ANAYEENDA JEHANAM/KUZIMU KIBIBLIA (Sehemu ya 01)

Kuzimu, Uncategorized No Comments

Shalom, jina la Bwana lipewe sifa. Karibu tujifunze neno la Mungu kwani ni wajibu wetu ili tupate maarifa ya kutosha na kukamilishwa kwa Roho mtakatifu ambaye ni muhuri wa Mungu (waefeso 4:30) pasipo lawama hadi siku ya kuja Mwokozi wetu. Leo tutaangalia anayeenda jehanam ni nani kibiblia na nini tufanye ili tuwe salama, lakini kabla ya kwenda mbele zaidi, tuweke msingi  wa maneno haya.

     KUZIMU/JEHANAM 

Si kila sehemu palipoandikwa kuzimu kwenye biblia, basi pametumika kuwakilisha Jehanam, hapana. Kuna sehemu neno Kuzimu limetumika kuwakilisha kaburi na kuna sehemu limetumika kuwakilisha shimo n.k mfano

Mhubiri 9:10  Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko KUZIMU uendako wewe. 

Neno kuzimu kwenye huo mstari halijamaanisha kuzimu yaani jehanum la! Bali limemaanisha kaburi (grave). Wengi kwa kutokuelewa hilo, wanatumia andiko hilo kuthibitisha kuwa baada ya kifo hakuna kinachoendelea kwani hakuna maarifa, shauri wala hekima huko kuzimu, wakidhania kuwa ni kuzimu yaani jehanum iliyozungumziwa hapo kumbe sio, bali muhubiri alimaanisha kaburi.

Andiko lingine linalofanana na hilo kwa maana ya kaburi ni hili.

Mwanzo 37:35  Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata KUZIMU. Baba yake akamlilia. 

Neno Kuzimu hapo limemaanisha kaburi (grave) na sio kuzimu yaani jehanum kama baadhi ya watu wanavyodhani. Vivyo hivyo, wengi wanatumia andiko hilo kuthibitisha kuwa, hakuna mateso kuzimu kwa kutokufahamu kuwa, kinachozungumziwa hapo ni kaburi na sio kuzimu yaani jehanum 

Unaweza soma mistari mingine kwenye biblia ambayo inamaanisha kaburi lakini imeandikwa kuzimu Ayubu 14:13  Zaburi 31:17

Vifungu vinavyoelezea shimo lisilokuwa na mwisho (bottomless pit) kama Kuzimu. Ufunuo 9:1 ufufuo 9:2  ufunuo 9:11 Ufunuo 11:7  Ufunuo 17:8 

Lakini neno Kuzimu linatumika pia kuwakilisha jehanum (hell)  ikiwa na maana kuwa, kuna sehemu utakuta kumendikwa Kuzimu, lakini ikimaanisha jehanam (hell) kule ambapo Bwana wetu Yesu Kristo alishuka na kuchukua funguo za huko na mamlaka yote. Mfano

Ufunuo 1:18  na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za KUZIMU. 

Neno Kuzimu hapo halijatumika kuwakilisha kaburi (grave) bali jehanum (hell). soma tena.

Zaburi 16:10  Maana hutakuachia KUZIMU nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. 

Hapo Kuzimu imetumika kuwakilisha jehanum (hell) kule ambapo Bwana alishuka, na huo ulikuwa ni unabii wa kufufuka kwake kutoka Kuzimu. Neno Kuzimu (hell) kwa sehemu kubwa limetumika au linatumika kuwakilisha jehanum (hell) na tunaweza sema kuwa Kuzimu na jehanum ni sehemu moja ( hell) 

Lakini sio kila sehemu kwenye biblia palipoandikwa Kuzimu, basi humaanisha kuzimu yaani jehanum, hapana. Na Wengi wanashindwa kuelewa hiki kitu na kufikia hatua ya kufundisha watu kuwa, mtu akifa hakuna kinachoendelea kwa kutumia vifungu vinavyotaja Kuzimu pasipo kufahamu sio Kuzimu ya jehanum iliyozungumziwa bali ni kaburi (grave) kama tulivyoona.

Ni sawa na neno BAHARI kwenye biblia, kiuharisia kuna SEA na OCEAN na kuna utofauti kati ya hivyo, lakini kwenye biblia vyote ni bahari. Ndivyo ilivyo na huko pia, kuna kaburi, jehanum, shimo lisilo na mwisho (bottomless pit) lakini utaona vyote hivyo vinatajwa kama Kuzimu.

Hadi hapo utakuwa unaweza kutofautisha neno Kuzimu wakati usomapo maandiko, basi fuatana nami katika sehemu ya pili ya makala hii.

Bwana akubariki. Shalom 





Mada zinginezo:

ANAYEENDA JEHANAM/KUZIMU KIBIBLIA (Sehemu ya 02)

Je! Ni kweli mshahara wa dhambi ni mauti na si moto wa milele?

Je! Ni kweli majuma sabini aliyoambiwa Daniel yamekwisha timia?(Daniel 9:23-27)

Je! Ni sawa kuwa na sala au maombi maalum kwa Malaika fulani kibiblia?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *