ONDOENI MIUNGU MIGENI ILIYO KWENU.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Nakusalimu katika jina KUU lipitalo majina yote, jina ambalo mwanadamu aweza kuokolewa kwa hilo akiwa hapa duniani, jina la Bwana wetu na Mungu wetu YESU KRISTO, sifa na utukufu ni wake milele na milele amina. 

Ukisoma maandiko utagundua kuwa, wakati Yakobo alipotaka kwenda uweponi mwa Mungu na kumjengea huko madhabahu, aliwaamuru watumwa wake na kuwaambia ONDOENI MIUNGU MIGENI ILIYO KWENU, hii ni kuonesha kwamba, Yakobo alijua kabisa kuwa, Mungu wake achangamani na miungu mingine.

Mwanzo 35:2 Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, ONDOENI MIUNGU MIGENI ILIYO KWENU, mjisafishe mkabadili nguo zenu. 

3 Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. 

Watu wote wa nyumbani mwa Yakobo, walimtii Yakobo na kuiondoa miungu yao migeni iliyopo kwao.

Mwanzo 35:4  Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. 

lakini unaweza jiuliza kwanini watu hawa waliambiwa waondoe mingu migeni ikiyopo kwao lakini wao wakaondoa na mapete yaliyokuwa masikioni mwao? Je! Hiyo nayo ilikua ni miungu yao? Jibu ni ndio, hivyo vitu vilikuwa na uhusiano  na miungu yao kipindi walipoenda kufanya ibada zao za miungu yao huko, na tunaweza lithibitisha hilo katika

Hosea 2:13  Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema Bwana. 

Umeona? Watu hawa walipoenda uweponi  mwa miungu yao Mabaali ili kuwafukizia uvumba, walijipamba kwa hayo mapete ya masikioni na vito, kuonesha kuwa kuna uhusiano kati ya hivyo vitu na miungu yao na ndio maana Yakobo aliwaambia waiondoe hiyo miungu yao migeni wanapoenda mbele za Mungu aliye hai ambaye achangamani na masanamu.

Lakini pia hata mitume wa Bwana Yesu walisisitiza juu ya miungu hiyo migeni katika kanisa na kuwaonya wateule wa Kristo.

1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, WALA KWA DHAHABU NA  LULU, wala kwa nguo za thamani; 

Mungu hachangamani na miungu mingine ambayo ni masanamu kama Yakobo alivyogundua hicho kitu. Mungu hapendi masanamu katika miili ya watoto wake.

2 Wakorinto 6:16  Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. 

Hivyo Dada/mama uliyeokoka tambua kwamba hutakiwi kuwa na hiyo miungu mingine juu yako uendapo uweponi mwa Bwana, na si uwapo kanisani tu la! Bali muda wote, kwani wewe ni hekalu takatifu la Mungu aliye hai. Hayo mahereni unayovaa mwilini mwako, hiyo mikufu shingoni mwako, hivyo vipini katika pua zako na juu ya macho yako, vyote ni miungu migeni katika mwili wako, vyote ni masanamu katika hekalu la Roho mtakatifu ambalo ni mwili wako hivyo IONDOE HIYO MIUNGU MIGENI ILIYOPO KWAKO.

Bwana akubariki. Shalom.


Mada zinginezo:

Je! Ni dhambi kwa mwanamke wa Kikristo kuvaa suruali?

INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI


Ufisadi ni nini katika maandiko?(Waefeso 5:18)


Kuuza cheni na hereni ni sawa kwa Mkristo?

LEAVE A COMMENT