hii kuwa Mungu anaangalia roho tu)
2 Wakorinto 7:1 Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.
Sasa utaanzaje kuwa na BIDII katika KUTAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE (upendo) NA UTAKATIFU? Ni rahisi sana. Kwanza kabisa ni kwa kudhamiria ndani yako kuacha dhambi zako zote na kumwamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako, kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu sawasawa na matendo 19:5 Matendo 10:18 na matendo 8:16 na Mungu mwenye lwe atakupa nguvu ya Roho mtakatifu itakayokuwezesha kushinda dhambi na kuishi maisha ya utakatifu huku ukifanya BIDII katika mambo hayo.
Bwana akubariki. Shalom.
Mada zinginezo:
JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA KORNELIO
JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA APOLO.
JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA MITUME ANDREA NA FILIPO.