Asiyeamini amekwisha kuhukumiwa.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Watu wengi leo hii wanatambua kuwa tunaishi katika siku za mwisho kutokana na maasi yalivyokua katika kiwango cha juu sana, kutokana na magonjwa na vita vinavyoendelea katika dunia. Lakini mbali na hicho watu pia wanafahamu kuwa hii dunia itaenda kushushiwa ghadhabu ya Mungu kutokana na uovu wa wanadamu.

2 Petro 3:6  kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. 

7 LAKINI MBINGU ZA SASA NA NCHI ZIMEWEKWA AKIBA KWA MOTO, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. 

Lakini Mungu hapendi watu waangamie, hapendi watu wapotee bali anapenda watu wote waifikilie toba ili wawe na uzima wa milele. 

2 Petro 3:9   Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 

Lakini hainaanishi kuwa endapo watu hawatotubu basi ataghairisha ghadhabu yake, jibu ni la! Kama ambavyo hakughairisha ghadhabu yake wakati wa Nuhu, kama ambavyo hakughairisha ghadhabu yake Sodoma na Gomora ndivyo atakavyofanya na katika hii dunia kwa wale wote watakaokataa wokovu ambao ulikuja duniani kwa njia ya Bwana Yesu ambaye kwa yeye kila atakayemwamini ataokoka na asiyemwamini ni kinyume chake na ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya WAZI WAZI kabisa.

Yohana 3:18  Amwaminiye yeye hahukumiwi; ASIYEAMINI AMEKWISHA KUHUKUMIWA; kwa sababu hakuliamini JINA la Mwana pekee wa Mungu.

Na ndio maana hata wakati anapaa kwenda Mbinguni alisema maneno hayo kwa uwazi tena

Marko 16:16  Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. 

Ndugu yangu ambaye bado upo nje ya Yesu Kristo fahamu kuwa umekwisha hukumiwa kwani nuru imekuja ulimwenguni lakini wewe huitaki hiyo nuru, bado unalipenda giza, bado unapenda anasa, bado unapenda uzinzi na uasherati, bado unapenda miziki ya kudunia inayosifia pombe na uzinzi, inayosifia sigara na bangi, bado unapenda kuonekana wewe ni kama mtu wa dunia hii kwa uvaaji milegezo, nguo za kuchanika chanika, vimini na suruali kwa wanawake, kunyoa Kama watu wa dunia hii, fahamu kuwa ukifa katika hali hiyo ndugu yangu mpendwa itakua ni majuto kwako kwani baada ya kifo ni hukumu (Waebrania 9:27)

Hivyo amua leo katika maisha yako kumwamini Bwana Yesu ili uwe upande salama, mwanimi na kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi na upate ondoleo la dhambi zako kwani usipofanya hivyo utahukumiwa. 

Hivyo kama upo tayari kumpokea, basi ni jambo jema sana, dhamiria kuacha dhambi zako zote katika maisha yako na kisha tafuta kanisa sahihi la kiroho ambalo utaweza pata msaada wa wokovu wako. 

Bwana akubariki. Washirikishe na wengine habari hizi njema. Shalom 


Mada zinginezo:

Je! Umeiamini Injili Ipi?


Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.


Nini maana ya kuokoka katika biblia?


Nini maana ya “ Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana”?


Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)


KUFANYA MATENDO MEMA HAIMAANISHI KUWA UMESHAUPATA WOKOVU

LEAVE A COMMENT