Nini maana ya “ Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana”?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: biblia inamaanisha nini inaposema “mtafuteni Bwana maadamu anapatikana? “ 

JIBU: hayo maandiko tunaweza yasoma katika 

Isaya 55:6 Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; 

Kwanza tuufahamu kuwa, Bwana yeye siku zote yupo na miaka yake haitakoma na ataendelea kuwepo milele na milele amina kama maandiko yanavyosema katika 

Zaburi 102:27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma. 

Sasa maandiko yanaposema tumfafute Bwana maadamu anapatikana, hapo mlengwa si Bwana bali ni sisi wanadamu. Maandiko yanaposema hivi, yanamaanisha kuwa utafika wakati ambao sisi wanadamu hatutokua na nafasi tena au fursa ya kupata msamaha na fadhili kutoka kwake japokua yeye atakuwepo siku zote. Sasa huo wakati wa sisi kutokupata fursa kwa Bwana umagawanyika katika sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza 

Ni pale mwanadamu unapokufa katika dhambi. Unapokufa katika dhambi kinachofuata moja kwa moja ni hukumu na kutupwa kuzimu kwenye mateso ukingojea siku ya mwisho ufufuliwe na uhukumiwe mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kutupwa katika ziwa la moto. Sasa ukiwa hapo kuzimu huwezi ona tena fadhili za Bwana hutoweza kumpata tena Bwana huko akutoe kwenye hayo mateso lakini wakati huo Bwana ataendelea kuwepo na maisha yatakua yanaendelea duniani kama kawaida. 

Hivyo basi, kwako wewe ndugu yangu, Bwana anapatikana sasa hivi, yaani muda huu ambao unavuta pumzi, kwamaana nyingine ni kuwa mtafute Bwana maadamu bado unaishi, hivyo tubu leo dhambi zako na ukampokee na kubatizwa katika ubatizo sahihi na atakupa uwezo wa kushinda dhambi. Lakini kama usipofanya hivyo na ukafa katika hali ya dhambi basi fahamu kuwa hutokua na nafasi ya kutubu tena. Mtafute Bwana maadamu anapatikana.

Sehemu ya pili

Ni pale ambapo watakatifu wa Bwana watakapokwisha nyakuliwa (unyakuo) na kwenda Mbinguni 

Yohana 14:3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. 

Unyakuo wa watakatifu (kanisa) utakapopita basi fahamu kuwa kinachofuata ni dhiki kuu, muda huo kutakua hakuna kutubu tena kwani Roho mtakatifu atakua ameshaondoka na mpinga kristo atakuwa kapewa madaraka kamili duniani. Sasa wakati huo utakua ni wa mateso sana kwako na Bwana hatopatikana kwako kwa kukupa wewe neema ya pili kwani mlango wa neema utakua umeshafungwa kwa watu wa mataifa hivyo sasa utamtafuta Bwana lakini hatopatikana na ndio maana umepewa shauri sasa umtafute kwani anapatikana sasa hivi. Ndugu yangu, mlango huu wa neema hivi sasa bado upo wazi hivyo Bwana anapatikana sasa hivi, basi tubu leo na ukampokee Bwana Yesu maadamu anapatikana. Lakini fahamu kuwa, inawezekana hata huko  usifike na ukafa kesho mchana, jiulize utakuwa wapi kama hujampokea Bwana? Utaomba rehema kama yule tajiri kule kuzimu lakini hutozipata  tena kwani wakati wa kuomba hizo rehema unao sasa hivi kwani Bwana anapatikana.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

MMEKWISHA KUSHIBA, MMEKWISHA KUPATA UTAJIRI, MMEMILIKI PASIPO SISI.


Ni lini Bwana alivitakasa vyakula vyote kulingana na 1 Timotheo 4:3?


USIMLAANI MKUU WA WATU WAKO.


KWA SABABU NALIWAOGOPA WALE WATU, NIKATII SAUTI YAO. 

Nini maana ya “Msitweze unabii”? (1 Wathesalonike 5:20)

LEAVE A COMMENT