USIMLAANI MKUU WA WATU WAKO.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina la Bwana lipewe sifa. Kuna moja ya tabia iliyozoeleka miongoni mwa wakristo leo hii, ambayo si sahihi kuwepo kwetu, na tabia hii si nyingine zaidi ya watu waliookoka kuwasema kwa mabaya viongozi wao. Wengi tumekuwa tukiwaongelea vibaya viongozi fulani kwa lengo la kuwaaibisha na kuwadharaulisha mbele za watu, kwa lengo la kuonesha kuwa hawafai na wengine huenda mbali zaidi na kufikia hata hatua ya kuwaita majina yasiyo faa katika maongezi yao. Ndugu yangu fahamu kuwa si sahihi kufanya hivyo kwani maandiko yanasema hivi. 

Kutoka 22:28  Usimtukane Mungu, WALA USIMLAANI MKUU WA WATU WAKO. 

Mkuu wa watu wako ni mtu yeyote yule ambaye anayo mamlaka fulani juu ya watu, anaweza akawa bosi wako kazini kwako, anaweza akawa mwenyekiti wa kitongoji, anaweza akawa mazazi wako katika familia, anaweza akawa mwalimu shuleni kwako, anaweza akawa mkufunzi chuoni kwako, ilimradi tu anayo mamlaka juu yako na wengine, huyo tayari ni mkuu wa watu wako hivyo hupaswi kumnenea mabaya mbele za watu kwa lengo la kumdhalirisha, haijalishi anakuchukia kiasi gani, haijalishi anakosea kiasi gani, fahamu hupaswi kumnenea mabaya mbele za watu kwani ni Mungu ndiye aliyemtia mafuta kuwa katika hiyo nafasi, ni Mungu ndiye aliyemuweka hapo na  Mungu anafahamu nini anachokifanya kwani kila mamlaka hutoka kwake na kila mtu humchagua yeye kama apendavyo.

Danieli 4:32  Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, NAYE HUMPA AMTAKAYE, awaye yote. 

Unaweza jifunza pia hata kwa  Daudi wakati akikimbizwa na mfalme Sauli, utagundua kuwa Daudi hakufanya kitu chochote cha kumwaibisha sauli kwani alijua huyo ni mtiwa mafuta wa Bwana, alijua kuwa sauli ni mkuu wa watu wake bado. 

Lakini pia unaweza jifunza hata kwa mtume Paulo pale alipopelekwa mbele ya baraza, alipigwa kinyume cha sheria kwa amri ya kuhani mkuu, kisha Paulo akamwambia na Mungu atakuadhibu wewe kwani unatoa amri kinyume cha sheria. Ni kweli, yule kuhani alifanya kosa, na kile Paulo alichomjibu kilikuwa ni sahihi kwa sababu wote wahukumuo kwa udhalimu Bwana atawahadhibu, lakini kwa jibu la Paulo ni wazi kabisa alikua anamuaibisha Kuhani mkuu wa Mungu, lakini paulo hakufahamu kuwa yule ni Kuhani na akakili kwa musema.

Matendo Ya Mitume 23:1  Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi.

 2 Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.

3 Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

 4  Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? 5 akasema, SIKUJUA, NDUGU ZANGU, YA KUWA YEYE NI KUHANI MKUU; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako. 

Hivyo, kama unaona mkubwa wako anachofanya si sahihi, unaweza mfuata kwa hekima sehemu ambayo huwezi mzalilisha na mweleze mapungufu yake na kama hatoelewa basi, lakini sio kwenda kumsema vibaya mbele za watu kwa lengo la kumwaibisha au kumdharirisha.

Bwana akubariki. Shalom.

Mada zinginezo:

Usimkatae (usimwache) Yesu aliye tumboni mwa Mariamu!USIMWACHE ALIYE CHEMCHEMI YA MAJI YA UZIMA.


Nondo ni kitu gani katika biblia?(Mathayo 6:19)


Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)

LEAVE A COMMENT