LAKINI KWA NENO LAKO NITAZISHUSHA NYAVU.

Shalom, Bwana Yesu apewe sifa milele na milele. Ile siku ambayo Bwana Yesu alipotumia chombo cha Simoni Petro kufundishia pale pwani, kuna NENO ambalo alilitamka pale kuwa twekeni hadi kilindini mkavue samaki, labda tusome kidogo.

Luka 5:3  Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.

 4 Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. 

Lakini Petro alianza kumjibu Bwana kwa kumueleza ni kwa namna gani walivyotaabika kwa muda mrefu usiku kucha bila kupata kitu, akanza kumweleza kuwa, walifanya kazi  kubwa mno usiku kucha bila mafanikio yoyote na kusema japo kuwa tumepitia hayo yote usiku kucha bila mafanikio, ila kwa neno lako tu! Tutashusha nyavu, na baada ya petro kushusha nyavu kwa kuamini na kutii neno la Bwana tunaona ni nini kilichotokea pale. Hebu tusome.

Luka 5:5  Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

 6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; 

Umeona hapo kwenye mstari wa 6? Anasema “Basi walipofanya hivyo“ kumaanisha kuwa, baada ya kutii lile neno la Bwana Yesu pale. Sasa ni nini tunajifunza hapo? Tunachojifunza hapo ni kuwa, kuna watu wengi sana leo hii ni kama Petro, wamesumbuka usiku kucha bila mafanikio yoyote, wamesumbuka kwa muda mrefu sana ama na magonjwa au shida mbali mbali, wanazunguka huko na kule kwa kila aina ya waganga wa kienyeji ili wapate suluhisho la matatizo yao huko (wala hawawezi pata  suluhisho huko zaidi ya kumkasilisha Mungu) lakini ndugu yangu nataka nikuambie kuwa neno la Bwana ni hili ambalo unapaswa ulitiii.

Matayo 11:28  Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 

Ndugu yangu, inawezekana umesumbuliwa na dhambi ya ulevi kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote yale katika maisha yako, umetumia kila aina ya madawa bila matokeo chanya yoyote, unachopaswa ni kutii tu neno la Mungu linalosema

Matayo 11:28  Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 

Baba/kaka, inawezekana unasumbuliwa  na tatizo la uvutaji wa sigara kwa muda mrefu, umetumia kila aina ya madawa bila mafanikio yoyote, basi tii leo hii neno la Bwana na kubatizwa katika sahihi na kumpokea Roho mtakatifu ambaye atakayekata kiu yote hiyo ndani yako.

Inawezekana unasumbuliwa na dhambi ya uzinzi na uasherati kwa muda sasa, inawezekana umeathirika na utazamaji wa picha chafu za ngono mitandaoni na huwezi kuacha, inawezekana umeathiriwa na ufanyaji masturbration na huwezi acha, ndugu yangu, tii neno la Bwana leo hii kama wakina Petro walivyofanya. Bwana leo hii anawaita wote walioangaika usiku kucha bila mafanikio yoyote watii neno lake, Bwana anawaambia  kuwa wamkubali yeye leo hii ili awaweke huru, Bwana anawaita leo hii wote waje kwake na kumtwika mizigo yao ili awepe raha nafsini mwao na uzima wa milele uliopo ndani yake.

Matayo 11:28  Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; 

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. 

Ndugu yangu, hilo ndilo neno la Bwana ambalo unapaswa ulitii, kama vile Petro alivyoshusha nyavu kwa neno la Bwana na kupata matokeo mzuri, vivyo hivyo nawe, tii neno la Bwana leo kwa kutubu dhambi zako na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la YESU ili upate ondoleo la dhambi zako na kuwa na raha nafsini mwako.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

Bwana akubariki, Shalom.


MADA ZINGINEZO

NI KWA NAMNA GANI BWANA YESU ALIKUJA KUTIMILIZA TORATI NA MANABII?


Koga ni nini katika biblia?


JE! MAPAMBO YA VITO NI DHAMBI?

2 thoughts on - LAKINI KWA NENO LAKO NITAZISHUSHA NYAVU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *