Koga ni nini katika biblia? 

Neno koga katika biblia tunaweza kulisoma katika vifungu vifuatavyo kwenye biblia.

Yoshua 9:5   na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka NA KUINGIA KOGA. 

Pia katika 

Kumbukumbu La Torati 28:22  Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, NA KWA KOGA; navyo vitakufukuza hata uangamie. 

Lakini pia, utaweza kulisoma tena neno hilo katika vifungu vifuatavyo (Amosi 4:9, Yoshua 9:12)

Koga ni safu/utandu (layer) ambayo husababishwa na viumbe hai vinavyoitwa fangasi, hii safu (layer) hufunika vyakula kama vile mikate n.k na kuvifanya visiwe na uzuri tena, kwa lugha rahisi tunaweza sema ni kama ukungu. Tazama picha

Shetani naye analo koga lake, anao ukungu wake ambao huwafunika wanadamu na kuwafanya wanadamu wakose ubora mbele za Mungu, huwafanya wanadamu wasimfikie Mungu kwa usahihi. Na hili koga (ukungu) la ibilisi lipo hadi sasa miongoni mwa watu wengi, na ibilisi ameliweka koga hili katika fikira za wakristo wengi na kuwafanya wakristo wawe vipofu.

2 Wakorinto 4:3   Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 

4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii [ Ibilisi ] amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. 

Sasa swali ni je! Na wewe fikira zako zimetiwa koga na kupofushwa na ibilisi kiasi kwamba, nuru ya injili ya utukufu wake Kristo haijakizukia?

Paulo anasema kuwa, ikiwa injili wanayoihubiri imesitirika, basi, imesitirika kwa hao wanaopotea ambao ibilisi amepofusha fikira zao. Je! Na wewe ni miongoni mwa hao ambao ibilisi amewapofusha fikra zao kwa koga na kuwafanya kuto kuitii injili ya Yesu Kristo?

Ukijiona hadi sasa Mkristo bado unazisujudia sanamu za Yesu, Maria, n.k kama ishara ya kumweshimu Mungu, na kuwaomba watakatifu walio kufa, injili ambayo Paulo wala mitume wengine hawakuihubiri, basi fahamu kuwa, koga la ibilisi limetanda kwenye fikra zako ili injili ya kweli ya Kristo isikuzukie

Ukiona hadi leo hii mkristo hutaki kukubali unapoambiwa kuacha moyo wako wa kiburi na kutokusamehe wale walio kukosea, kusengenya watu, umbea, matukano, wivu, hasira, uongo, uchawi, na ushirikina, basi fahamu kuwa, ibilisi amepofusha fikra zako kwa koga lake, ili nuru ya Utukufu Wake Kristo isikuzukie

Ukijiona Mkristo tegemeo lako ni chumvi ya upako, mafuta ya upako, maji ya upako, na kila kitu cha upako, na wala hutaki kuwa mwomvaji daima kwa Bwana na kuacha maisha yako ya dhambi, uzinzi na uasherati unao ufanya, rushwa unazotoa na kupokea, nguo zako za nusu uchi na masuruali unayovaa mtaani mwanamke, makucha bandia na makope babdia, basi fahamu kuwa, ibilisi alishapofusha fikra zako

Lakini mbali na hayo yote, Yesu Kristo bado anatupenda, kwani alikufa msalabani kwa ajili yetu, tena hamkatai mtu endapo tukiamua kuziacha njia zetu mbaya na kumgeukia yeye.

Yohana 3:36 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.

Hivyo amua leo kuliondoa hilo koga la ibilisi katika fikra zako, na kutiwa nuru kwa kumwamini Bwana Yesu Kristo kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako zote (kama hukufanya hivyo) na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo sawa sawa na matendo 8:16 matendo 10:48 matendo 19:5 na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu atakayekuongoza katika kweli yote ya kuyafahamu maandiko na kuyaishi.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Mana ni nini katika maandiko?


Kutahayari ni nini katika biblia?


Pazia la Hekalu ni nini katika biblia?


Kupiga panda ni nini katika  (Mathayo 6:2)



Bawabu ni nani na hufanya kazi gani?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *