Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)


SWALI: Tukisoma sifa za askofu katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Timotheo, zinasema kuwa, askofu anatakiwa awe mume wa mke mmoja, mpole, n.k lakini pia sifa nyingine inamtaka askofu asifiwe mtu aliyeongoka karibuni ili asije akajivuna na kuanguka katika HUKUMU YA IBILISI. Sasa hiyo hukumu ya ibilisi inayozungumziwa hapo ni ipi? 

1 Timotheo 3:6 Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka KATIKA HUKUMU YA IBILISI. 


JIBU: Hukumu ya ibilisi inayozungumziwa hapo sio kwamba, mtu akiongoka karibuni na kuwa askofu, basi, ibilisi atakuja na kumuhuku mtu huyo, hapana! Bali hukumu ya ibilisi inayozungumziwa hapo, ni hukumu inayofanana na ile aliyoipata ibilisi kutokana na kujivuna kwake. Utakumbuka kuwa, ibilisi alianguka katika hukumu kwa kukosa kwake mbele za Mungu kulikotokana na kujivuna kwake.

Ezekieli 28:17  Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. 

Soma tena

Isaya 14:13  Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. 

Ndivyo ilivyo pia hata kwa watu walioongoka karibuni na kuwa maaskofu. Watu kama hao wana uwezekano mkubwa mno wa wao kujivuna na kujisifia kwa kujiona kuwa ni wa changa na wamepewa jukumu kubwa la kusimamia makanisa. Wanaweza sema “nimemwamini Bwana wiki iliyopita na sasa ni askofu” hivyo kujivuna kwao huko (kutokana na uchanga wao katika imani) kukawapelekea kuanguka katika hukumu hiyo inayofanana na ile aliyoipata ibilisi kutokana na kujivuna kwake. 


Mwangalizi yoyote wa kanisa (askofu) hana budi kuwa mkomavu wa imani kwa kupitia madarasa mbali chini ya Roho mtakatifu. Mfano; mtume Paulo ilimchukua muda kadhaa kuwepo Arabuni na kukaa Antiokia kabla ya kuwa mwangalizi wa makanisa kwa mataifa, Timotheo na Tito nao, walipitia safari mbali mbali na madarasa mbali mbali katika imani kabla ya kuwa waangalizi wa makanisa wakati ambao Paulo alipokuwa mzee, sasa watu kama hawa siku zote ni wanyenyekevu mbele za Mungu na si rahisi kuwa na majivuno hata kidogo kwani wanao uozoefu mkubwa katika imani.


Lakini pia, hata na watu wengine ambao wapo ndani ya wokovu, iwe kwa muda mrefu au kwa muda mchache, hatuna budi kuwa wanyenyekevu na kutokuwa na tabia ya kujivuna ili kuepekana na hukumu ya namna hii iliyompata ibilisi kutokana na kujivuna kwake. Bwana aliweka wazi kabisa juu ya hukumu hii kwa kusema, kila ajikwezaye atashushwa.

Luka 14:11 Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. 

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa, hukumu ya ibilisi inayozungumziwa hapo ni ile hukumu aliyoipata ibilisi kutokana na kujivuna kwake, yaani kushushwa, hiyo ndiyo hukumu itakayo mpata kila ajivunaye na kujikweza

Na sisi tukilijua hilo, hatupaswi tena kuwa watu wa kujivuna na kujisifu mbele za watu kutokana na vipawa vyetu, karama zetu, misaada yetu au neema ambazo Mungu ametupa, hatupaswi kabisa kujivunia na kujitukuza mbele za wenzetu.

Wagalatia 6:4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. 

Bwana akubariki, Shalom.

+255652274252/ +255789001312

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

Mada nyinginezo:

Kupiga panda ni nini katika  (Mathayo 6:2)



UMEFUNGULIWA KAMA BARABA?


Je neno “Mego” linamaana gani katika biblia?


Koga ni nini katika biblia?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *