Ni lini Bwana alivitakasa vyakula vyote kulingana na 1 Timotheo 4:3?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: kulingana na maandiko, Mungu aliwaamuru wana wa Israel wasile baadhi ya vyakula kwani vilikuwa ni najisi kwao, lakini baadae mtume Paulo anasema kuwa vyakula vyote Mungu alivitakasa (1Timotheo 4:3)  Sasa ni wakati gani huo ambao hivyo vyakula vilitakaswa?

JIBU: Ni kweli kabisa Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo kuwa, wasile baadhi ya vyakula kwani ni najisi kwao, unaweza soma vyakula na wanyama hao katika kitabu cha (Walawi 11)

Walawi 11:3  Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala. 

Lakini mtume Paulo anasema kuwa, vyakula vyote Mungu alivitakasa ili vipokelewa kwa shukrani na hao walio na imani na wenye kuijua kweli

1 Timotheo 4:3  wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, AMBAVYO MUNGU ALIVIUMBA VIPOKEWE KWA SHUKRANI NA WALIO NA  IMANI WENYE  KIJUA HIYO KWELI. 

Ni kweli kabisa kuwa, sasa hakuna chakula kilicho najisi kwa mwanadamu, ila kama mtu hapendelei kula chakula fulani anaweza asile lakini hakuna kilicho najisi. Mungu aliviita vyakula fulani najisi ili kufunua kitu fulani rohoni, ukitaka kufahamu ni nini Bwana alikuwa anafunua tuandikie ujumbe wako kwenye sanduku la maoni.

Tukirudi kwenye maandiko, biblia inasema kuwa Sheria ya Bwana ipo ndani ya Bwana Yesu (zaburi 40:8) na pia maandiko yalimtabiri  Bwana Yesu kuwa, atakapokuja atawafunulia wana wa Yakobo mambo yote waliyofundishwa

Yohana 4:25  Yule mwanamke akamwambia, NAJUA YA KUWA YUAJA  MASIHI, (AITWAYE KRISTO); NAYE  ATAKAPOKUJA, YEYE ATATUFUNULIA  MAMBO YOTE.

 26  Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye. 

Umeona? Kumbe Bwana Yesu alikuja pia kuwafunulia mambo ambayo Mungu aliyaficha kwao tangu zamani, na jambo moja wapo alilofunua ni hili la vyakula najisi kwa kusema.

Marko 7:14  Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. 

15  Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. 

16  Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] 

Bwana Yesu aliwafunulia hilo jambo hapo, na hakuishia hapo tu, bali aliendelea mbele zaidi na kuvitakasa tena vyakula vyote viwe halali kuliwa kama kule mwanzo alipomuumba  mwanadamu katika bustani ya Edeni

Marko 7:19   kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? KWA KUSEMA HIVI ALIVITAKASA VYAKULA VYOTE. 

Hivyo, kwa neno hilo la Bwana Yesu, vyakula vyote vilitakaswa na wala hakuna chakula kilicho najisi. Kumekua na mafundisho mengi sana siku hizi za mwisho, ambayo yanawazuia watu kula vyakula fulani kwa kisingizio kuwa, mtu akila hivyo hawezi jazwa Roho mtakatifu, ndugu yangu, Roho mtakatifu alishanena wazi wazi kuwa siku za mwisho zitatokea hizo roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani ya kuwaamuru watu wajiepeshe na vyakula fulani ambavyo Mungu alishavitakasa

1 Timotheo 4:1  Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; 

2  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3  wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru WAJIEPUSHE NA VYAKULA, AMBAVYO MUNGU ALIVIUMBA VIPOKEWE KWA SHUKRANI NA WALIO NA  IMANI WENYE  KIJUA HIYO KWELI.

 4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; 5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. 

Dada/kaka, ukiona mchungaji wako anakuamuru ujiepushe na vyakula fulani basi, fahamu kuwa nyuma yake kuna hizo roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani, ukiona kiongozi wako wa dini anakwambia chakula fulani ni najisi fahamu kuwa nyuma yake kuna hizo roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.

Je! Bado unasikiliza roho zidanganyazo? Kama ni ndio acha mara moja ndugu yangu na ukampokee Roho mtakatifu ndani ya maisha yako leo na kukutia muhuri wa Mungu  hadi ile siku ya ukombozi (Waefeso 4:30) kwa kumwamini Bwana Yesu na kuacha dhambi zako zote na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la YESU.

Ubarikiwe na Bwana. Shalom 


Mada zinginezo:

Koga ni nini katika biblia?


Mana ni nini katika maandiko?


MMEKWISHA KUSHIBA, MMEKWISHA KUPATA UTAJIRI, MMEMILIKI PASIPO SISI.


Nondo ni kitu gani katika biblia?(Mathayo 6:19)

LEAVE A COMMENT