AKASEMA YASIYO FAA KWA MIDOMO YAKE.

Shalom, jina la Bwana lipewe sifa milele na milele amina. Kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia, utakuwa unafahamu kuwa, Musa mtumishi wa Mungu, hakuwaingiza wana wa Israel katika nchi ya ahadi, kwani, alimkosea Bwana, yeye na ndugu yake Haruni huko kadeshi penye maji ya meriba na hivyo Bwana kumpa adhabu ya kufa na kutowapeleka wana wa Israel ng’ambo ya Jordani.

Kumbukumbu La Torati 32:48  Bwana akasema na Musa siku iyo hiyo, akamwambia, 

49 Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki; 

50 ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe pamoja na watu wake; 

51  kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli.

 52 Kwani utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli. 

Lakini tunaona kuwa, japokuwa Mungu alimwambia mtumishi wake Musa kwamba hatovuka Jordani, lakini bado aliendelea kutembea nae, bado aliendelea kuwa mtumishi wake na hata ikafika wakati, Musa akaenda na kujinyenyekeza mbele za Mungu ili asamehewe na apate kibali cha kuvuka Yordani, lakini Mungu alikataa kama tunavyosoma.

Kumbukumbu La Torati 3:23  NIKAMNYENYEKEA BWANA WAKATI HUO, nikamwambia, 

24 Ee Bwana Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu?

25  NAMI NAKUOMBA NIVUKE, NIKAIONE HIYO NCHI NZURI ILIYOKO NG’AMBO YA  JORDANI, mlima ule mzuri, na Lebanoni.

26  Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili. 

Bwana alikataa shauri la Musa mtumishi wake, na Musa akakosa kuvuka Jordani na kukosa kuingia katika nchi hiyo nzuri, unaweza pata picha jinsi gani mtumishi huyu wa Mungu alivyopata huzuni? Unaweza vuta picha jinsi alivyojisikia alivyoambiwa na Mungu wazi wazi kuwa, huvuki Jordani? Ni wazi kuwa, hakujisikia vizuri na hasa ukizingatia kuwa, kuna  watu ambao waliosababisha hadi yeye na Haruni ndunguye wasiweze kuvuka Jordani, watu ambao hawataki kumcha Mungu, watu ambao hawana hofu na Mungu, watu ambao hawakumbuki matendo makuu ya Mungu, hivyo kumsababishia hasara Musa, kwani waliikasilisha roho yake Musa na kupelekea Musa KUSESEMA YASIYO FAA KWA MIDOMO YAKE.

Zaburi 106:32  Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, HASARA IKAMPATA MUSA KWA AJILI YAO, 

33 KWA SABABU WALIIASI ROHO YAKE, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake. 

Sasa hiyo iliandikwa ili itufundishe na sisi pia, sisi tulio watumishi wa Mungu, kuwa, tunapaswa tujilinde muda wote ili tusinajisiwe roho zetu na watu kwa kutukasilisha na kusema maneno yasiyofaa kwa midomo yetu, kwani, tunaweza kosa thawabu fulani katika maisha yetu kama Musa alivyokosa kuvuka Jordani, ingawa tutaendelea kuwa watumishi wa Mungu. Sasa ni mazingira gani ambayo tukijiweka, kuna uwezeano mkubwa wa  kusema maneno yasiyofaa kwa midomo yetu? Ni pale ambapo tunapoingia katika mabishano ya dini, mabishano ambayo hayana maana na wala hayampi Mungu utukufu, mazingira kama hayo yanaweza kutusababishia kutoa maneno yasiyofaa kwa watu ambao tunabishana nao, na ndio maana maandiko yanatuonya kuwa, tujiepushe nayo.

Tito 3:9  Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.

10 Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; 

11 ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe. 

Bwana akubariki. Shalom.



Mada zinginezo:

Mede ni nini kama tunavyosoma katika Wafilipi 3:14?




LAKINI KWA NENO LAKO NITAZISHUSHA NYAVU.


Je! neno “Mego” linamaana gani katika biblia?


ANAYEENDA JEHANAM/KUZIMU KIBIBLIA (Sehemu ya 01)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *