MSIFADHAHIKE KWASABABU YA DHIHAKA ZAO

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, Jina la Bwana lipewe sifa milele na milele. Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa, watu ambao wameamua kuacha kuishi maisha ya dhambi na kumfuata Bwana, huwa wanaonekana kama ni watu wa ajabu sana, mfano mtu ambaye hakubali kupokea rushwa kazini kwake kwasababu ameokoka, huwa anaonekana ni mtu wa ajabu sana na wafanyakazi wenzake au kaka/dada ambaye ameamua kuacha kuishi maisha ya kwenda club na kampani za uzinzi na ulevi, huwa anaonekana ni mtu ambaye mshamba sana. Hivyo ndivyo ilivyo kwani hata Bwana Yesu alisema kuwa ulimwenguni tunayo dhiki (Yohana 26:33) na dhiki yenyewe inakuja kwasababu tunataka kuishi maisha ya utauwa katika Yesu Kristo 

2 Timotheo 3:12  Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. 

Ndivyo ilivyo katika jamii nyingi sasa hivi, watakatifu ni watu wa ajabu sana kama maandiko yanavyosema katika 

Mika 7:4  Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. 

Mchungaji unayekemea uvaaji vimini,suruali, mawigi, hereni na mapambo ya kila aina, fahamu kuwa utaonekana kama mbigili na michongoma tu. Mwalimu unayekemea uvaaji wa nguo za kubana kwa wanaume, unyoaji mbaya, milegezo, n.k fahamu kuwa utaonekana kama mbigili na michongoma tu, na hii yote ni kwasababu unataka kuishi maisha ya utauwa katika Yesu Kristo 

Hata wewe dada unayekataa kufanya uasherati na bosi wako kwasababu ni uovu, fahamu utaonekana kama mbigili tu, wewe kaka unayekataa kupokea rushwa na wizi wa fedha hapo Kazini kwako, utaonekana kama mbigii tu kwa wafanya kazi wenzako. Lakini usife moyo wala usifadhahike kwasababu yao kama Bwana alivyosema katika 

Isaya 51:7  Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. 

Inawezekana umeacha kuimba miziki ya kidunia na kuamua kumwimbia Mungu, na katika kuacha kwako hali yako ya maisha ikawa si nzuri tena, hivyo wale wenzako uliokua ukiimba nao wakakucheka na kukudhihaki, ndugu yangu, usifadhahike kwa dhihaka zao hizo.

Inawezekana umeamua kuacha kufanya biashara ya uuzaji wa pombe kwasababu umemfuata Bwana, na mambo yako ya maisha yakaenda vibaya na wenzako wakakudhihaki kutokana na hali yako kuwa mbaya, ndugu yangu, usifadhahike kwa sababu ya hizo dhihaka zao, biashara ya pombe haina thamani sana kuliko uzuri ule ujao, pesa za rushwa utakazo kula hazina uzuri kuliko ahadi zile alizotuahidi.

2 Petro 1:4  Tena kwa hayo AMATUKIRIMIA AHADI KUBWA MNO, ZA THAMANI, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. 

Ndugu yangu uliyeamua kumfuata Kristo, usiogope matukano na dhihaka za watu, jipe moyo kwani macho yake siku zote yanawatazama wenye haki na tukishinda tutaviona vitu vizuri sana alivyotuandalia

1 Wakorinto 2:9  lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. 

Hivyo nikutie moyo ndugu yangu, unayepitia dhihaka na mateso mbali mbali katika maisha yako kwasababu tu umeamua kuubeba msalaba wako na kumfuata Bwana Yesu, usife moyo kwani hata watakatifu waliokutangulia walipitia dhihaka kama hizo na wale wajao baada yako watapitia kama hizo tu, hivyo usikate tamaa zidi kusonga mbele ukimtazama Kristo aliye mwanzilishi na muhitimishi wa imani yetu.

Bwana akubariki. Shalom 

Mada zinginezo:

NANYI KWA SUBIRA YENU MTAZIPONYA NAFSI ZENU



Je unamtumikia Mungu mahali ulipo?


USIBATILISHE KAZI YA MSALABA WA YESU KWA INJILI ISIYOWEZA KUOKOA ROHO ZA WATU.


Je! Ni kweli ubatizo wa maji hauna umuhimu tena?

LEAVE A COMMENT